HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, July 21, 2018

LUGOLA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA IDARA ZILIZO CHINI YAKE

*Pia akerwa na tabia ya wahalifu kupanga ratiba, ataka kazi zifanye saa 24 


Na Said Mwishehe, Globu ya jamii 

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi Kangi Lugola ametoa maagizo kadhaa kwa idara mbalimba zilizopo chini yake kuhakikisha wanayatekeleza kwa maslahi ya nchi. 

Ametoa maagizo hayo leo jijini Dar es Salaam wakati anatoa tathimini ya ziara yake aliyoifanya katika vyombo vya vyote vya ulinzi na usalama na idara zote za wizara hiyo. 

Amefafanua katika ziara yake aliyoianza Julai 11 mwaka huu yako mambo ambayo ameyabaini na hivyo ameona haja ya kuyaeleza kwa mustakabali wa ustawi wa Taifa kwa ujumla. “Miongoni mwa mambo ambayo nimeelekezwa na Rais Dk.John Magufuli ni kuhakikisha anasimamia suala la Magereza kujitosheleza kwa chakula. 

“Hivyo nimeagiza Jeshi la Magereza nchini kuwasilisha mkakati madhubuti na unaotekelezeka wa kujitosheleza kwa chakula ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kulisha wafungwa,”amesema. 

Akifafanua katika hilo amesema kuwa kama mkakati huo kutakuwa na kipengele kinachoweka vikwazo kwa wafungwa kutofanya kazi za kuzalisha basi katika Bunge la Septemba wataanza kwa kuweka kipengele ambacho kinaelekeza wafungwa kufanya shughuli za uzalishaji chakula. 

“Mbona walioko majumbani wanalima kwa ajili ya kupata chakula kwanini waliko magerezani wasilime chakula kwa ajili yao na ikiwezekana kupata na ziada kwa ajili ya kulisha maeneo mengine,”amesema. 

AGUSIA VITU HATARISHI GEREZANI 

Wakati huo huo Lugola amesema ili kukomesha vitendo vya kuingiza vitu hatarishi magerezani ikiwemo simu za mkononi tayari ametoa maagizo kwa Kamishna Jenerali wa Magereza kusimamia kikamilifu nidhamu ya askari wake wenye wajibu mkubwa katika kukomesha vitendo hivyo vya kihalifu. 

“Katika kikao changu na maofisa wa Magereza , nimezungumza na CGP kuwa gereza lolote ambalo linapatikana na matukio hayo Mkuu wa Gereza awatajibika. 


UTATUZI AJALI ZA BARABARANI 

Pia Waziri Lugola amesema katika utatuzi wa ajali za barabarani ambazo zimekuwa tatizo kubwa kwa kupoteza maisha ya Watanzania na kuacha majeruhi amesema tayari amevunja baraza la Taifa la Usalama barabarani na kamati zake za mikoa na wilaya ili kuanza upya. 

“Kabla ya mwisho wa mwezi huu nitakuwa nimeshaunda baraza jipya.Aidha nimeagiza Jeshi la Polisi nchini kuongeza juhudi katika usimamizi wa Sheria ya usalama barabarani na ukaguzi wa magari ili kudhibiti ajali. 

“Hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kutotii sheria za usalama barabarani na kuendesha magari mabovu yanayosababisha ajali na kusababisha vifo,”amesema. 

Aidha amesema amesema kumekuwepo na kero ya muda mrefu ya askari na watumishi raia kutobalishiwa mishahara baada ya kupandishwa vyeo. 

“Nimewaagiza wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama na idara zote ndani ya Wizara hii ifikapo mwisho wa Agosti kero zote ziwe zimetatuliwa na  asiwepo askari wala raia ambaye analipwa mshahara tofauti na cheo chake au kutolipwa mashahara kabisa,”amesema. 


KUHUSU WAKIMBIZI 

Wakati huohuo Waziri Lugola amesema ametoa maagizo kwa Idara ya Huduma za Wakimbizi kuongeza kasi ya kurejesha wakimbizi wa Burundi kwani hali ya amani kwenye nchi hiyo imerejea. 

Pia ametoa maagizo kuhakikisha wakimbizi wote wasioishi kambini warejeshwe kambini mara moja. 

HITAJI LA KUFANYA KAZI SAA 24 

Pia Waziri Lugola amesema kwa suala la usalama wa raia na mali zao ni jambo muhimu kwa Watanzania ambao wanahitaji kufanya kazi saa 24 ili kuendana na azma ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati. 

Amesema tayari ametoa maelekezo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini kuwalisha mkakati wa kuimarisha usalam ili watanzania waweze kufanya shughuli za kiuchumi na kijamii kwa saa 24 wakiwa na uhakika na usalama wao na mali zao. 

“Hatuwezi kupewa amri , maelekezo na ratiba za kazi zetu na wahalifu.Gari inatoka Kagera na kasha inapita Mwanza eti ikifika Morogoro inaambiwa haitakiwi kusafiri usiku kwasababu ya kufohia usalama.Hii haiwezekani.Tutakaa na wadau wa usafiri ili nao utapate maoni yao na kasha tutaamua,”amesema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad