Benki ya CRDB imetoa zawadi za kwanza
kwa washindi wa kampeni yake ya TemboCardVisa ijulikanayo kama “Shuhudia Kombe
la Dunia FIFA 2018 na TemboCardVisa” katika hafla fupi iliyofanyika katika hoteli ya
Ramada Encore iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo jumla ya washindi 15 wamekabidhiwa zawadi zao ikiwamo zawadi ya
tiketi kwenda kushuhudia mechi za Kombe la Dunia nchini Urusi kwa washindi wa 3 wa
kwanza kwa wiki tatu za mwanzo za kampeni. Wakati washindi wengine 12 walioshika
nafasi ya pili hadi tano wamekabidhiwa zawadi za seti ya luninga na king’amuzi cha
Dstv kilicholipiwa kwa miezi miwili ya Kombe la Dunia.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utoaji zawadi Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya
CRDB Dokta Charles Kimei alisema kampeni hiyo ina lengo la kuwahamasisha wateja
wa Benki ya CRDB kufanya malipo na manunuzi kwa kutumia kadi zao za
TemboCardVisa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa baadhi ya washindi wa kampeni ya TemboCardVisa ijulikanayo kama “Shuhudia Kombe la Dunia FIFA 2018 na TemboCardVisa” iliyofanyika katika hoteli ya Ramada Encore, jijini Dar es salaam.
“Lengo letu ni kuwajengea wateja wetu utamaduni wa kutumia kadi zao kufanya malipo
na manunuzi mitandaoni ‘online shopping’ na kupitia vifaa vya manunuzi vilivyopo
sehemu mbalimbali kama supermarkets, maduka ya rejareja, mahotelini, mahospitalini
na taasisi nyingine mbalimbali binafsi na za serikali,” alisema Dokta Kimei.
Kampeni ya “Shuhudia Kombe la Dunia FIFA 2018 na TemboCardVisa” ilizinduliwa
rasmi mapema mwezi wa nne kwa Benki ya CRDB kushirikiana na Visa International
ambao pia ni moja ya wadhamini wa Kombe la Dunia mwaka huu.
Dokta Kimei pia aliwapongeza washindi wote walioibuka kidedea katika shindano hilo
huku akiwasihi wateja wengine wa Benki hiyo kuendelea kushiriki katika Shindano hilo
linalotarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa mwezi wa saba.
“Mshindi ni mteja ambaye atafanikiwa kufanya miamala mingi zaidi ya manunuzi kupitia
kadi yake ya TemboCardVisa,” alisema Dkt. Kimei.
Akizungumza katika hafla hiyo Meneja Mkuu wa Visa Afrika Mashariki Ndugu Sunny
Walia aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha
wateja kutumia kadi zao kufanya malipo huku akiwataka wateja kuendelea na
utamaduni huo kwani sasa dunia inaondokana na matumizi ya pesa taslimu hivyo ni
vizuri kujiweka tayari.
“Niwapongeze pia washindi wetu, na niwaombe waendelee kutumia kadi zao za
TemboCardVisa na wakawe mabalozi pia kwa ndugu jamaa na rafiki zao ili siku
nyingine nao tuwaone wakishinda,” alisema Ndugu Sunny Walia
Kwa upande wake Mkuu wa Uendeshaji Multichoice Tanzania ambao pia ni washirika
wa kampeni hiyo Ndugu Ronald Shelukindo, alisema imekuwa ni fahari kwao
kushirikiana na Benki ya CRDB katika kampeni hiyo ya “Shuhudia Kombe la Dunia FIFA
2018 na TemboCardVisa” huku akisema Multichoice itahakikisha washindi hao
wanapata fursa ya kushuhudia Kombe la Dunia mubashara kupitia ving’amuzi vyao
ambavyo vitakuwa na ofa maalum katika msimu wa Kombe la Dunia.

Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa akifafanua jambo, katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa baadhi ya washindi wa kampeni ya TemboCardVisa ijulikanayo kama “Shuhudia Kombe la Dunia FIFA 2018 na TemboCardVisa” iliyofanyika katika hoteli ya Ramada Encore, jijini Dar es salaam.
“Niwakumbushe pia huduma ya malipo ya Dstv inapatikana katika SimBanking, hivyo
basi hamna sababu ya kuhangaika kulipia ving’amuzi vyenu vinapokaribia kuisha,”
alisema Ndugu Shelukindo.
Kampeni ya “TemboCardVisa” pia imekuwa ikiendeshwa kupitia mitandao ya kijamii ya
Instagram, Facebook na Twitter kwa hashtag maalum ya #TwenzetuRussia2018,
ambapo watu wamekuwa wakishiriki na kushinda zawadi mbalimbali ikiwamo fedha
taslimu.
Kwa mara ya kwanza Benki ya CRDB ilizindua huduma ya TemboCard mwaka 2002,
ikilenga kuwapa wateja wake urahisi na unafuu wa upatikanaji wa huduma popote
walipo kupitia kadi hizo za TemboCard. Mpaka sasa Benki ya CRDB imefanikiwa
kuingiza katika soko jumla ya TemboCard milioni 3. Urahisi, usalama na unafuu wa
huduma ya TemboCard unawawezesha wateja wengi wa Benki ya CRDB kufanya
malipo kwa ajili ya bidhaa na huduma mbalimbali bila kuhitaji fedha taslimu.
Dkt. Kimei alimalizia kwa kuwashukuru wateja wa Benki ya CRDB kwa kuifanya kuwa
Benki nambari moja na bora zaidi, huku akisema kuwa wateja wa Benki hiyo
wamekuwa na mchango mkubwa sana katika ukuaji wa Benki ya CRDB.
“Bado tuna tiketi maalum za nusu fainali ambazo tunatangaza washindi wake hivi
karibuni. Hivyo naendelea kuwahimiza Watanzania kuendelea kufanya malipo na
manunuzi kupitia kadi zao za TemboCard Visa,” alihitimisha Dokta Kimei.
Hii ni mara ya tatu kwa Benki ya CRDB kupeleka wateja wake kushuhudia Kombe la
Dunia kwani mwaka 2010 na mwaka 2014 benki hiyo iliendesha kampeni kama hii
ambapo iliwapeleka wateja wake kushuhudia mechi za Kombe la Dunia nchini Afrika ya
Kusini na Brazil.
No comments:
Post a Comment