HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 22, 2018

WANAWAKE GAIRO WAONGOZA KIMKOA KUJIFUNGUA WAKIWA NA UMRI CHINI YA MIAKA 20

Na John Nditi, Gairo
WANAWAKE wajawazito 2,600  sawa na asilimia 27   kati ya 9,577 waliojifungulia  zahanati na vituo vya afya  kwa mwaka 2017 katika halmashauri ya wilaya ya Gairo , mkoani Morogoro walibainika  kuwa  chini  umri wa  miaka 20.

Hali hiyo ilisababisha  kujitokeza  kwa vifo  vitokanavyo na uzazi pingamizi unaochagiwa na uchungu mkali,  kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua  na kifafa cha mimba.

Mratibu wa Afya  ya Mama na Mtoto wa wilaya ya Gairo, Edifonzia Mhafigwa alisema hayo   wakati akiwasilisha taarifa katika   mkutano wa kujadili utoaji wa elimu kuhusu kutokomeza vifo vitokanavyo na uzazi kwenye   siku ya  Utepe Mweupe ambayo  kimkoa ilifanyika  katika  kata ya Ukwamani , wilayani humo.

Mbali na changamoto hiyo, wanawake wajawazito waliojifungulia kwa wakunga wa jadi  kwa mwaka 2017 walifikia 1,270 , waliojifungulia njiani  ni 108 , waliojifungulia nyumbani ni 180 na kwenye  Zahanati walikuwa ni 3,482.

Alisema  , jambo hilo linachangiwa na mambo mbalimbali yakiwemo ya wanawake wajawazito kushindwa kuhudhuria kliniki kwa wakati ama kuchelewa kufijkishwa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa ajili ya kujifungua .

Naye Mratibu wa Afya ya uzazi na mtoto mkoa wa Morogoro, Annua Mhogo alisema kuwa , mkoa huo una vituo 341 vya huduma za afya ya uzazi kwa mama na mtoto (RCH), Vituo vinavyotoa elimu ya uzazi wa mpango 282  na  vituo vya kujifungulia  ni 298.

Mhogo alisema , watoto waliozaliwa kwa mwaka 2017 walikuwa ni 73,232 , ambapo vifo vya watoto chini ya miaka mitano vilikuwa ni 1,335 wakati vifo vya akina mama wajawazito  wakati wa kujifungua ama baada ya kujifungua walikuwa ni 80.

Alisema  takwimu za kimkoa  zinaonesha  kuwa wilaya hiyo  inaongoza  kuwa na  idadi ya  akina mama wanaojifungulia  kwa wakunga wa jadi na mimba za utotoni ambao wanaozeshwa  wakiwa bado na umri mdogo.

Naye Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania , Rose Mlay aliishauri Serikali kuendelea kuongeza wataaamu wa sekta ya afya wakiwemo wauguzi wenye ujuzi hasa kwenye zahanati vijijini ili kupunguza vifo hivyo.

Mlay pia aliwataka wanaume  kuwajali wake zao wanapokuwa wajawazito kuwasindikiza kliniki ili elimu itakayotolewa na wataalamu wa afya hasa waauguzi iwe ni chachu ya kuhakikisha  usalama wa mama na kiumbe kilichomo tumoni mwa mama mjamzito ili awezefungue salama katika vituo vya afya ama zananati yenye  mtaalamu.

Nao baadhi ya wakazi wa Gairo ,Elieza Ernest ,Julieti Sangara , Lucia James pamoja na Andason Ndajiro  kwa nyakati tofauti walisema  ukosefu wa zahanati za kutosha katika vijiji vingi ni miongoni mwa  changamoto zinazowakabili akina mama wajawazito.

Walisema , hali hiyo inawalazimu  kutembea umbali mrefu kuzifuata zahanati na vituo vya afya kuhudhuria kliniki  wakati hawana kipato cha kuwawezesha kugharamia  usafiri.

Hivyo walishauri ,  halmashauri ya wilaya ya Gairo kuweka utaratibu wa kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa zahanati na vituo vya afya pamoja na kuwasambaza wauguzi na madaktari wa kutoka na vitendea kazi na dawa .

Kwa upande wake  Mganga mkuu wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Dk Dennis Ngalomba  alisema,  halmashauri hiyo  ina vijiji 50  na kata 18 ambapo kulingana na sera ya afya ya kila kata iwe na  kituo cha afya,  upungufu ni  vituo 17  , wakati zahanati zilizopo ni 24 na upungufu ni 26.

Hata hivyo alisema , jukumu la wananchi ni kuanzisha maboma na halmashauri itaendelea kumalizia kupaua hadi hatua ya kusajili zanahati na vituo vya afya juhudi  ambazo zinaendelea kutekelezwa na uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo.
 Katibu Tawala wa wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, Adam Bibangamba ( aliyesimama) akitoa hotuba yake ya  ufunguzi wa mjadala wa elimu  juu ya  njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi kwa  wanawake wajawazito  na kupinga mimba za utotoni  wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika  kata ya Ukwamani , wilayani humo. ( Picha na John Nditi).
Mkazi wa  Kata ya Ukwamani , wilaya ya Gairo akichangia mada
  Baadhi ya wananchi  wa kata ya Ukwamani , wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro wakisiiliza na kusoma vipeperushi vya  elimu  ya  njia ya kupunguza vifo vitokanavyo  na uzazi vya akina mama wajawazito na kupinga mimba za utotoni, wakati wa mjadala wa uelimisghaji jamiii  siku ya utepe mweupe iliyofanyika  kwenye kata hiyo.
Wazee wa  kata ya Ukwamani, wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro ( mstari wa mbele ) wakiwasikiliza wataalamu wa afya ( hawapo pichani) wakati wa utoaji wa elimu  ya  njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi kwa  akina mama wajawazito na kupinga vita  kujifungulia kwa wakunga wa jadi na  mimba za utotoni, wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika  kwenye kata hiyo.
 Mfanyakazi wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania, Lucy Nzuki ( mwenye kushika karatasi ) akiandika dodoso kwa mmoja wa wakazi wa Kata ya Ukwamani , wilaya ya Gairo , mkoa wa Morogoro wakati wa utoaji wa  elimu  ya  njia ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pingamizi kwa  wanawake wajawazito  na kupinga mimba za utotoni wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika  kwenye kata hiyo wilayani humo.
 Mratibu wa Taifa wa Muungano wa Utepe Mweupe Tanzania , Rose Mlay ( kushoto) akibadilishana mawazo na Mganga mkuu wa wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro , Dk Dennis Ngalomba ( kulia) na watendaji wengine wa wilaya hiyo mara baada ya kumalizika kwa majadiliano kati ya wananchi na wataalamu namna ya njia bora ya kupunguza vifo hivyo wakati wa  utoaji wa elimu  wakati wa siku ya utepe mweupe iliyofanyika  kata ya Ukwamani , wilayani humo , majadiliano hayo yalikuwa na ujumbe wa “ Vifo vitokanavyo na uzazi havivumiliki “ Wajibika.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad