HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, March 26, 2018

MKURUGENZI MKUU MSD AMTAJIA RAIS MAGUFULI CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI

Na Said Mwishehe, Globu ya Jamii
MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Lauraean Bwanakunu pamoja na mafanikio ambayo wameyapata katika kutekeleza majukumu yao ya kununua, kusambaza, kutunza na kusambaza dawa na vifaa tiba, changamoto inayowakabili ni ya ununuzi wa vifaa vya kitaalam toka wazalishaji.

Ametaja baadhi ya vifaa hivyo ni  vya macho, meno, moyo na  figo ambapo vinaagizwa kwa uchache na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI),Hospitali ya Taifa Muhimbili(MNH) na ORIC.

Azungumza leo jijini Dar es Salaam mbele ya Rais John Magufuli  wakati wa uzinduzi wa magari mapya ya msaada ya kusambaza dawa ambayo yametolewa na Global Fund kwa MSD, Bwanakunu amesema wazalishaji wa vifaa hivyo wanaona oda ni ndogo na hivyo wamekuwa na wakati mgumu kupata.

Amemhakikishia Rais Magufuli kuwa, MSD wamejipanga kukabiliana na changamoto hiyo na mwezi ujao watazungumza na Shirika la IDA lililopo Denmark na wengine ili kuwakusanyia vifaa hivyo pamoja na nchi nyingine kwa lengo la kuwapunguzia gharama za manunuzi.

Amesema kampuni hizo hufanya manunuzi ya nchi mbalimbali ikiwemo umoja wa mataifa na hivyo wanataka kufaidika na mfumo huo.

Bwanakunu amemueleza Rais Magufuli , changamoto ya pili wanayokabiliana nayo ni ya maoteo kutokana na kutokuwa sahihi na kufanya suala la ununuzi kuwa la kubahatisha.

Akizungumzia kuongezeka kwa bajeti ya kununua dawa kutoka Sh.bilioni 31 hadi Sh.bilioni 250, Bwanakunu amesema yale yalikuwa maajabu na kama ndoto na kila mtu kwenye mnyororo wa ugavi alichanganyikiwa ghafla.

"Kuna zahanati ilikuwa inapata dawa za Sh.400,000 kwa mwaka na sasa inapata Sh.milioni 10. Furaha hii haikuwa kwa vituo vya kutolea huduma za afya , watumishi wa afya lakini zaidi sisi watumishi wa MSD umetuondolea kero ya Watanzania kudhani mtu akiumwa na mbwa au nyoka basi shida ni MSD wakati hatuna fedha za kununua dawa hizo.

"Kwa sasa tunatembea kifua mbele .Aidha ni muhimu pia tukafahamu kuwa MSD inanunua dawa zenye jumla ya Sh.bilioni 460 kwa fedha za Serikali na wafadhili kila mwaka ni Sh.bilioni 28.Tena hizi ni za miaka miwili tu ndizo zinazotumika kwa viwanda vya ndani kutokana na viwanda vya uzalishaji wa dawa kuwa vichache na uwezo wa kuhudumia mahitaji ya MSD,"amesema.

Amefafanua kwa wastani wananunua dawa za Sh.bilioni 21 kwa mwezi na kutumia nafasi hiyo kumueleza Rais ni kiasi gani cha fedha kinakwenda nje ya nchi.

Bwanakunu amemwambia Rais Magufuli kuwa,  MSD imejipanga kuhakikisha magari hayo mapya yanaleta tija iliyokusudiwa na kueleza wamechukua hatua kadhaa kuhakikisha magari hayo yanafanya kazi kwa ufanisi na yanakuwa katika hali nzuri.

Kwa upande wake Rais Magufuli akizungumzia MSD ameipongeza kwa kazi nzuri ambayo ameifanya na kwamba anaridhishwa na utendaji kazi wao na kutumia nafasi hiyo kumhakikishia Bwanakunu kuwa hata akitaka kupandisha mishahara ya watumishi atakuwa tayari kukubali maombi yao.

Amesema anakumbuka kuna wakati mkurugenzi huyo wa MSD alikuwa anapigwa madongo lakini amemhakikishia achape kazi na yeye ndio mkurugenzi huku akisisitiza kuelezea namna ambavyo afurahishwa na taasisi hiyo inayofanya kazi kizalendo.

"MSD mnafanya kazi nzuri sana, nimesema kutoka moyoni mnanifurahisha na lazima niwapongeze.Mimi ni mgumu kupongeza hivyo ukiona natoa pongezi mjue nimeridhishwa na mnachokifanya.

"Endeleeni kuongeza maduka ya dawa na kama watumishi ni wachache basi ongezeni wengine.Msikubali kuwatumia watu wa halmashauri maana nawajua kule kuna wajanja wengi watawakwamisha.Tamisemi iko chini yangu hivyo nawajua.Msifanye kazi na halmashauri fanyeni wenyewe kwa kutumia watumishi wenu,"amesema Rais Magufuli.
Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Kuu ya Madawa, Laurean Bwanakunu akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi magari 181 yatakayokuwa yakisafirisha vifaa tiba na vitendanishi katika Mikoa na Halmashauri mbalimbali nchini. Hafla hiyo ilifanyika leo Jumatatu Machi 26, 2018 katika Ofisi za MSD Keko Mwanga Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad