Benki ya CRDB yasaini mkataba wa
hali bora kwa wafanyakazi wake na Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Fedha,
Biashara, Huduma na Ushauri (TUICO), katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya
Ramada Encore iliyopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Menejimenti
ya Benki ya CRDB na Viongozi wa TUICO.
Akizungumza na Waandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt.
Charles Kimei alisema mbali na kusaidia kuongeza morali na motisha ya utendaji kazi
kwa wafanyakazi, mkataba huo wa hali bora utakwenda kusaidia kuongeza ustawi kwa
wafanyakazi na familia zao na hivyo kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (katikati)
pamoja na Mkuu wa Sekta ya Fedha -TUICO Tanzania, Willy Kibona (kushoto)
wakisaini Mkataba wa Makubaliano wa hali bora za Wafanyakazi kati ya
Benki ya CRDB na Taasisi ya Fedha, Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri
(TUICO) katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es salaam leo Februari
15, 2018. Kulia ni Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB,
Dorah Ngaliga.
"Ustawi wa wafanyakazi ni muhimu sana kwetu na tunajitahidi kuhakikisha tunatoa
kipaumbele katika hili. Mkataba huu utakuwa ni wa kipindi cha miaka mitatu tangu
tarehe ya utiaji saini ambapo kuna mambo 19 ambayo kwa pamoja tumeyaridhia na
kuyapitisha”, alisema Dkt. Kimei.
Dkt. Kimei alisema katika mkataba huo wa hali bora kwa wafanyakazi, Benki ya CRDB
imetoa kipaumbele katika kuboresha afya za wafanyakazi wake. “Benki ya CRDB
imekuwa ikichangia asilimia 100 katika huduma za matibabu kwa wafanyakazi wake,
tunajivunia sana kwa hilo. Kutokana na mafanikio na umaarufu wa mpango huu
tunaoutumia, tumeamua kuboresha zaidi ahadi yetu kwa wafanyakazi wetu mara
nyingine tena, "alisema Dkt. Kimei.
Dkt. Kimei alisema kwa upande wa huduma za afya, wafanyakazi wa Benki ya CRDB
sasa wameongezewa huduma nyingine ikiwamo huduma za macho na miwani pamoja
na huduma ya matibabu kwa wastaafu na wategemezi wao kupitia Shirika la Bima ya
Afya ya Taifa (NHIF). Hii inamaanisha kuwa wafanyakazi wa Benki ya CRDB
wataendelea kutibiwa kama bado wapo kazini pindi wakistaafu.
Baadhi ya mambo mengine ambayo yaliridhiwa katika mkataba huo wa hali bora kwa
wafanyakazi wa Benki ya CRDB ni pamoja na utaratibu mpya wa uthibitishwaji wa
wafanyakazi kazini, utaratibu ulioboreshwa wa kushughulikia migogoro ya kikazi,
utaratibu wa likizo ya ugonjwa, utaratibu wa likizo ya uzazi, utaratibu wa mazishi
ambapo sasa Benki hiyo itagharamia mazishi ya wazazi wa mfanyakazi, mtoto wa
kuzaliwa wa mfanyakazi, au aliyeasiliwa pamoja utaratibu wa utoaji tuzo kwa
wafanyakazi wa Benki hiyo.
Akimalizia hotuba yake Dkt. Kimei alisema Benki CRDB pia imeanzisha Kamati za
Ustawi wa Wafanyakazi katika matawi yake yote kwa ajili ya kubuni na kuratibu
programu na shughuli mbalimbali zinazolenga kukuza ustawi wa wafanyakazi na familia
zao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei akibadilishana
Mkataba wa makubaliano na Mkuu wa Sekta ya Fedha -TUICO Tanzania, Willy
Kibona (wa pili kushoto) hali bora za Wafanyakazi kati ya Benki ya CRDB
na Taasisi ya Fedha,
Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri (TUICO) katika hafla fupi
iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Ramada, jijini Dar es salaam leo Februari 15, 2018.
Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Tully Mwambapa akizungumza jambo katika hafla fupi iliyofanyika jijini Dar es salaam leo Februari 15, 2018.
Baadhi washiriki
No comments:
Post a Comment