Benki ya CRDB kwa kushirikiana MasterCard
International leo wamezindua rasmi kadi mbili zenye mfumo wa “Credit-Card” zijulikanazo
kama “TemboCard World Rewards na TemboCard Gold Credit-Card, katika hafla
iliyofanyika Makao makuu ya Benki hiyo.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Dkt. Charles
Kimei alisema kadi hizo zenye mfumo wa “Credit-Card” ni za kwanza kuingizwa sokoni na
Benki ya CRDB. “Credit-Card ni mfumo maalum wa kadi za kibenki ambapo mteja anaweza
kutumia kadi yake kufanya manunuzi au malipo kwa kiwango cha fedha zaidi ya zile
alizonazo kwenye akaunti yake” alisema Dkt. Kimei.
Akizungumzia juu ya faida ya kadi hizo Dkt. Kimei alisema zinamuongezea mteja uwezo wa
kufanya manunuzi pasipo kuwa na wasiwasi wakutokuwa na fedha za kutosha katika
akaunti yake. “Kadi hizi zitamuwezesha mteja kupata mkopo wa muda mfupi na hivyo
kumuwezesha kutimiza malengo yake” alisema Dkt. Kimei
Dkt. Kimei alisema TemboCard World Rewards ni maalum kwa ajili ya wateja wakubwa,
ambapo mteja atapata mkopo wa hadi shilingi milioni 50, huku muda wa kurudisha mkopo
ukifika hadi siku 50. TemboCard Gold Credit Card yenyewe ni maalum kwa ajili ya wateja
wa kati na wajasiriamali, ambapo mkopo wao unaenda hadi shilingi milioni 20, na muda wa
kurudisha mkopo ukiwa ni siku 45.
“Mbali ya kuwa kadi hizi zinawapa wateja wigo mpana wakufanya manunuzi, wateja pia
watakuwa wakinufaika na punguzo la bei katika maduka, hoteli, migahawa na sehemu
mbalimbali duniani endapo watafanya malipo kupitia kadi zao, bima ya safari na bidhaa
watakazonunua kupitia kadi zao pamoja na fursa ya kutumia zaidi ya kumbi za VIP katika
viwanja mbalimbali vya ndege duniani kote” alisema Dkt. Kimei.
Akizungumzia namna ambavyo kadi hizo zitakwenda kusaidia kukuza uchumi wa nchi Dkt.
Kimei alisema Credit card zinawezesha watu kufanya malipo ya manunuzi ambayo pengine
wasingeweza kumudu kwa wakati huo hivyo kupelekea biashara kuzalisha mapato ambayo
kiuhalisia wasingeweza kuyapata, jambo ambalo hupelekea kukua kwa mzunguuko wa
fedha na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.
Dkt. Kimei alihitimisha hafla hiyo kwa kuwakaribisha wateja wa Benki ya CRDB na
watanzania kwa ujumla kutembelea matawi yaliypo karibu yao ilikujaza fomu za maombi ya
kupata kadi hizo za “TemboCard World Rewards na TemboCard Gold Credit-Card. “Fomu
za maombi pia zinapatikana kupitia website ya Benki, tunawakaribisha hata wale ambao sio
wateja bado, tutawafungulia akaunti na kuwapa kadi hizi”, alisema Dkt. Kimei.
Benki ya CRDB ndio Benki ya kwanza kuingiza sokoni kadi yake ya malipo iliyopewa jina la
“TemboCard” ambayo kwa kiasi kikubwa imesaidia kuwapa wateja wa Benki hiyo uhuru wa
kupata huduma kwa muda na mahali wanapotaka. Tokea ilipoingia sokoni TemboCard
imepata umaarufu mkubwa hasa baada ya kuungana na makampuni makubwa yanayotoa
huduma za kadi ya Visa, MasterCard na China Union na hivyo kuunda TemboCardVisa,
TemboCard MasterCard na hivi karibuni TemboCard China Union Pay.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei (katikati) akizungumza wakati wa uzinduzi wa kadi mpya (TemboCard Word Rewards na TemboCard Gold Credit) uliofanyika makao makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam, Februari 21, 2018. Kushoto ni Mkurugenzi wa Huduma Mbadala wa Benki ya CRDB, Philip Alfred na kulia ni Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Tully Mwambapa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB akionyesha kadi mpya za TemboCard World Reward na Tcembocard Gold Credit zilizozinduliwa leo hii (February 21, 2018) makao makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment