HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, 11 May 2018

DC SOPHIA MJEMA AHIMIZA WATUMISHI ILALA KUCHAPA KAZI, AZINDUA KAMPENI YA UJENZI WA CHOO CHA MTOTO WA KIKE

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
MKUU wa Wilaya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam Sophia Mjema amewahimiza watumishi wa wilaya hiyo kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii huku akisisitiza kwake ni kazi tu kama kauli mbiu ya Serikali ya Awamu ya Tano inavyohimiza watu kufanya kazi.

Mbali ya kuhimiza watumishi wa Wilaya ya Ilala kufanya kazi Mjema amezindua rasmi kampeni ya ujenzi wa choo cha mtoto wa kike katika wilaya hiyo kwa shule zote za msingi ambapo amesema yeye binafsi anaunga mkono kampeni hiyo kwa kujenga choo cha matundu sita huku akiahidi kuhamasisha wadau wa maendeleo kusaidia ujenzi huo.

Mjema amesema hayo leo mbele ya Watumishi Wanawake wa Manispaa ya Ilala ambao wamekuwa na utamaduni wa kila mwaka siku kama ya leo kukutana na kufanya tathimini ya utendaji kazi wao na kwa mwaka huu wameamua kuhamasishana kujenga choo cha mtoto wa kike ambacho kitakuwa rafiki na kumsaidia mtoto wa kike kupata nafasi ya kujisitiri hasa wakati anapokuwa kwenye hedhi baada ya kubaini kwa sasa wanafunzi hasa wa darasa la saba kuwa na wakati mgumu kutokana na mazingira ya vyoo vilivyopo shuleni kutokuwa rafiki kwao.

"Tumekutana leo moja ya lengo kuu ni kufanikisha ujenzi wa choo cha mtoto wa kike wa Wilaya ya Ilala ambaye tunaamini ndio atakuwa mtumishi wa wilaya yetu kwa siku zijazo.Hivyo lazima mtoto huyu tumuangalie na kutatua changamoto zake anapokuwa shuleni.Nimezindua kampeni hii ya ujenzi wa choo cha mtoto wa kike kwa lengo la kumuondolea changamoto wanazokutana nazo sasa.

"Binafsi nitajenga choo cha matundu sita na tayari kuna wadau ambao wamejitolea nao kujenga matundu ya vyoo ambavyo vitakuwa na kila kitu muhimu kwa ajili ya mwanafunzi wa kike aliyeko shuleni.Vyoo vitakavyojengwa vitakuwa na kiti chooni, kutakiwa na kioo cha binti kujiangalia na eneo la kufua nguo yake iwapo itatokea bahati mbaya imechafuka,"amefafanua na kuongeza kazi ya ujenzi wa vyoo hivyo itaanza mara moja kwani awamu hii ni ya Hapa Kazi Tu.

Amefafanua kutokana na maumbile ya mtoto wa kike yalivyo ni rahisi kupata magonjwa ya aina mbalimbali yakiwamo ya satarani ya shingo ya kizazi na UTI kutokana na kutumia vyoo ambavyo si safi na hivyo moja ya mikakati ya wilaya hiyo ni kujenga vyoo ambavyo vitakuwa safi ili kumuepusha mtoto wa kike kupata magonjwa.

Ameelezea kuwa mkakati wa ujenzi wa vyoo hivyo utakwenda sambamba na ujenzi wa matundu ya vyoo kwani hivi sasa Wilaya hiyo inadaiwa matundu ya vyoo 3000 , hivyo kazi ya kuvijenga inaendelea.

Kwa upande wa Ofisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Wilaya ya Ilala Elizabeth Thomas amesema kutokana na changamoto ambayo wanaipata watoto wa kike shuleni, Watumishi Wanawake wa manispaa hiyo wameamua kuchangishana fedha pamoja na kuwaomba wadau mbalimbali kusaidia kufanikisha ujenzi wa choo cha mtoto wa kike katika shule za msingi.

 "Wanawake ni jeshi kubwa na kueleza idara ya elimu msingi kuna watumishi 4000 kati yao wanaume ni 500.Manispaa hiyo ina idara 13 na idadi ya watumishi wanawake ni kubwa na kwa mazingira hayo wameona haja ya kutatua chagamoto ya mtoto wa kike ambaye ndio mtumishi ajaye wa manispaa hiyo,"amesema/

Awali wakati anamkaribisha Mjema, Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala Dar es Salaam Tabu Shaibu amesema changamoto za mtoto wa kike ni nyingi na wanazipata katika njia mbalimbali na hivyo mwaka huu Watumishi Wanawake wamekuja kivingine kwa kuamua kuanzisha kampeni ya ujenzi wa choo cha mtoto wa kike katika shule za msingi 120 za manispaa na wao wameanza kwa kujenga choo cha mfano katika Shule ya Msingi Chanika.

"Watumishi Wanawake katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam wameamua kuanzisha kampeni maalumu ya ujenzi wa Choo cha mtoto wa kike kwa kuanza na shule zote za msingi katika manispaa hiyo.

"Tafiti zimefanyika kuhusu sababu zinazochangia mahudhurio hafifu ya mtoto wa kike darasani hasa  wa darasa la saba na takwimu zao zinabainisha wasichana wa darasa la saba hawahudhurii shuleni kati ya siku nne hadi tano kila mwezi.Vyoo visivyofaa kwa matumizi hasa kwa wasichana wanaoingia hedhi huleta changamoto kubwa kwao.

"Kutokana na changamoto hiyo watumishi wanawake wa Manispaa ya Ilala wameona wanao wajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali na kuendelea kuihamasisha jamii na wadau kujenga choo bora cha kisasa kitakachokuwa rafiki kwa mtoto huyu wa kike,"amesema Shaibu.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akizungumza wakati akizindua rasmi kampeni ya ujenzi wa Choo cha mtoto wa kike kwa shule za msingi uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Watumishi Wanawake wa Manispaa ya Ilala wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema leo.
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema akiwa pamoja na Ofisa Habari wa Manispaa ya Ilala Tabu Shaibu(kulia)wakiwa wameshika tuzo ya heshima ya kutambua mchango wa mkuu huyo wa wilaya hasa katika utumishi wake wa kiongozi katika kuitumikia jamii ya Ilala.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad