HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 28 June 2018

MAKANDARASI FANYENI KAZI KWA BIDII NA UADILIFU-KWANDIKWA

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa amezungumzia umuhimu wa Makandarasi kuungana ili kupata miradi mingi inayotekelezwa na Serikali na hivyo kuwezesha fedha nyingi zinazopelekwa kwenye miradi kuwanufaisha makandarasi wazawa.
Akizungumza wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa siku mbili wa wakandarasi jijini Dodoma, Mhe. Kwandikwa amesema ni wakati sasa kwa wakandarasi kuwa waadilifu katika kutekeleza miradi ya Serikali ili kunufaika na upendeleo unaofanywa na Serikali kwa makandarasi wazawa.
“Tumieni wataalamu wenye weledi wa kutosha katika miradi mnayopewa na Serikali muijenge kwa ubora na kuikamilisha kwa wakati kulingana na mikataba ili kuiwezesha Serikali kuwaamini na kuwapa miradi mingi na mikubwa ya ujenzi makandarasi wazawa’, amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Mhe. Kwandikwa amesema Serikali inaendelea kulipa madeni ya nyuma ya Wakandarasi na itaendelea kufanya hivyo ili kuhakikisha hali za uchumi kwa wakandarasi wazawa inaimarika na kumudu kujenga miradi mingi zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakandarasi Nchini (CRB) Eng. Consolata Ngimbwa ameiomba Serikali ifanye mabadiliko yatakayowezesha makandarasi wazawa kupata kazi nyingi zaidi hususani katika miradi mikubwa inayoendelea kujengwa Nchini.
Amesema hali za wakandarasi wengi kwa sasa si nzuri sababu hawapati miradi mingi ya kuwawezesha kufaidika na utekelezaji wa miradi hiyo hivyo ni wakati wa Serikali kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa ili kukuza uchumi na kuimarisha kampuni za wazawa kimtaji.
“Tunaomba Serikali itenge miradi mingi ya upendeleo kwa wakandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo lakini kuwezesha fedha nyingi kubaki nchini” amesema Eng. Ngimbwa.
Naye Msajili wa bodi ya CRB, Bw. Reubeni Nkori amesema kwa sasa makandarasi wenyeji ambao ni wengi wanapate fedha chache kutoka kwenye miradi ya ujenzi inayoendelea nchini ikilinganishwa na wakandarasi wachache kutoka nje wanaopata fedha nyingi.
Mkutano wa mwaka wa siku mbili wa Makandarasi ulioanza leo jijini Dodoma unawakutanisha Makandarasi wote nchini kujadili na kujitathmini ukiongozwa na kauli mbiu isemayo “Ukuaji wa Makandarasi kwa uchumi endelevu, fursa na changamoto”.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akisalimiana na Mjumbe wa Bodi ya Usajili Makandarasi (CRB), Eng. Light Chobya, kabla ya kufungua Mkutano wa mwaka wa siku mbili wa Bodi hiyo unaofanyika mjini Dodoma.
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akifungua Mkutano wa mwaka wa siku mbili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), unaofanyika mjini Dodoma.
 Sehemu ya Makandarasi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (hayupo pichani), wakati akifungua Mkutano wa mwaka wa siku mbili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), hiyo unaofanyika mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa (katikati), katika picha ya pamoja na Makandarasi mara baada ya kufungua  Mkutano wao wa mwaka mjini Dodoma. Wa pili kulia waliokaa ni Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi, Eng. Joseph Nyamuhanga.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad