HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 16 February 2018

DK. KALEMANI AAGIZA MKANDARASI KUMALIZA HARAKA MRADI WA UMEME WILAYANI KISHAPU

Na Robert Hokororo, Ofisi ya Mkurugenzi
Waziri wa Nishati, Mh. Dk. Medard Kalemani Februari 15 mwaka amefanya ziara wilayani Kishapu ambapo amezindua ujenzi wa miradi ya kusambaza umeme vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Akiwa kwenye vijiji vya Negezi na Mwamashele, Dk. Kalemani alimuagiza mkandarasi anajenga mradi huo kukamilisha kwa wakati na kuviunganisha vitongoji vyote kwa umeme bila kuruka nyumba.
Alimuagiza kufikia Aprili mwaka huu kazi ya kusambaza nishati hiyo iwe imekamilika ili wananchi wanufaike na huduma hiyo na hivyo kuweza kuutumia kwa shughuli za maendeleo.
“Mkandarasi ongeza kasi hakuna kulala kumaliza mradi huu hatutaki wananchi wakwame na tunahakikisha vijiji vyote 118 vinapata huduma ya umeme, nakuagiza ndani ya siku 40 hapa Mwamashele umeme uwe umewaka,” alisema.
Dk. Kalemani aliwataka wananchi hao kuutumia umeme huo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi zikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo ili kujipatia kipato.
Pia aliwahimiza kuwa tayari kupokea nishati hiyo katika nyumba zao kwa kutandaza nyaya na kuwataka kuitunza miundombinu inayosambaza umeme ikiwemo, nguzo, nyaya na transifoma ili isaidie kutokatika kwa huduma hiyo.
Mbali ya kutoa pongezi kwa Shirika la Umema Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Shinyanga kwa kazi nzuri, pia aliliagiza kujenga vituo vya huduma katika maeneo ya vijijini ili kusogeza huduma kwa wananchi badala ya kufika wilayani kuhudumiwa.
Pia aliagiza kuwa mchakato wa kuunganishiwa umeme usizidi siku saba na pia vipaumbele viwe kwa taasisi za Serikali na kuagiza Halmashauri ya Kishapu kutenga bajeti kwa ajili ya kutandaza nyaya.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mh. Boniphace Butondo alimpongeza waziri kwa kuchapa kazi na kutaka wananchi waendelee kumpa ushirikiano mbunge wa jimbo hilo, Mh. Suleiman Nchambi.
Aliupongeza mradi huo na kusema kuwa umewatendea haki wananchi hususana vijana wanajishughulisha na shughuli zinazotumia umeme ambao wamelazimika kutumia majenereta na sola.
Butondo alisema kuwa mradi wa REA utakuwa umerahisisha shughuli za maendeleo ambapo pia aliomba kata zingine sita zaidi zifikiwe na umeme ili ziweze kuinua uchumi wake.

 Waziri wa Nishati, Mh. Dk. Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Negezi ambako aliwasha umeme katika taasisi ya Serikali ambako tayari mradi huo ulijengwa awamu iliyopita. 
 Mbunge wa Kishapu, Seleman Nchambi akizungumza katika mkutano wa hadhara wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati kijiji cha Negezi. 
 Sehemu ya wananchi wakifuatilia matukio kwenye shughuli hiyo.
 Sehemu ya nguzo zikiwa tayari zimewasili kijiji cha Negezi kwa ajili ya kuanza kusimikwa wakati wa ujenzi wa mradi huo vijiji mbalimbali.
Viongozi wa dini wakifuatilia matukio katika uzinduzi huo kijiji cha Mwamashele.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad