HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, May 11, 2018

POLISI KANDA MAALUM DAR YAWASHIKILIA WATU 10 KWA TUHUMA ZA WIZI WA KUTUMIA SILAHA

Na Emmanuel Masaka, Globu ya jamii
KAMANDA wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Lazaro Mambosasa  amesema hali ya usalama ya Jiji hilo ni shwari  huku akielezea matukio kadhaa ambayo yametokea katika kukabiliana na matukio ya uhalifu.

Mambosasa amezungumza leo jijini Dar es Salaam ambapo ameelezea pia kukamatwa kwa watu 10 wanaotuhumiwa kwa ujambazi wa kutumia silaha.

Amewataja watuhumiwa hao ni Bushiri Ally (29) mkazi wa Tandika, Mohamed Ismaili (18) mkazi wa Tandika, Issa Saidi (19) mkazi wa Yombo, Mlekwa Ally (18) mkazi wa Tandika, Shabani Nassoro (17) mkazi wa Tandika, na watano wengine ambao majina yao wameyahifadhi kwa sababu za kiupelelezi.

Mambosasa amesema Aprili 29 mwaka huu, saa sita usiku katika maeneo ya Tandika Foma askari wakiwa doria waliitilia shaka gari namba T 401 CLF aina ya Toyota Alteza rangi ya fedha na kuanza kulifuatilia kisha kulikamata na kukuta watu watano wakiwa ndani ya gari hilo.

Amefafanua askari waliwaweka chini ya ulinzi watu hao na kufanya upekuzi ndani ya gari hilo na kufanikiwa kukamata  Bastola aina ya Browning yenye namba N635BRE ikiwa na risasi mbili ndani ya Magazine ikiwa na Watuhumiwa waliokamatwa kwenye gari hiyo ni Bushiri Ally (29) mkazi wa Tandika, Mohamed Isimaili (18) mkazi wa Tandika, Issa  Saidi (19) mkazi wa Yombo, Mlekwa Ally (18) mkazi wa Tandika na Shabani Nassoro (17) mkazi wa Tandika.

"Watuhumiwa hao walihojiwa na mtumiwa mmoja Bushiri Ally alikiri bastola hiyo ni ya kwake na aliiokota Tandika mtaa wa Mteja mwaka 2014 na huwa anaitumia kufanyia vitendo vya uhalifu katika maeneo mbalimbali ya Jiji,"amesema.

Katika tukio lingine Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linawashikilia watuhumiwa watano kwa tuhuma za kukutwa na Bastola 2 na risasi 16, nyundo moja na bisisi  tatu ambavyo walikuwa wakivitumia katika matukio mbalimbali ya uhalifu wa wizi wa magari hapa Jijini.
Amesema watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na operesheni kali inayoendelea kufanyika dhidi ya wezi wa magari na wahalifu wanaotumia silaha.

Aidha ameeleza Mei 5 mwaka huu, saa tano usiku maeneo ya Mbezi Makondeko Remmy Wilbard (41) mkazi wa maeneo hayo akiwa anatoka kwenye biashara zake na gari Toyota Noah namba T681 DJM rangi ya fedha.

Amesema na alipofika nyumbani kwake alishuka kwenye gari lake kwaajili ya kwenda kufungua geti, ghafla alivamiwa na watu watatu wakiwa na bastola moja na silaha za jadi na kumpora gari hilo.
"Mlalamikaji alifungua kesi katika kituo cha Polisi Kimara na upelelezi ulianza mara moja ambapo Mei  7 mwaka 2018, saa 12 jioni Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam lilipata taarifa kutoka msiri wake kuwa huko Sinza Kumekucha kuna watu wanataka kuuza gari la wizi.

Amesema ulifanyika ufuatiliaji na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili, na baada ya kufanya mahojiano ya kina na watuhumiwa hao yalipelekea kuwakamata watuhumiwa wengine watatu.
Baada ya kukamilisha mahojiano na watuhumiwa hao watano Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es salaam liliongozana na watuhumiwa hao hadi kwenye makazi yao  na kufanya upekuzi.

Hivyo Mei 8 mwaka huu maeneo ya Kimara King’ong’o Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam lilienda mpaka kwenye nyumba ya mtuhumiwa wa kwanza na kufanya upekuzi na kufanikiwa kupata silaha bastola ambayo haijatambulika aina yake yenye namba AK-0383 TZCAR 71414 iliyokuwa imefichwa ndani ya kabati la nguo ndani ya nyumba ya mtuhumiwa.

Ameongeza kuwa Mei 10 mwaka huu , saa tano usiku maeneo ya Mbagala rangi tatu alikamatwa mtuhumiwa mwingine  baada ya kufanyiwa Upekuzi katika nyumba anayoishi alikutwa na silaha bastola aina ya Beretta U.S.A CORP. ACOOKEEK.MD ikiwa imefutwa namba na risasi sita ndani ya magazine.

"Watuhumiwa hao walikiri kujihusisha na wizi wa magari na uhalifu wa kutumia silaha katika maeneo ya Jiji.Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao hivi,"amesema. 
Kuhusu hali ya usalama barabarani Mambosasa amesema kuanzia Aprili 14 mwaka hadi Mei 10 mwaka huu kikosi cha usalama barabarani kinaendelea na juhudi za kupunguza ajali za barabarani kwa kufanya ukaguzi na ukamataji magari na pikipiki mbovu.

Amesema katika kipindi hicho jumla ya magari yaliyokamatwa ni 44,879 idadi ya pikipiki zilizokamatwa 1,466, idadi ya daladala zilizokamatwa ni 17,199, idadi ya magari mengine (binafsi na malori) ni 27,680 na bodaboda waliofikishwa mahakamani kwa makosa ya kutovaa kofia ngumu na kupakia mshikaki ni 103,hivyo jumla ya makosa yaliyokamatwa ni 125,456. Fedha zilizopatikana kutokana na makosa ya usalama barabarani ni jumla ya Sh.1, 563,082,500.
 Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akionesha silaha mbalimbali zilizo kamatwa na Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali  jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza na waandishi wa habari leo juu kukamatwa kwa watuhumiwa kumi kwa tuhuma za ujambazi wa kutumia silaha. (Picha na Emmanuel Massaka Globu ya jamii)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad