HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 24 April 2018

Mafundi mitambo wa redio jamii watakiwa kutumia nafasi zao kuleta mabadiliko

Na Mwandishi wetu
Washiriki wa mafunzo ya ufundi mitambo ya kurushia matangazo ya redio ambayo yameshirikisha mafundi kutoka redio jamii 25 zilizopo Tanzania Bara na Zanzibar wametakiwa kutumia vyema mafunzo ili yakalete mabadiliko katika maeneo yao ya kazi.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mwandisi Upendo Mbele wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo ya siku saba ambayo yameandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).

Mbele alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatawapa uwezo wa kujua vifaa ambavyo wanavitumia katika vituo vyao na hivyo ni vyema wakayatumia vizuri ili yalete mabadiliko katika maeneo ya kazi.

"Ukiwa fundi mafunzo ni lazima, tuwashukuru UNESCO kuandaa mafunzo haya na nyie mtumieni muda wenu vizuri mkiwa hapa. Lengo kuu la kuwa hapa ni kujenga na kuboresha kile kitu ambacho hakikuwepo, unavyokuwa na upana zaidi na wewe utakuja kuwa mwalimu kwa wengine," alisema Mbele na kuongeza.

"Mkikaa pamoja tunaamini mtabadilishana ujuzi kuhusu mambo mbalimbali, lakini kama mkifika na mkawa mnatumia tu mitandao mtatoka kama mlivyoingia. Tumeambiwa kuwa tutakuja kuangalia kwenye vituo vyenu kama mafunzo mnayopewa hapa mnaelewa, maana isije mkatoka hapa alafu mkarudi kule mkawa mnafanya tofauti."

Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni fundi na mwandishi wa habari wa redio Kahama FM, Bakari Khaled alisema ni mambo mengi wamejifunza katika mafunzo hayo ambayo kwa namna moja au nyingine yatawasaidia kutatua matatizo ya ufundi ambayo yanawakabili.

"Tumekuwa tukinufaika na mafunzo haya, yametusaidia sana, redio jamii nyingi hazina uwezo wa kuajiri mafundi kabisa katika vituo na badala yake wana mafundi ambao wanawatumia kunapotokea tatizo, lakini kwa sisi ambao tumepata uzoefu na ujuzi huu matatizo madogo ambayo yanatokea tunayafanya wenyewe,

"UNESCO wamekuwa wakitusaidia sana, kwa sasa redio jamii zimetoka katika hatua ya chini na sasa zimekua hata kushindana na redio zengine za kibiashara, na TBC wamekuwa wakitufunza mambo mengi sana kwahiyo tukienda kujifunza pale tunaona kwa macho kwamba hiki kilitumika wakati wa analog na hiki ni digital, mafunzo haya yametujenga sana," alisema Khaled.
 Mkurugenzi wa Idara ya Ufundi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Mwandisi Upendo Mbele wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya ufundi mitambo ya kurushia matangazo ya redio kwa mafundi mitambo wa redio jamii 25 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambayo yameandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
 Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya ufundi mitambo ya kurushia matangazo ya redio kwa mafundi mitambo wa redio jamii 25 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambayo yameandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
 Washiriki wa mafunzo ya ufundi wa kurushia matangazo ya redio kwa mafundi mitambo wa redio jamii 25 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wakipewa maelezo kuhusu matumizi ya mitambo hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad