HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 19 June 2018

Mufindi, PELUM kutoa Hatimiliki za kimila 700

Na Mwandishi Wetu
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kushirikiana na Shirika la PELUM Tanzania imeanza zoezi la kutoa hatimiliki za kimila zipatazo 747 kwa wananchi wa vijiji vitano vikiwemo vya Usokami, Ugesa, Magunguli, Isaula na Makungu.

Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Mufindi, Simon Mbago ameyazungumza hayo hivi karibuni alipokuwa akihojiwa na Mwandishi wa Habari hii ofisini kwake ambapo amesema kuwa hatimiliki hizo zimeanza kutolewa baada ya wananchi wa vijiji hivyo kufanyiwa mpango wa matumizi ya ardhi kupitia mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamia Sekta ya Kilimo unaofadhiliwa na watu wa Marekani.

“Tunalishkuru Shirika la PELUM kwa kufanya kazi nasi kwani limetusaidia kutekeleza moja ya majukumu yetu ya upimaji ardhi na utoaji hatimiliki ambapo hatimiliki hizo zinatarajia kunufaisha wanawake 250, wanaume 385, wenza wenye ushiriki wa pamoja 97 pamoja na maeneo ya Taasisi 15”, alisema Mbago.

Mbago ameongeza kuwa ni jukumu la kila Halmashauri kuhakikisha inatenga fedha kwa ajili ya shughuli za maendeleo ili kuvifanyia vijiji vyake mpango wa matumizi ya ardhi hivyo uwepo wa mashirika binafsi likiwemo la PELUM husaidia kwa kiwango kikubwa kuchochea maendeleo katika Halmashauri mbalimbali.

Pia Mbago amefafanua umuhimu wa hatimiliki hizo kuwa zitasaidia wananchi wa Halmashauri hiyo kuzitumia katika kuomba mikopo kwenye Taasisi za fedha kwa kuweka dhamana maeneo yao pamoja na kupunguza migogoro ya ardhi kwenye vijiji husika hasa kwa wananchi waliopo mipakani mwa wilaya ya Kilolo na Mufindi.

Kwa upande wake mwananchi wa kijiji cha Usokami, Evance Kibasa amesema hatimiliki ya kimila aliyokabidhiwa imemuhakikishia ulinzi halali na wa kisheria wa eneo lake kijijini hapo.

Nae Mwanakijiji Asafu Mgelekwa ambaye amekabidhiwa hatimiliki ya umiliki wa pamoja na mwenza wake amesema anashukuru kukamilika kwa zoezi hilo kwani amepata uhakika hata akitangulia mbele ya haki amemuacha mwenza wake kwenye mikono salama kutokana na kuwepo kwa migogoro mingi ya kifamilia baada ya mume kufariki.
 Asafu Mgelekwa na Mkewe Atuganule Lunyungu wakiwa wameshikilia hati zao za pamoja.
Simon Mbago Afisa Ardhi Mufindi akimsaidia mwananchi kuweka saini kwenye fomu kama uthibitisho ya kuwa amepokea hati.
 Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Ugesa wakiwa katika picha ya pamoja wakiwa na hatimiliki zao za kimila.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad