HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, March 9, 2018

MKUTANO WA MPANGO KAZI WA WATAALAM WA MALARIA KUTOKA MAREKANI NA ZANZIBAR WAFANA

Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Wataalamu wa maswala ya afya wametakiwa kutanua wigo katika Tafiti zao na wajikite zaidi katika tafiti za maradhi yatokanayo na vyanzo vya maji (Water born diseases)

Maradhi hayo ambayo hutokana na maji ikiwemo Kichocho, Matende, Minyoo, Vikope na Malaria huchukua asilimia 60 ya maradhi yanayowasumbua wananchi.

Waziri wa Afya wa Zanzibar Hamad Rashid Mohamed ametoa wito huo alipokuwa akizindua Mpango kazi wa Wataalam wa Malaria kutoka Shirika la Misaada la Marekani na Wizara ya Afya Zanzibar uliofanyika Ukumbi wa Hotel ya Ngalawa mjini Unguja.

Amesema tafiti zitakapofanywa juu ya maradhi hayo zitabainisha chanzo na njia nzuri za kujikinga na mwisho kuifanya Zanzibar kuwa sehemu isiyosumbuliwa na magonjwa hayo.

Waziri Hamad amefahamisha kuwa licha ya Zanzibar kupiga hatua kubwa katika kudhibiti ugonjwa wa malaria bado juhudi zinahitajika za kutokomeza moja kwa moja malaria ifikapo mwaka 2023.

Amesema miongoni mwa juhudi hizo ni pamoja na jamii kutoa mashirkiano kwa Wataalam wa afya ikiwemo kulalia vyandarua vilivyowekewa dawa za Malaria.

Amefahamisha kuwa Chandarua kilichowekwa Dawa ya malaria hudumu kwa takriban mwaka mmoja hivyo Wananchi wanapaswa kujilinda dhidi wa Mbu wanaoeneza ugonjwa huo.

Waziri Hamad ameisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha dawa za matibabu ya ugonjwa wa malaria na dawa za magonjwa mengine zinapatikana wakati wote.

Aidha ameongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuongeza nguvu zake kwenye kuuwa viluilui katika madimbwi ba maeneo maalum ili kusaidia miakakati ya upigaji dawa majumbani.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya ameushukuru Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI) kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kila hatua.

Awali Mkuu wa kitengo cha kupambana na Malaria Zanzibar Dkt. Abdalla Ali amesema Zanzibar imebaki hatika hali yake nzuri ya kupambana na ugonjwa wa Malaria toka mwaka 2007 ambapo hadi sasa maambukizi yapo chini ya asilimia 1.

Hata hivyo ameyataja maeneneo ya Wilaya za Kati, Magharibi B na Wilaya ya Micheweni kuwa ni miongoni mwa maeneo ambayo yanaendelea kuathiriwa na ugonjwa huo.

Akitaja Vipaumbele vya Kitengo cha malaria Dkt Abdalla amesema kwa mwaka 2019-2020 kitengo kitaendelea kufuatilia Wagonjwa wa malaria kwa uangalizi wa hali ya juu.

Amesema kwa mwaka huu eneo litakalobainika kutokea Mgonjwa wa Malaria watalazimika kuwapima watu wa familia na majirani ili kunusuru ongezeko la maradhi hayo.

Zanzibar kwa muda mrefu imekuwa ikipokea msaada kutokana Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI) na kuiwezesha Zanzibar kuwa mfano wa kuigwa katika mapambo dhidi ya ugonjwa huo.
 Naibu Waziri wa Afya Harusi Said Suleiman akitoa salamu zake kabl ya kumkaribisha Waziri wa Afya kufungua mkutano wa Mpango kazi wa Wataalam wa Malaria kutoka Shirika la Misaada la Marekani na Wizara ya Afya Zanzibar uliofanyika Ukumbi wa Hotel ya NGalawa mjini Unguja. Picha na Abdalla Omar-Maelezo Zanzibar.
 Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akisoma hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Mpango kazi wa Wataalam wa Malaria kutoka Shirika la Misaada la Marekani na Wizara ya Afya Zanzibar uliofanyika Ukumbi wa Hotel ya NGalawa mjini Unguja. Picha na Abdalla Omar-Maelezo Zanzibar
 Katibu Mkuu Wizara ya Afya Asha Abdulla akitoa neno la shukran kwa Mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI) kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali kila hatua. 
 Mkuu wa kitengo cha kupambana na Malaria Zanzibar Dkt. Abdalla Ali akiwasilisha taarifa ya tahmini ya hatua walizozichukua za kupambana na Malaria kwa mwaka 2017 na mikakati yao kwa mwaka huu mbele ya Wajumbe walioshiriki Mkutano wa Mpango kazi wa Wataalam wa Malaria Zanzibar. 
 Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Mpango kazi wa Wataalam wa Malaria kutoka Shirika la Misaada la Marekani (PMI) na Wizara ya Afya Zanzibar uliofanyika Ukumbi wa Hotel ya NGalawa mjini Unguja.Mkutano huo umefunguliwa na Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed-Picha na Abdalla Omar-Maelezo Zanzibar
Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad