HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, 24 July 2018

MCHAKATO WA TUZO ZA MWAJIRI BORA WAANZA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.
CHAMA cha Waajiri Tanzania (ATE) kimezindua rasmi tuzo ya Mwajiri  Bora kwa mwaka 2018 ili kutathmini mchango wa rasimali watu kwa kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika utendaji wa masuala mbalimbali ya kibiashara.

Tuzo ya Mwajiri Bora (EYA) lilianzishwa mwaka 2005 na kuendeshwa kila mwaka na chama cha waajiri Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa ATE Dkt Aggrey Mlinuka amesema kwamba tuzo ya mwajiri bora wa mwaka imelenga zaidi kuwatambua wanachama waliofanya vizuri katika kuweka mikakati bora yenye kutathmini usimamizi wa rasilimali watu na shughuli za kibiashara.

Dkt Mlinuka amesema kwa miaka kadhaa tuzo hizo zimehamasisha makampuni wanachama kuweka juhudi katika masuala ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu kama msingi mkakati wa makampuni yao kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, furaha, ushindani na yenye kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

Amesema, kutokana na maoni yaliyotolewa na wanachama, wadau na wataalamu mbalimbali tuzo ya mwajiri bora kwa mwaka jana ilihusisha tuzo 8 zaidi ili kuendana na mazingira ya kibiashara kwa sasa ikiwemo uwiano wa kazi na maisha, mwajiri bora ni yule anayesimamia vema nguvu kazi inayoonekana kupotea, waajiri bora ni wenye mikakati inayojali afya za waajiri.

Mengine ni tuzo ya utofautishwaji na ushirikishwaji, waajiri bora ni wanaowachochea na kuwajali waajiriwa wenye ujuzi, waajiri bora wenye mahusiani mazuri baina ya waajiri na waajiriwa, waajiri bora wenye majina makubwa na imara huvutia wateja, waajiri, wadau na mwajiri bora ni yule aliyewekeza kwenye teknolojia.

Ameeleza kuwa, tuzo hizo zinasimamiwa na kampuni ya TanzConsult inayoongozwa na Prof Beautus Kundi na wanachama watatakiwa kuanza kujaza fomu hizo kupitia tovuti ya tuzo ya waajiri ambapo baadae mwaka huu Mwezi Desemba mshindi atapatikana.
Mkurugenzi Mtendaji wa  Chama cha Waajiri (ATE) Dkt Aggrey Mlinuka akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa tuzo ya Mwajiri bora kwa mwaka 2018 itakayofanyika Desemba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad