HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 20 February 2018

WAZIRI JAFO KUWAVALIA NJUGA WAWEKEZAJI WENYE MASHAMBA PORI AMBAYO HAWAKUYAENDELEZA

WAZIRI  wa Nchi ofisi ya Rais Tamisemi  Selemani Jafo amesema hawezi kuwavumilia hata kidogo baadhi ya wawekezaji ambao wamekuwa na tabia ya  kufanya  udang’anyifu kwa wananchi kutokana na kuchukua maeneo makubwa ya ardhi pasipo kuyaendeleza mpaka yanapelekea kuwa mashamba pori hivyo ameagiza yarudishwe katika mikono ya serikali za vijiji ili wananchi wenyewe waweze kuyaendeleza katika shughuli nyingine za kimaendeleo.

Jafo ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kikazi kwa wananchi wa kijiji cha Kimara Misale kilichopo kata ya Mafizi katika halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe ambapo amekwenda kwa ajili ya kuweza kujionea  na kutembelea miradi mbali mbali ya maendeleo pamoja na kuweza kusikiliza changamoto ambazo zinawakabili wananchi wa jimbo lake.

Amesema kumekuwepo na wimbi kubwa la mashamba pori katika baadhi ya maeneo  ambayo kwa kipindi cha muda mrefu  yametelekezwa hivyo  ameahidi kulivalia njuga suala hilo kwa lengo la kuweza kuwapa fursa wananchi waweze kurudishiwa maeneo yao ambayo yamechukuliwa na watu wachache ambao wameshindwa kabisa  kuyaendeleza kama inavyostahili.

Aidha Waziri Jafo katika hatua nyingine  ametoa muda wa  siku 30 kwa watendaji wa idara ya ardhi ya halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha wanamaliza mgogoro wa mipaka ya  ardhi uliopo baina ya wananchi wa kijiji cha Kimara misale kata ya mafizi na  baadhi ya vijiji vingine ambavyo vipo katika halmashauri ya Kibaha vijijini.

Awali  baadhi ya wananchi hao akiwemo  Issa Zoka na Salumu Hombo  wakitoa malalamiko yao kwa niaba ya wenzao kwa  Waziri katika mkutano wa adhara wamesema kumekuwepo na migogoro kila kukicha  ya kugombania mipaka ambayo inachangia wakati mwingine kutoelewana kwa watendaji na viongozi katika suala la  ukusanyaji wa mapato na mambo mengine ya  kufanya maendeleo.

KUWEPO kwa ongezeko la mashamaba pori katika baadhi ya maeneo hapa nchini hususan katika Wilaya ya Kisarawe iliyopo Mkoa wa Pwani ni kutokana na baadhi ya wawekezaji kununua ardhi kwa makubaliano ya kuwekeza katika ujenzi wa  huduma mbali mbai za kijamii ikiwemo shule, zahanati, masoko lakini mwisho wa siku wanayatelekeza na wengine kuyatumia kuchukulia  mikopo benki.
 Waziri wa nchi ofisi ya Rais Tamisemi Seleman Jafo akizungumza na wananchi wa kijiji cha  kimara misale iliyopo kata ya Mafizi Wilayani Kisarawe wakati wa ziara yake ya kikazi kwa ajili ya kukagua miradi mbai mbai ya maendeleo na kuweza kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili wananchi ii kuweza kuzitafutia ufumbuzi.
Baadhi ya viongozi wa halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wakiwa katika mkutano wa adhara kumsikiliza Waziri jafo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kujionea miradi mbai mbali ya kimaendeleo inayotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na nguvu za wananchi wenyewe.(PICHA  ZOTE NA VICTOR MASANGU)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad