HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, 15 March 2018

AFANDE SELE AJIUNGA CCM RASMI MBELE YA RAIS DKT JOHN MAGUFULI

Na Leandra Gabriel, Globu ya jamii
MSANII maarufu nchini katika muziki wa kizazi kipya Selemen Msindia a.k.a Afande Sele amesema amefurahishwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli na kwamba amekuwa mbishi wa kukubali lakini kazi ya Rais imemfanya aamue kumfuata Chama Cha Mapinduzi(CCM).

Afande Sele amesema kuwa anamfananisha Rais Magufuli kama dereva wa gari ambaye analiendesha vema na yeye kama abiria ametulia anakunywa soda yake na hivyo anachoweza kumlipa kwa vitendo ni kujiunga CCM ili ashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Taifa.

Msanii huyo amesema hayo leo mchana huu mbele ya Rais Magufuli aliyeko mkoani Morogoro ambako kuna tukio la kufanyika uzinduzi wa Kiwanda cha Sigara cha Philip Moris kilichopo Kingolwira mkoani hapo.

"Nimekuwa ni mtu wa kufikiria na kubisha hadi pale ninapojiridhisha.Naomba nitumie nafasi hii kumwambia Rais Magufuli tangu umekuwa Rais umefanya kazi kubwa ambayo binafsi na Watanzania wengine imenivutia. Kuanzia muda huu naomba Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro mnipokee rasmi.

"Utendaji kazi wa Rais Magufuli umenifanya nikubali kwa ridhaa yangu niwe upande wake.Nchi inakwenda na mambo mengi yanafanyika kwa ajili yetu na hata mataifa mengine duniani yanajua kazi ambayo inafanywa na Rais wetu,"amesema Afande Sele.

Baada ya kutangaza uamuzi huo, wananchi waliokuwa mbele ya Rais walianza kushangilia kwa shangwe huku wengine wakipiga kelele kuonesha furaha yao kutokana na uamuzi wa msanii huyo kujiunga CCM. Afande Sele amekuwa vyama vya upinzani kwa muda mrefu na historia yake inaonesha amewahi kupita CUF,Chadema na ACT-Wazalendo na leo amejiunga CCM rasmi.

No comments:

Post a comment

Post Bottom Ad