HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 29, 2018

Mbulu yapatiwa fedha za kuhamia Haydom

Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, imepokea kutoka serikali kuu kiasi cha sh1 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa makao makuu mapya yatakayojengwa Mji mdogo wa Haydom. 

Pia, kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 Halmashauri hiyo imetengewa sh. 2.3 bilioni za ujenzi wa jengo la ofisi na nyumba za kuishi watumishi. 

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hudson Kamoga aliyasema hayo jana wakati akizungumza juu ya mikakati ya ujenzi wa makao makuu mapya yatakayojengwa Haydom. 

Alisema baada ya kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo kupitisha uamuzi wa ujenzi wa makao makuu ya halmashauri hiyo kuwa Haydom, hivi sasa wapo kwenye mchakato wa utekelezaji. 

"Hadi mwakani kipindi kama hiki tutakuwa tumeshahamia kwenye makao makuu mapya ya halmashauri yetu kule Haydom na kuondoka hapa Mbulu mjini," alisema Kamoga. 

Alisema awali Mbulu iligawanywa mwaka 2015 na kuwa na halmashauri mbili ya mji na wilaya, hivyo huu ni wakati wa kujenga ofisi zao mpya kwa lengo la kusogeza huduma za jamii karibu na wananchi. 

"Tunaishukuru serikali inayoongozwa  na Rais John Magufuli kwa kutupatia fedha hizo za ujenzi wa makao makuu mapya ya halmashauri yetu ya wilaya," alisema Kamoga. 

Mkazi wa mji mdogo wa Haydom, Paul John alishukuru uamuzi wa kujengwa makao makuu mapya kwenye eneo hilo tofauti na uamuzi wa awali wa kujenga Dongobesh. 

"Huku kuna huduma mbalimbali za kijamii nyingi ikiwemo kituo kikubwa cha polisi, benki hospitali kubwa, tofauti na Dongobesh ambayo haina hata benki," alisema John. 

Mkazi wa Dongobesh Aloyce Martin alisema kuenea kwa unywaji na biashara ya pombe haramu ya gongo kwenye eneo hilo kumewagharimu hadi kusababisha makao makuu mapya ya halmashauri hiyo yakahamishiwa Haydom. 

"Makosa ni ya kwetu sisi wenyewe kwani tulipata nafasi badala ya kuitumia ipasavyo sisi tukaichezea hadi ikawadondokea watu wa Haydom," alisema Martin. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akimkabidhi zawadi ya daftari mwanafunzi wa darasa la tatu wa shule ya msingi Barazani Kata ya Maghang, Julieth John kutokana na utunzaji bora wa vyanzo vya maji na mazingira, kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mkoani Manyara, Hudson Kamoga akizungumza na wananchi wa Kata ya Maghang juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad