HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Sunday, 25 February 2018

Makamu Mwenyekiti wa UWT afanya ziara katika Mkoa wa Magharibi Unguja.

Na Is-Haka Omar, Zanzibar.
VIONGOZI na watendaji wa Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi(UWT) Tanzania wameshauriwa kuendeleza utamaduni wa kuwatembelea wananchi ili kuibua kero zinazowakabili na kuzifanyia kazi kwa mujibu wa matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya  mwaka 2015/2020.

Pia wametakiwa kuzitendea haki dhamana za uongozi walizonazo katika medali za kisiasa kwa kuhakikisha CCM inazidi kuwa Chama bora na imara chenye sera , taratibu na misingi ya maadili yanayokidhi matakwa ya wananchi wote bila ya ubaguzi wa kidini na kikabila.

Ushauri huo umetolewa kwa wakati tofauti na Waasisi na viongozi wa zamani wa UWT katika mwendelezo wa ziara ya Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa Ndugu Thuwayba Kisasi, katika Mkoa wa Magharibi Unguja.

Akizungumza mwasisi wa UWT aliyewahi kushika nyadhifa mbali mbali ndani Umoja huo na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa CCM Taifa Bi.Mariam Hengwa (75) hapo nyumbani kwake kwa Mchina mwisho, amesema Chama Cha Mapinduzi kipo ngazi za chini kwa wananchi hivyo viongozi hao wapange utaratibu wa kuwatembelea wananchi mara kwa mara.

Bi. Mariam amesema viongozi wa UWT wanatakiwa kubuni mipango mbali mbali ya kimaendeleo itakayoongeza Ari na utendaji kwa Akina Mama wa Umoja huo, na kuwavutia wanawake wa upinzani kujiunga na CCM.

Hata hivyo amewakumbusha kuwa ni lazima viongozi hao wawe na mbinu mpya za kuwasimamia watendaji kwa lengo la kuondokana na mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea.

Kwa upande wake mwanasiasa mkongwe visiwani Zanzibar na muasisi wa UWT Bi. Rufea Juma Mbarouk (73), amesema njia ya pekee ya kurejesha hadhi na heshima ya UWT ni Akina mama hao kuacha tabia za fitna, majungu na kauli za kuchafuana kisiasa  badala yake washikamane na kulinda maslahi ya  Chama.

Bi.Rufea aliyewahi kushika nyadhifa ndani ya SMZ na Chama Cha Mapinduzi, amesema enzi za uongozi wake wanawake walikuwa kitu kimoja wakipendana na kushirikiana kwa kila jambo, ndio maana taasisi hiyo ilivuka vikwazo na changamoto za kisiasa na imebaki salama na  kuwa na heshima kitaifa na kimataifa.

“ Viongozi, watendaji na wanachama wote wa UWT  acheni tabia na ubinafsi usiokuwa na faida kwa Chama na Umoja wetu, fanyeni kazi kwa bidii na mtambue kuwa CCM inakutegemeeni sana”, aliwasihi viongozi hao Bi. Rufea.

Naye Bi.Salama Majaliwa ambaye ni miongoni mwa waasisi wa Umoja huo, alisema UWT imekuwa taasisi yenye nguvu toka enzi za Afro-Shiraz Party(ASP), ambapo Akina mama walikuwa mstari wa mbele katika kupigania demokrasia ndani na nje ya CCM.

Bi.Salama ameeleza kwamba licha ya kuwepo na mabadiliko ya mfumo wa kisiasa ni lazima viongozi wa UWT waliopo hivi sasa madarakani wasome alama za nyakati na kufanya siasa zinazoendana na mahitaji ya wananchi.

Pamoja na hayo muasisi huyo amesisitiza suala la mshikamano kwa UWT huku akiwakumbusha jukumu la msingi la Chama Chochote cha kisiasa ni kushinda kwa kila uchaguzi na ibara ya tano(5) ya Katiba ya CCM inaelekeza suala hilo, hivyo ni jukumu la Umoja huo kuhakikisha Chama Cha Mapinduzi kinashinda na kuendelea kuongoza dola mwaka 2020.

Akitoa tathimini ya ziara hiyo Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa Ndugu Thuwayba Kisasi, ameahidi kuzifanyia kazi kwa vitendo nasaha, maelekezo na ushauri uliotolewa na viongozi hao wa zamani ili kujenga Jumuiya na Chama yenye nguvu kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Amesema lengo la ziara hiyo ni kuwatembelea na kuwakagua waasisi wa Chama, Serikali na Jumuiya kwa kujifunza mambo mengi ya kiuongozi na kiutendaji kutoka kwao.

Pia ameeleza kuwa miongoni mwa tunu ya kujivunia kutoka kwa viongozi hao ambao ni Akina mama ni kupigania Demokrasia na misingi ya usawa ndani ya CCM, iliyowawezesha wanawake kusimama wenyewe na kupata nafasi za uongozi katika Chama na Serikali.

Mapema akizungumza Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UWT Zanzibar Ndugu Tunu Kondo, amesema Umoja huo unathamini na kuwaenzi wastaafu mbali mbali kwani nguvu na maarifa yao ndio matunda yanayowanufaisha wanachama na wananchi kwa ujumla.
 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Kisasi (kushoto) akisikiliza kwa makini nasaha za muasisi wa UWT Bi. Salama Majaliwa alipotembelewa nyumbani kwake Mwera na uongozi wa Umoja huo. 
 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Kisasi (kushoto) akimkabidhi  muasisi wa UWT Bi. Salama Majaliwa alipotembelewa nyumbani kwake Mwera na uongozi wa Umoja huo.

 VIONGOZI mbali mbali wa UWT wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Taifa, Thuwayba Kisasi wakiwa nyumbani kwa muasisi wa UWT Bi. Salama Majaliwa wakibadilishana mawazo.
 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Kisasi (kushoto) akisikiliza kwa makini nasaha za muasisi wa UWT, Bi. Mariam Hengwa(aliyekuwa katikati akizungumza) alipotembelewa na UWT yumbani kwake Kwa mchina-Mombasa Unguja.
 MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Kisasi (kulia) akisikiliza kwa makini nasaha za muasisi wa UWT, Bi. Rufea Juma Mbarouk(kushoto) alipotembelewa na UWT nyumbani kwake Mbweni Unguja.
MAKAMU Mwenyekiti wa UWT Taifa, Thuwayba Kisasi (kulia) akimkabidhi zawadi muasisi wa UWT, Bi. Rufea Juma Mbarouk(kushoto) alipotembelewa na UWT nyumbani kwake Mbweni Unguja.


No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad