HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 7, 2018

Tanzania Yang’ara Mifumo Ya TEHAMA Inayolenga Kuleta Ustawi wa Wananchi Vijijini

Frank Mvungi- MAELEZO, Mbeya
Tanzania imetajwa kuwa nchi iliyofanikiwa kuwa na mifumo bora ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayolenga kuchochea ustawi wa maisha ya wananchi hasa wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Akizungumza katika mahojiano maalum yaliyofanyika Jijini Mbeya leo, Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Mawasiliano wa Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma  (PS3) Bw. Desderi Wengaa, amesema kuwa hivi sasa Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa kuwa na mifumo bora na inayoongea, hali inayosaidia kuimarisha huduma kwa wananchi hasa wanyonge. 
PS3 ni mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).  Mradi huu wa miaka mitano unatekelezwa katika mikoa 13 ya Tanzania bara.
“Mifumo hii inalenga kuwawezesha watoa huduma katika ngazi ya vituo vyao kama Zahanati, Shule na Vituo vya Afya kutoa huduma kulingana na mahitaji ya wananchi na vipaumbele vya Serikali ambavyo kimsingi vinalenga kuwaletea wananchi maendeleo endelevu,” alisisitiza Wengaa.
Akifanua, Bw.Wengaa amesema kuwa mfumo kama wa Epicor 10.2 utasaidia Serikali kujua mapato na matumizi ya fedha za umma katika sekta za kipaumbele kama Afya na Elimu, ikiwa ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa rasilimali zote, ikiwemo fedha zinatumika kuboresha maisha ya wananchi.
Ameongeza kuwa kwa kutumia mifumo hiyo, thamani halisi ya fedha zitakazotumika katika miradi ya maendeleo itaonekana na pia itaongeza muda wa kuwahudumia wananchi katika vituo vya kutolea huduma, kwakuwa muda utakaotumika kwa kila anayehitaji huduma kuwa mchache.
Akieleza mikakati ya kufanya mifumo hiyo ilete matokeo tarajiwa, Bw. Wengaa amesema kuwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa kushirikiana na PS3 watakuwa na dawati la kufuatilia na kuhakikisha kuwa mifumo yoye inafanya kazi na kuleta matokeo tarajiwa.
Akizungumzia moja ya mfumo unaotumika katika sekta ya afya (Government of Tanzania Hosipital Management System – GoT-HoMIS) amebainisha kuwa unasaidia kutunza kumbukumbu za mgonjwa kuanzia siku ya kwanza anapofika kupata huduma, hivyo kuisaidia Serikali katika kutambua mahitaji halisi katika maeneo husika na hivyo kuboreshwa kwa huduma zinazotolewa.
Wakati Mfumo mwingine ni ule unaotumika katika kupanga mipango, bajeti na kutoa taarifa (PlanRep) ambao unasaidia watendaji katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuandaa mipango na bajeti katika vituo vyao na kuiwasilisha Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kupitia mfumo huo, hivyo kuokoa rasilimali fedha na muda uliokuwa unatumika awali kuandaa mipango na bajeti hizo.
Tanzania kutajwa kuwa nchi ya kupigiwa mfano ni kutokana na pia kuwepo kwa mifumo kama ile ya kubaini mahitaji ya watumishi katika sekta ya afya, hasa katika vituo vya kutolea huduma na vipaumbele vya eneo husika.
Kuhusu mifumo hiyo kuongea, Wengaa amebainisha kuwa, hali hiyo itasaidia kubainisha uwiano wa majukumu kati ya mtumishi mmoja na mwingine katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo kubaini watumishi wanatekeleza majukumu mengi zaidi kuliko inavyotakiwa ili kuweza kuongeza watumishi wengine katika eneo hilo. 
Baadhi ya mifumo hiyo ni PlanRep, WISN na POA, GoT-HoMIS na mfumo wa kuandaa taarifa za uhasibu katika ngazi ya kutolea huduma (FFARS), ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.  WISN na POA inasimamiwa kwa pamoja na Ofisi ya Rais Utumishi, ikiwa ni moja ya hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuboresha huduma za afya hapa nchini.
Mkuu wa Timu ya Mifumo ya Mawasiliano wa Mradi wa Kuimarisha Mifumo ya Sekta za Umma  (PS3) Bw. Desderi Wengaa akisisitiza kuhusu umuhimu wa mifumo hiyo katika kuwaletea wananchi maendeleo, wakati wa mahojiano maalum leo Jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad