HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, February 15, 2018

Maisha Magic Bongo kufadhili Harusi ya aina yake, Ni ya washindi wa shindano la ‘Harusi ya Ndoto Yako'

Wakazi wawili wa jiji la Dar es Salaam ambao ni wachumba Solomon Mwaigwisa na Magreth Richard wameibuka washindi wa shindano la Harusi ya Ndoto Yako lililokuwa likiendeshwa na chaneli ya Maisha Magic Bongo Dstv chaneli 160.

Wapenzi hao wameshinda zawadi ya ufadhili wa harusi yao ya kifahari itakayofanyika jijini Dar Es Salaam mwishoni mwa mwezi April mwaka huu.  Pamoja na kushinda Harusi ya Ndoto Yao, wawili hawa pia watapewa zawadi ya fungate kwa hisani ya hoteli ya kitalii ya Voyager Beach iliyopo jijini Mombasa nchini Kenya.

Washindi hao walitangazwa jana katika kilele cha siku ya wapendanao katika hafla iliyofanyika makao makuu ya MultiChoice Tanzania jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na washindi hao.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania Maharage Chande amesema channel ya Maisha Magic Bongo imeamua kuwatunuku watazamaji wake zawadi hiyo kupitia kipindi chake maarufu cha Harusi Yetu kinachorushwa na channel hiyo ambacho huonyesha harusi mbalimbali


Kipindi cha Harusi Yetu kilianza kuruka mnamo Novemba 2016 ambapo msimu wa pili wa kipindi hicho ulianza mwezi Julai mwaka 2017. Kipindi hicho hurusha harusi mbamlimbali huku kikiangazia walikotoka wanandoa, hatua wanazopitia katika mahusiano yao na hatimaye tukio la kufunga ndoa.

Kuanzia ilipoanza awamu ya pili Maisha Magic Bongo ilianzisha shindano maalum lililojulikana kama Harusi ya Ndoto Yako ambapo washiriki walikuwa wakijibu kuhusiana na kipindi cha harusi yetu ambapo kila wiki kulikuwa na swali moja. Hadi kufikia mwisho wa shindano mnamo mwezi Desemba mwaka jana jumla ya washiriki 1,112 walishiriki ambapo 448 waliingia kwenye mchujo wa wawali na hatimaye kubakia wanne ambao waliitwa kwenye usaili maalum uliokuwa na jopo la watahini saba.

Baada ya usaili huu, Solomon mkazi wa Dar es Salaam pamoja na mchumba wake Magreth waliibuka washindi na hivyo kupata zawadi ya kugharimiwa harusi yao itakayofanyika jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 28 mwezi April mwaka huu.

Akifafanua kuhusu zawadi hiyo, Maharage alisema zawadi hiyo inamaanisha maharusi hao watarajiwa watagharimiwa kila kitu kuanzia ukumbi, mavazi, chakula, vinywaji, burudani, pamoja na fungate la kukata na shoka katika moja ya hoteli za kitalii Voyager Beach Hotel katika ufukwe wa Mombasa nchini Kenya.
Wakizungumza katika hafla hiyo, Solomon pamoja na mchumba wake Magreth wamesema wamefurahi sana kushinda na kutuzwa ufadhili wa harusi yao. “Sote tunafahamu ni jinsi gani zoezi la harusi linavyokuwa na patashika hususan kwenye suala la gharama. 
Hivyo nafurahi sana na ninamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kushinda katika shindano la Harusi ya Ndoto Yangu kwani sasa sisi kazi yetu ni kufikiria tu jinsi tutakavyoendesha maisha yetu kwani suala la harusi limekamilika” alisema Solomon, Bwana Harusi mtarajiwa.

Ameipongeza Chaneli ya Maisha Magic Bongo kwa kubuni shindano hilo ambalo lilileta msisimko mkubwa na kwamba anaamini kuwa channel hiyo itaendelea kuimarika kwani kwa sasa imekuwa maarufu sana kwa kuwa ni chaneli inayowafanya watanzania wajivunie vipaji vyao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad