HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, February 2, 2018

RAIS MAGUFULI AMLILIA MZEE KINGUNGE NGOMBALE MWIRU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa waasisi wa Taifa na mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea leo tarehe 02 Februari, 2018 saa 10:30 alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake Jijini Dar es Salaam tarehe 22 Desemba, 2017.

Mhe. Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.

“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu” amesema Mhe. Rais Magufuli.

Kufuatia msiba huu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu, na amewaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.

Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu Kingunge Ngombale Mwiru mahali pema peponi, Amina.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Februari, 2018

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad