HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 19 July 2018

DCB YATANGAZA KUPATA FAIDA YA SH. BILIONI MOJA

Said Mwishehe,Globu ya jamii
BENKI ya Biashara Dar es Salaam(DCB) imetangaza kupata faida ya Sh.bilioni moja katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018 ambacho kimeishia Juni.

Akizumgumza leo Dar es Salaam Mkurugenzi wa Fedha wa DCB Zacharia Kapama amesema faida hiyo ni ongezeko la asilimia 106 kutoka faida ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2017.

"Ongezeko hilo la faida pia lilipatikana kutokana na kuimarika kwa mapato yatokanayo na riba pamoja na yale yasiyotokana na riba.

"Na limechagizwa na mkazo wa benki katika amana za gharama nafuu, usimamizi wa mizania wenye ufanisi, ufunguaji wa tawi la Dodoma na vituo vya huduma, ukuaji wa mfumo wa kibenki wa kidijitali na wa mawakala pamoja na ongezeko la wateja na miamala,"amesema.

Kapama amesema pia mafaniko hayo yametokana na ukuaji wa mikopo ambapo benki hiyo imefanikiwa kuongeza kiwango cha mikopo kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na mikopo iliyokuwepo katika Desemba mwaka 2017.

Pia amesema ufanisi wa benki hiyo umeongezeka hasa katika usimamizi wa matumizi ya riba na yasiyo ya riba, ufanisi wa mizania na uboreshaji wa huduma za utoaji wa mikopo.

Amefafanua katika utoaji huduma, benki ya biashara ya DCB imefanikiwa kuongeza idadi ya wateja kufikia 191,133 katika nusu ya pili ya mwaka iliyoishia Juni mwaka 2018 kutoka 188,305 Desemba mwaka 2017.

"Ongezeko hili la wateja 2,828, limechangia kuimarisha mapato ya benki kupitia kuongezeka kwa miamala, amana za kudumu na utoaji mikopo.

"Mikopo ghafi ya wateja iliongezeka kufikia Sh.bilioni 93.7 kufikia Juni mwaka 2018, kutoka Sh.bilioni 88.7 iliyokuwepo Desemba mwaka 2017, ambalo ni ongezeko la asilimia 5,"amesema.

Aidha Kapama amesema benki hiyo imefanikiwa kupunguza kiwango cha mikopo chechefu kutoka asilimia 18.8 Desemba mwaka 2017 kufikia asilimia 17.7 katika nusu mwaka inayoishia Juni 2018.

Ameongeza upunguaji huo  umechagizwa na ufanisi katika ukusanyaji wa madeni sugu, utoaji wa mikopo mizuri na kwa kuzingatia weledi, hali iliyoboresha ulipaji wa wateja.

"Ili kuongeza ufanisi wa mizania, benki ilipunguza amana ghali kwa kiwango kikubwa na hivyo kusababisha amana za wateja kupungua katika nusu ya pili ya mwaka 2018 ikilinganishwa Desemba mwaka 2017.

"Upunguaji huu wa amana ghali umechangia kupungua kwa gharama za riba za amana na hivyo kuiwezesha benki kutoa mikopo nafuu Zaidi kwa wateja,"amesema.

Kuhusu benki hiyo amesema ilianzishwa mwaka 2002 kutokana na kilio cha wakazi wengi wa Jiji la Dar es Salaam kutokuwa na namna ya kupata mitaji midogo ya biashara jambo ambalo lilikuwa changamoto kubwa kwa wajasiriamali wadogo wadogo katika jitihada za kuboresha biashara zao.

Pia sambamba na masharti magumu kutoka kwa benki nyingi za kibiashara na kwa kipindi chote cha miaka 16 ya uendeshaji, jukumu mama la benki hiyo limeendelea ni kutoa huduma bora za kifedha.

"Katika miaka yake takriban 16 ya uendeshaji, benki ya DCB imeweza kukuza idadi ya matawi kutoka tawi moja na kufikia manane (8) hadi mwaka huu wa 2018,"amesema.

Amesema ukuaji huo umechangia benki kupata faida mfululizo tangu mwaka 2004 hadi mwaka 2015, na imekuwa ikitoa gawio kwa wanahisa wake katika kipindi chote cha miaka 12.

"Hata hivyo, kutokana na changamoto za mpito, benki ilipata hasara katika miaka miwili ya 2016 na 2017, kabla ya kuzirekebisha na kurejea katika faida mwaka huu wa 2018,"amesema.

Kuhusu mafaniko Kapama amesema DCB ndio benki ya kwanza kuorodheshwa katika soko la hisa la Dar es Salaam, ni benki pekee iliyokua kutoka benki ya wananchi/jamii (community bank) na kufanikiwa kuwa benki ya biashara na imefanikiwa kukuza mtandao wa matawi yake.
Mkuu wa Idara ya Fedha wa Benki ya Biashara ya DCB, Zacharia Kapama (katikati) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati benki hiyo ikitangaza faida ya Sh.bilioni 1.0 katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2018. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano Rahma Gemina na kushoto ni Mkaguzi Mkuu wa ndani Deogratias Thadei.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad