HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, June 21, 2018

'KUNA ONGEZEKO KUBWA LA MAGONJWA YASIYOAMBUKIZA'

Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii

SERIKALI imesema kumekuwa na ongezeko kubwa la magonjwa yasiyoambukiza kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni hali inayotishia afya ya mama na mtoto wakati wa kijifungua pindi wanapofika hospitalini.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza kutoka Wizara ya Afya,Maedeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk . Sara Maongezi wakati akifungua Programu ya AstraZeneca ya Healthy Heart Africa (HHA).

Programu hiyo inatokana na ushirikiano wa Touch Foundation na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.Lengo ni  kupunguza maradhi ya shinikizo la damu wakati wa mimba.

Maongezi amefafanua ubia uliozinduliwa leo katika mradi huo utakaoongeza utekelezaji wa programu hiyo nchini Tanzania.  

"Ubia huo unakusudia kwa kiasi kikubwa kupunguza kuenea kwa maradhi ya shinikizo la damu, hasa miongoni mwa wanawake wajawazito ikiwa ni kuunga mkono mpango mkakati wa Serikali wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza,"amesema Dk. Maongezi.

Ameongeza kupanda kwa shinikizo la damu ni moja ya vihatarishi vikubwa vya ugonjwa wa moyo hali ambayo msukumo wa damu katika moyo  huzuizwa au kukatizwa na chembe chembe za mafuta kwenye mishipa ya koronari  na mwishowe huenda ikasababisha kiharusi.

Amefafanua kwa bahati mbaya, ugonjwa wa moyo ni moja ya vyanzo vikubwa vya kifo nchini Tanzania hasa kwa wajawazito wakati wa kujifungua.

Amesema  kupitia ufadhili wa AstraZeneca, shirika la Touch Foundation litaendeleza mpango wa Healthy Heart Africa  ambao tayari unatekelezwa huko Kenya na Ethiopia, kwa kufuata mazingira halisi ya Tanzania kama linavyotekelezwa mpango wake wa Mobilizing Maternal Health (MMH) katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza.

 "Serikali tunaukaribisha ubia huu mpya kwa vile unakwenda sambamba na azma yetu inayolenga kinga kwa jamii, kuboresha afya, kupima, na kutoa matibabu mapema, na kuwasaidia waathirika. 

"Ubia huu pia unajikita katika imani aliyonayo Rais John Magufuli kwamba kazi ya kujenga uchumi na kupambana na umaskini inategemea zaidi afya bora ya raia wake.

"Kwa hiyo, nausifu mpango huu na kuwa na matarajio mema katika safari yetu ya kuboresha maisha ya Watanzania kwa kupambana na maradhi ya shinikizo la damu nchini mwetu,"amesema.

Ameongeza shinikizo la damu kwa asilimia 16 unasababisha vifo vya mama wajawazito nchini Tanzania na kwamba ingawa kiwango cha kuenea kwa ugonjwa huo ni kikubwa.

Ambapo watu milioni 150 katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara wakitarajiwa kuathiriwa na maradhi hayo ifikapo 2025.Viwango vya uelewa na tiba bado viko chini, hali inayoonyesha ipo haja kwa programu nzima kujielekeza zaidi katika kukuza uelewa na tiba ya shinikizo la damu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwandamizi wa Programu ya Healthy Heart Africa ya AstraZeneca, Ashling Mulvaney, amesema wao kama kampuni ya dawa duniani yenye urithi mkubwa wa kisayansi, uboreshaji wa mfumo wa afya imekuwa ndio nguzo yao kubwa.

Amesema waamini nguvu ya pamoja itakuwa ni silaha kubwa katika mapambano dhidi ya changamoto zinazoikabili sekta ya afya kama magonjwa yasiyoambukiza ambayo sasa ndio chanzo kikubwa cha vifo duniani.

Ameweka wazi kuwa  lengo la programu ya Healthy Heart Africa nchini Tanzania ni kukuza uwezo wa mfumo wa sekta ya afya kukabiliana na maradhi ya shinikizo la damu miongoni mwa wanawake  wajazito kwa kuimarisha uwezo wa wafanyakazi wa sekta ya afya na kuimarisha mbinu za kuwasaidia akina mama katika wilaya sita.

"Lengo la mpango huu ni kutoa mafunzo kwa wafanyakazi 350 kuhusu mbinu za kutoa huduma pamoja na kuwapima wafanyikazi 1,800 na  wanawake wajawazito 50,000 katika kipindi cha miaka mitatu kwa kuwashauri wajiunge na matibabu, iwapo itahitajika,"amesema Mulvaney.

Wakati huo huo Mganga Mkuu wa Shirika la Touch Foundation, Steven Justus, amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004, taasisi hiyo imeelekeza nguvu zake kuboresha sekta ya afya nchini Tanzania.

"Ubia huu na kampuni ya kimataifa ya AstraZeneca na Serikali ya Tanzania ni fursa pekee ya kuunganisha juhudi za pamoja za mapambano dhidi ya maradhi ya shinikizo la damu kwa wajawazito kwa kuwahusisha wahudumu wa afya ili kuleta mafanikio katika mfumo wa afya na maisha ya watu,"amesema.

Programu ya Healthy Heart Africa, ambayo ilianzishwa nchini Kenya mwaka 2014, ina lengo la kuwafikia watu milioni 10 wanaokabiliwa na shinikizo la damu barani Afrika katika jitihada za kuliunga mkono Shirika la Afya Duniani (WHO).

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad