HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Wednesday, 30 May 2018

DKT. ASHATU KIJAJI AZIPONGEZA BENKI KUSHUSHA RIBA ZA MIKOPO

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Uamuzi wa Serikali wa kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na benki za biashara  nchini, umechochea taasisi za fedha yakiwemo mabenki kuanza kupunguza viwango vya riba ya mikopo hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi.

Hayo yalisemwa Jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji wakati wa kufunga warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha uliowashirikisha wabunge, washirika wa Maendeleo, wakuu wa Taasisi za fedha na Wizara ya Fedha na Mipango.

Dkt. Kijaji, alisema kuwa Serikali kupitia Benki Kuu imeshusha riba ya mikopo kwa taasisi za fedha kutoka asilimia 16.0 hadi  asilimia 9.0 na  kupunguza kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa katika Benki hiyo na benki za biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0  kuanzia mwezi Aprili 2017, jambo ambalo limeleta matokeo chanya katika kuimarisha uwezo wa taasisi kukopesha wateja wao.

Miongoni mwa Benki zilizoshusha viwango vyao vya riba za mikopo ni CRDB ambayo imetangaza kushusha riba kutoka asilimia 22 hadi 16 na kuongeza kiasi cha kukopa kwa wafanyakazi kutoka Sh. milioni 50 hadi Sh. milioni 100 huku muda wa kurejesha ukiongezwa kutoka miaka mitano hadi saba.

Benki  nyingine ni NMB ambayo imeongeza muda wa marejesho ya mikopo kwa wafanyakazi, wajasiriamali wadogo na wakubwa kutoka miezi 60 hadi 72, na  imepunguza riba ya mikopo kwa wafanyakazi kutoka asilimia 21 hadi 19 na wajasiriamali wadogo kutoka asilimia 23 hadi 21.

Dkt. Kijaji amezipongeza benki zilizoshusha viwango vya riba  na ameitaja hatua hiyo kuwa ni muhimu katika kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda hata kabla ya mwaka 2025 na kutoa wito kwa taasisi hizo za fedha kuitupia jicho sekta ya kilimo kutokana na umuhimu wake katika kutimiza malengo ya kukuza viwanda.

Aidha, Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali imekamilisha andiko “Blue Print” ambalo lengo lake ni  kuboresha mazingira ya kufanya biashara nchini ili kuleta tija kwa wafanyabiashara na Sekta ya Fedha kwa ujumla

Alisema Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai mbalimbali yaliyohakikiwa ya watumishi, wakandarasi na watoa huduma wengine  yaliyohakikiwa ili kuongeza ukwasi katika jamii na kwa kwamba uhakiki uliofanyika umeokoa kiasi kikubwa cha fedha za Serikali ambazo zingelipwa wakati madai hayakuwa sahihi.

Naibu Waziri huyo aliipongeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa kushiriki kwa vitengo katika utekelezaji wa Mpango huo kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari katika eneo la Mkulazi na Mbigiri - Morogoro na  mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa ya nyama eneo la Makunganya  mkoani  humo.

Naye Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Khatibu Kazungu, alieleza kuwa warsha hiyo iikuwa na manufaa makubwa na kwamba Wizara inaandaa mkakati wa utekelezaji wa Sekta ya Fedha wa Miaka kumi ambao utakujumuisha pia mawazo ya wadau hao.

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Prof. Honest Ngowi,  amepongeza hatua ya Serikali ya kuwa na majadiliano na Sekta ya fedha kwa kuwa ina mchango mkubwa katika kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Akitoa tathimini yake kuhusu utekelezaji wa Mpango huo, Prof. Ngowi, alisema kuwa sehemu ya miradi kumi ya kipaumbele, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), ufufuaji wa Shirika la Ndege na Ujenzi wa Kiwanda cha Sukari Mkulazi mkoani Morogoro, ni baadhi ya miradi muhimu inayotekelezwa.

Kwa Upande wao,  Mbunge wa Muheza Mhe. Adadi Rajab na Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Maria Kangoye, wamezishauri Sekta za Fedha nchini kuiwezesha zaidi sekta ya kilimo ili ikue haraka na kuishauri pia Wizara ya Fedha na Mipango, kufanya mikutano ya namna hiyo na wadau kabla ya Bunge la Bajeti kuanza ii manufaa yake yaweze kuwa makubwa zaidi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), akifunga  warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.
 Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Khatib Kazungu akizungumza wakati wa  kufunga warsha  ya wadau wa Sekta ya Fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma. 
 Mbunge wa Jango’mbe Mhe. Ally Hassan King akizungumza  wakati wa  kufunga warsha ya wadau wa Sekta ya Fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.
 Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe Dkt. Honest Ngowi akiongoza mjadala wakati wa warsha  ya wadau wa sekta ya fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.
 Mmoja wa wadau wa Sekta ya Fedha  akizungumzia umuhimu wa ushirikishwaji wa sekta hiyo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo hapa nchini ili kuchochea maendeleo.
 Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA), Dkt. Boghayo Saqware  akizungumzia hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa   warsha  ya wadau wa sekta ya fedha iliyolenga kujadili mchango wa sekta hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda leo Jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad