HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, July 16, 2018

KIVUKO CHA MV. NYERERE CHAFUNGWA INJINI MPYA

Na Theresia Mwami - TEMESA
Kivuko cha MV. NYERERE kinachotoa huduma kati ya Bugorola na Ukara katika Wilaya ya Ukerewe Mkoani Mwanza, kinafungwa injini mpya tangu kununuliwa kwake na kuanza kutoa huduma mwaka 2004.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bugorola, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Dkt. Mussa Mgwatu alisema kivuko cha MV. Nyerere kinafungwa injini mbili mpya zenye thamani ya shilingi milioni 191 ili kuongeza ufanisi wa kivuko katika kutoa huduma kwa wananchi wa Bugorola na Ukara. Dkt. Mgwatu amewaagiza mafundi wanaofunga injini hizo wafanye kazi usiku na mchana ili waweze kukamilisha ufungaji wa injini mapema iwezekanavyo ili kivuko kiendelee kutoa huduma ya usafrishaji wa abiria na mali zao.

 Aidha, Dkt. Mgwatu amesema Serikali imedhamiria kuimarisha usafiri wa vivuko katika Ziwa Viktoria kwa kujenga vivuko vipya vitakavyotoa huduma katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Kigongo, Busisi, Kayenze, Bezi, Chato, Bwina, Bukondo, Senga, Muharamba, Kikumbaitale, Izumacheli na Nkome pamoja na kuvifanyia ukarabati vivuko vya MV. Nyerere, MV. Misungwi, MV. Sengerema na MV. Sabasaba.

Nae meneja wa vivuko TEMESA Mhandisi Hassan Karonda amebainisha kuwa mifumo ya injini ya kivuko cha MV. NYERERE imechoka sana kwa sasa kwa kuwa ni ya muda mrefu. Alisema, injini mbili mpya pamoja na giaboksi zinazofungwa katika kivuko cha MV. Nyerere ni za aina ya Perkins zenye nguvu ya kilowatt 161 kila moja na zinafungwa na mafundi wa TEMESA kwa kushirikiana na wale wa kampuni ya Delta Industrial Equipment Limited. Aliongeza kuwa kazi ya kufunga injini itaenda sambamba na kazi ya kukipaka rangi kivuko hicho na baada ya hapo kivuko kitaendelea kutoa huduma kama hapo awali lakini kwa kasi zaidi.

Kivuko cha MV. Nyerere kina uwezo wa kubeba tani 25 sawa na abiria 100 na magari 3 kwa wakati mmoja. TEMESA inasimamia uendeshaji wa vivuko 30 vya serikali vilivyoko kwenye jumla ya vituo 19 Tanzania bara.
 Kivuko cha MV. NYERERE kinachotoa huduma kati ya Bugorola na Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, kikiwasili upande wa Bugorola kutokea Ukara. Kivuko hiki kinafungwa “engines” mbili mpya aina ya Perkins pamoja na “gearbox” zake zenye uwezo wa kilowatt 161 kila moja, ili kukiongezea kasi pamoja na kuondoa changamoto ya moshi unaotoka pindi kinapotembea. MV. NYERERE ilijengwa mwaka 2004, inauwezo wa kubeba tani 25 ambazo ni sawa na abiria 101 na magari matatu.
   Abiria wakiwasili katika eneo la Bugorola wakitokea kisiwani Ukara wilayani Ukerewe Mkoani mwanza. Kivuko hiki kinafungwa “engines” mbili mpya aina ya Perkins pamoja na “gearbox” zake zenye uwezo wa kilowatt 161 kila moja, ili kukiongezea kasi na kuondoa changamoto ya moshi unaotoka pindi kinapotembea. MV. NYERERE ilijengwa mwaka 2004, inauwezo wa kubeba tani 25 ambazo ni sawa na abiria 101 na magari matatu.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Dkt. Mussa Mgwatu (mwenye Kaunda suti nyeusi) akikagua “engine” moja wapo kati ya mbili zitakazofungwa kwenye kivuko cha MV. NYERERE zenye uwezo wa kilowatt 161 kila moja, ili kukiongezea kasi na kuondoa changamoto ya moshi unaotoka pindi kinapotembea. MV. NYERERE ilijengwa mwaka 2004, inauwezo wa kubeba tani 25 ambazo ni sawa na abiria 101 na magari matatu.

Picha na Theresia Mwami - TEMESA

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad