HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 15, 2018

MAKAMU WA RAIS MGENI RASMI HARAMBEE YA KUCHANGISHA FEDHA KWA AJILI YA UJENZI WA HOSPITALI WILAYA YA MUHEZA

*Kufanyika kesho jijini Dar es Salaam, Mhandisi Tumbo aomba wananchi kuchangia ili kufanikisha ujenzi huo

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
MKUU wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Mhandisi Mwanasha Tumbo amewaomba wananchi wa wilaya hiyo na Watanzania kwa ujumla kuchangia ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo ambapo kesho Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye harembee ya uchagiaji fedha kufanikisha ujenzi huo.

Kwa sasa Wilaya hiyo haina Hospitali ya Wilaya na wananchi wanaohitaji huduma za afya wamekuwa wakitumia hospitali teule ya Kanisa la Anglikana ambayo imeingia mkataba na Serikali na kutokana na idadi ya wananchi wa wilayani hapo hospitali hiyo imezidiwa.

Hayo yamesemwa leo na Mhandisi Tumbo wakati akizungumzia harambee ya kuchangisha fedha inayotarajia kufanyika kesho jijini Dar es Salaam kwa lengo la kufanikisha ujenzi wa Hospitali mpya ya Wilaya hiyo.

Mhandisi Tumbo amesema kutokana na Wilaya ya Muheza kutokuwa na Hospitali ya Wilaya tangu kuanzishwa kwake mwaka 1974, wananchi wamekuwa wakiteseka pindi wanapohitaji huduma za afya na hivyo wakaamua kuchanishana fedha ili kuanza ujenzi wa hospitali hiyo.

Amefafanua tayari wananchi na wadau wa maendeleo wilayani Muheza mkoani Tanga na Watanzania kwa ujumla wameanza kuchingiaa ujenzi huo na hadi kukamilika kwake zinahitajika fedha Sh.bilioni 11.1, hivyo wakati wakisubiri fedha za Serikali Kuu na zile za kwenye bajeti wameamua kuanza kwa kuchangisha fedha hizo.

"Kesho tutakuwa na harambee itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni ambapo wananchi wa Wilaya ya Muheza wanaoishi Dar es Salaam pamoja na watanzania wengine tunaomba wajitokeze kuchanga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya.

"Mgeni rasmi kwenye tukio hilo la harembee ya kuchangisha fedha atakuwa Makamu wa Rais ,Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa wachangiaji ambao tumewapa kadi ya kuja kwenye harembee hiyo kila mchangiaji atachangia kuanzia Sh.milioni moja kwa walio na kadi.Na wote ambao tumewaalika kesho wana kadi za mualiko,"amsema.

Amefafanua kwa wale ambao wanahitaji kadi ni vema wakawasiliana naye kwa kutumia namba yake ya simu ya mkononi ya 0713 341937 ili wapatiwe kadi huku akifafanua pia mbali ya wale ambao watafika kesho kwenye harambee hiyo pia wameandaaa utaratibu mwingine wa kuchangia ujenzi huo.

Mhandisi Tumbo amesema ili kufanikisha ujenzi huo wanapokea mchango wa kiasi chochote cha fedha na hao wachangie kupitia Tigopesa au M-pesa kwa kutumia namba 395533 ambayo kumbukumbu namba ya kampuni ni 123.

"Tunatambua jitihada za Serikali katika kutatua changamoto kwenye sekta ya afya, na hasa Muheza lakini kwa upande wetu tumeamua kuanza kwa kuchangishana, wapo wanaotoa fedha, wapo wanaochangia kokote, mchanga , saruji na vifaa vingine vya ujenzi.Tumeanza vizuri kwani tayari msingi wa wadi ya akina mama na watoto umejengwa na lengo letu hadi Oktoba mwaka huu tuwe tumekamilisha ili wananchi wapate huduma za afya.

"Tukifanikiwa kuwa na Hospitali ya Wilaya Muheza mwananchi anayehitaji huduma za matibabu ya afya atakuwa na nafasi ya kuchagua aende kwenye Hospitali ya Anglikana au ya Wilaya.Niishukuru Hospitali ya Anglikana kutokana na kutoa huduma za tiba kwa wananchi wa Muheza,"amesema Mhandisi Tumbo.

Pia amesema wakati wanaendelea kutafuta fedha kujenga Hospitali ya Wilaya ya Muheza, wanaendelea na jitihada za kujenga zahanati na ujenzi huo unaendelea kwa kasi kutokana na wananchi kuhamasika kuchangia ili kuondoa changamoto ya uhaba wa zahanati za vituo vya afya.
Mkuu wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Mhandisi Mwanasha Tumbo(wa kwanza kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu harambee ya uchangiaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya ya Muheza katika ukumbi wa Golden Tulp jijini Dar es Salaam leo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad