HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, May 14, 2018

Balozi Seif akutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya Kifalme ya Oman

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya  Kifalme ya Oman Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi alisema uwepo wa Jumla la Ajabu liliopo Forodhani Mji Mkongwe maarufu {Beit Al Ajaib}utaendelea kuwa utambulisho wa Zanzibar Kimataifa katika masuala ya Kihistoria na Utamaduni.

Alisema Jengo hilo Maarufu ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na Dunia    tokea Karne ya 17 linastahiki kufanyiwa matengenezo makubwa ili kulirejeshea hadhi yake ya kawaida na Oman tayari imeshajitolea kugharamia matengenezo hayo.

Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi aliyeambatana na Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Bwana Hamud Al Has alisema hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.

Katibu Mkuu Salum alisema hatua ya Serikali ya Oman kujitolea gharama za Matengenezo ya Jumba hilo imekuja kutokana na Historia kubwa ya Uhusiano uliopo kati ya Zanzibar na Oman kwa Karne kadhaa zilizopita.

Alisema Historia ya pande hizo mbili zenye udugu wa Damu hasa katika masuala ya Utamaduni utaendelea kuwepo na kuimarishwa kwa faida ya Vizazi vya sasa na vile vitakavyokuja  hapo baadae.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Kale wa Omar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ujio wa  Ujumbe wake  kufanya ziara Visiwani Zanzibar umepangwa kufanya Uratibu wa ushirikiano wa mambo kadhaa yatakayoweza kusaidia kuimarisha Ushirikiano wa pande hizo mbili.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar  bado ni tulivu na kuwaomba Waoman  kutumia fursa iliyopo ya Zanzibar ni Njema kufika kujifunza mambo tofauti ya Kihistoria ambayo yana mafungamano ya Oman.

Balozi Seif  aliuhakikishia Ujumbe huo wa Oman  kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kutoa ushirikiano kwa ndugu zao wa Oman na kusema kwamba Wasimamizi pamoja na Wajenzi wa Matengenezo wa Jumba la Beit Al Ajaib watepewa msaada wa kina katika kuona kazi hiyo inakwenda na kumalizika kwa mafanikio makubwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba mambo yaliyopo Zanzibar yenye mafungamano na uhusiano na Oman akitolea mfano Majengo ya Kihistoria yaliyopo Mji Mkongwe yataendelea kutunzwa ili iwe kumbukumbu nzuri ya uwezo wa ushirikiano wa pande hizo mbili.

Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Mambo ya Kale wa Oman Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi na Ujumbe wake tayari wameshatembelea sehemu mbali mbali za Kihistoria, maeneo ya Viungo pamoja na kukutana na Viongozi mbali mbali wanaohusika na masuala ya Mambo ya Kale.

  Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya  Kifalme ya Oman Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi Kulia akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar. Katikati yao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed na Nyuma ya Balozi Seif ni Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Bwana Hamud Al Has.
 Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi aliyenyanyua Mkono akielezea Mikakati ya Oman katika kuendeleza Uhusiano na Zanzibar wakati akizungumza na Balozi Seif Ali Iddi wa kwanza kutoka Kulia.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa kwanza Kutoka Kulia akiishukuru Serikali ya Oman kwa misaada inayoendelea kutoa kwa Zanzibar.
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Kale wa Serikali ya  Kifalme ya Oman Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi aliyevaa Kilemba akifafanua jambo mara baada ya kumaliza mazungumzo yao na Balozi Seif. Kushoto ya Bwana Salum Mohamed Al – Mahrooqi ni Waziri wa Habari, Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar Mh. Mahmoud Thabit Kombo na Kulia ya Balozi Seif ni Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud Mohamed. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad