HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, May 31, 2018

Balozi Seif afanya mazungumzo na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Jamuhuri ya Cuba kwa kumaliza Uchaguzi wa Bunge salama wa kuwachagua Wajumbe wa Baraza Kuu la Nguvu ya Umma lenye Mamlaka ya kumchagua Rais wa Baraza la Taifa la Nchi hiyo.

Alisema uchaguzi huo uliofanyika Mnamo Tarehe 11 Machi, 2018,  ambapo Wajumbe wa Baraza la Taifa la Cuba walimchaguwa Bwana Miguel Diaz –Canel kuwa Rais wa Nchi hiyo aliyekuwa msaidizi wa Kiongozi wa Taifa hilo Bwana Raul Castro ulikuwa na amani na kushuhudiwa na Jumuiya za Kimataifa.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo wakati akizungumza na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandes kwenye Makazi yake Jijini  Dar es salaam.

Alisema kufuatia kumalizika kwa uchaguzi  huo Tanzania na Cuba zitaendelea kupata wasaa zaidi wa kushirikiana katika masuala na sekta zilizoanzishwa ambazo ana matumaini ya kuendelezwa chini ya Rais huyo Mpya wa Cuba Bwana Maguel Diaz – Canel mwenye fikra za watangulizi wake waliolenga kuona ustawi wa Bara la Afrika unaimarika na kukua siku hadi siku.

Akitoa shukrani zake Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo Hernandes alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Cuba itaendelea kuiunga Mkono Tanzania hasa katika masuala ya Elimu na Afya.

Profesa Lucas alisema miradi ya pamoja iliyoanzishwa akiutolea mfano ule wa Afya umeanza kutoa sura ya matumaini kufutia baadhi ya Madaktari Wazalendo wa Zanzibar kuendelea na mafunzo yao ya Juu ya Udaktari Nchini Cuba baada ya kumaliza masomo yao Zanzibar chini ya usimamizi wa Wataalamu na Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Matantas cha Nchini humo.

Kiongozi huyo Mpya wa Taifa la Cuba akiwa wa Tatu tokea Taifa hilo kupata Uhuru wake  alishika wadhifa huo kwa kupata Asilimia 85.65%  baada ya kushinda Viti Mia Sita na Tano.

Bwana Miguel Diaz – Canel wa Chama cha Kikoministi anayeshika nafasi hiyo ya Urais katika kipindi cha Miaka Mitano akiendelea hadi Mwaka 2023 amepungukiwa na Viti 7 ikilinganishwa na Uchaguzi uliopita wa Mwaka 2013 ambapo mshindi aliibuka na Viti 612.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa salamu za pole kwa Rais wa Cuba Bwama Miguel Diaz – Canel kupitia Balozi wa Nchi Hiyo Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo kufuatia ajali ya Ndege ya Boeing 737 ya Shirika la Ndege la Cuba { Cubana Airlines }.

Ajali hiyo iliyotokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Havana wa Jose Marti ilisababisha idadi ya Vifo vya Abiria Mia 111 hadi kufikia mapema wiki hii ambao walikuwemo kwenye Ndege hiyo.

Balozi Seif kupitia Balozi huyo wa Cuba Nchini Tanzania aliwataka Wananchi wa Cuba pamoja na wale wenye jamaa na ndugu zao waliokumbwa na Umauti huo kuwa na moyo wa Subira katika kipindi hichi kizito cha Msiba.

Alisema Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla wanaungana na Serikali ya Cuba pamoja na Wananchi wake katika msiba huo uliojumuisha pia Vijana ambao ndio nguvu kazi iliyokuwa ikitegemewa na Taifa hilo.

Ndege hiyo ya Abiria ilipata ajali mara baada ya kuruka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Jose Marti  katika Mji  Mkuu wa Havana ikielekea Mji wa Holguin ulioko Mashariki mwa Nchi hiyo.

Kwa mujibu wa takwimu za Vyombo vya Habari hiyo ni ajali ya Tatu kubwa za Ndege Nchini Cuba tokea mnamo Mwaka 2010.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akisalimiana na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Profesa Lucas Domingo alipofika kwenye Makaazi yake Jijini Dar es salaam kumpongeza kwa Cuba kumaliza Uchaguzi wa Rais salama.
Balozi Seif akitia saini Kitabu cha Wageni mara baada ya kukaribishwa kwenye Ubalozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Jijini  Dar es salaam.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziabr Balozi Seif  Kulia na Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Prifesa Lucas Domingo  Kushoto wakibadilishana mawazo kwenye Makaazi ya Balozi wa Cuba Jijini Dar es salaam.
Balozi Seif na Profesa Lucan akiangalia baadhi ya Picha na matukio mbali mbali yaliyojiri kwenye Maktaba ya Ubalozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi Kulia na Mke wa Balozi wa Cuba Nchini Tanzania Mama Melyin Suazez Alvarez  Kati kati Wakimfanyia mzaha Mtoto wa Mke wa Balozi Huyo aitwae Evelyn Hernandes Suarez.
Balozi Seif akiagana na Mke wa Balozi wa Jamuhuri ya Cuba Nchini Tanzania Mama  Melyin Suarez Alvarez. Kati kati yao ni Balozi Lucas Domingo Hernandes na Mtoto wake  Evelyn Hernandes Suarez. Picha na – OMPR – ZNZ.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad