HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 1 February 2018

TBL yatoa ufafanuzi juu ya madai kudukuliwa mfumo wake wa taarifa, Yatangaza punguzo la bei ya rejareja kwa bia ya Castle Lite Premium Lager

Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), leo imetoa ufafanuzi juu ya taarifa zilizozagaa mitandaoni za kudukuliwa kwa mfumo wake wa kuhifadhi taarifa na kusisitiza kuwa mfumo wake huo wa taarifa uko salama baada ya kujiridhisha.

Mapema jana asubuhi kulionekana taarifa ya video kwenye mtandao wa YouTube ya mtu aliyevalia kofia iliyofunika uso (Mask) ikieleza kuwa, mfumo wa kuhifadhi taarifa wa TBL umedukuliwa na hivyo kuhatarisha kuvuja kwa taarifa zake muhimu.
Mkurugenzi wa Masoko wa TBL - Afrika Mashariki, Thomas Kemphuis akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam leo wakati akitolea ufafanuzi juu ya taarifa za kudukuliwa kwa mfumo wa mtandao wao wa kuhifadhi taarifa na kusisitiza kuwa mfumo wa taarifa zao zipo salama. Kushoto ni Meneja Masoko, Udhamini, Habari na Promosheni za Wateja - Afrika Mashariki, George Kavishe na Kulia ni Meneja Mawasiliano ya Nje wa TBL, Zena Tenga.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Masoko wa TBL - Afrika Mashariki, Thomas Kemphuis alisema, baada ya uchunguzi wa kina kampuni hiyo imejiridhisha pasipo na shaka kuwa hakuna tukio la aina hiyo lililotokea na kusisitiza taarifa zake zipo salama huku ikiwataka wanahisa wake, wadau pamoja na umma kwa ujumla kutokuwa na wasiwasi.

Akisisitiza nia ya TBL kuendelea kutoa huduma bora, Kemphuis alisema kampuni hiyo inachukulia kwa uzito mkubwa suala la usalama wa mifumo yake na ndiyo sababu ya kufanya uchunguzi wa haraka na wakina mara baada ya kupata taarifa za uvumi juu ya udukuzi.
Meneja Masoko, Udhamini, Habari na Promosheni za Wateja - Afrika Mashariki, George Kavishe akifafanua jambo.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa TBL itaendelea kutengeneza mifumo imara ya ulinzi wa taarifa zake ili kuepuka matukio yasiyotarajiwa kama udukuzi. Wakati huo huo, TBL imetangaza habari njema kwa wateja wake baada ya kutoa punguzo la bei kwa bia yake pendwa ya Castle Lite Premium Lager kutoka bei ya sasa ya shilingi elfu 2,500 hadi shilingi 2,000.

Kwa mujibu wa Kemphuis, punguzo hilo la bei ni zawadi kwa wateja wa bia hiyo kwa kuwa wateja waaminifu na zaidi kwa kuiunga mkono kampuni ya TBL kupitia bidhaa zake. “Kupunguza bei ya bia ya Castle Lite Premium Lager kunadhihirisha shukrani zetu kwa wateja wetu kwa kutuunga mkono kwa kipindi kirefu. TBL siku zote ipo tayari kuwasikiliza wateja wake na kuwapa kile wanachokitaka,” alibainisha. #CastleLiteHacked

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad