HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, March 8, 2018

KAIMU MKURUGENZI MTENDAJI MPYA WA STAMICO KANALI SYLIVESTER DAMIAN GHULIKU AKABIDHIWA OFISI

Na Koleta Njelekela, Stamico Dar Es Salaam
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO Kanali Sylivester Damian Ghuliku amekabidhiwa rasmi Ofisi na aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO Mhandisi John Nayopa na kuanza kazi rasmi tarehe 05 Machi, 2018.

Makabidhiano hayo yamefanyika Makao Makuu ya STAMICO yaliyopo barabara ya Umoja wa Mataifa, Upanga jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya STAMICO Balozi Alexander Muganda.

Akizungumza katika hafla hiyo fupi ya makabidhiano, Mhandisi Nayopa amesema STAMICO inajukumu kubwa la kusimamia rasilimali za madini kwa niaba ya Serikali pamoja na kuwekeza katika Miradi ya Kimkakati ya Uchimbaji Madini, ili kuongeza mchango wa madini katika Pato la Taifa.

Amemshauri Kanali Ghuliku kuendeleza ushirikiano na Serikali, Wizara ya Madini na wadau katika kutekeleza miradi ya ubia na isiyo ya ubia; kuendesha kampuni zake tanzu na kuendeleza leseni za uchimbaji pamoja na shughuli za wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Kanali Ghuliku, ambaye ni Mhandisi Mitambo,  alimpongeza Mhandisi Nayopa kwa utendaji kazi makini na ubunifu wake katika harakati za kutekeleza miradi ya Shirika na ameahidi kuyaendeleza mema yote aliyoyakuta yenye nia ya kuliinua Shirika.

Mhandisi Nayopa pia alitumia fursa hiyo kuwaaga wafanyakazi kupitia Kikao Maalum cha kumtambulisha Kanali Ghuliku kwa wafanyakazi ambacho kiliendeshwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa STAMICO Balozi Alexander Muganda.

Akizungumza baada ya utambulisho huo, Balozi Muganda aliwataka Menejimenti na Wafanyakazi kumpa ushirikiano Kanali Ghuliku na kutanguliza mbele ubunifu katika kutekeleza miradi ya Shirika na kulinda maslahi mapana ya Taifa.

Katika salaam zake kwa Wafanyakazi kama Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO, Kanali Ghuliku aliwaeleza Wafanyakazi kuwa ameukubali kwa moyo mmoja uteuzi huo uliofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa Simon Msanjila na aliwataka Wafanyakazi wampe ushirikiano ili malengo ya Shirika yaweze kufikiwa ipasavyo na kwa wakati.

“STAMICO haiwezi kukua na kustawi kwa nguvu ya mtu mmoja, bali itaendelea kustawi ikiwa wafanyakazi tutafanya kazi kwa ushirikiano kwa lengo la kuleta maendeleo kwenye Shirika. Mazuri aliyofanya Engineer Nayopa hatuna budi kuyaendeleza kwa manufaa ya Shirika” alisisitiza Kanali Ghuliku.

Kabla ya uteuzi huo, Kanali Ghuliku alikuwa Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uhandisi Umeme na Mitambo, Tawi la Ugavi na Uhandisi katika Makao Makuu ya Jeshi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa zamani wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Mhandisi John Nayopa (kulia) akimkabidhi taarifa ya Utendaji Kazi ya Shirika Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mpya wa Shirika hilo Kanali Sylivester Damian Ghuliku(kushoto) katika hafla fupi iliyofanyika katika Ofisi za Makao Makuu ya STAMICO zilizoko jijini Dar es Salaam.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO, Kanali Sylivester Damian Ghuliku akiwa katika picha ya pamoja Viongozi wa STAMICO na Wafanyakazi mara baada kukabidhiwa ofisi hiyo tayari kwa kuanza utekelezaji wa majukumu ya STAMICO.
Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa STAMICO, Deus Magala(kushoto) akikabidhi Clients Service Charter ya Shirika kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO, Kanali Sylivester Damian Ghuliku(kulia) mara baada ya Kiongozi huyo kukabidhiwa ofisi na kusaliamiana na Wafanyakazi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad