HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, January 8, 2018

WAZIRI MKUU MHE. KASSIM MAJALIWA KATIKA ZIARA YA MKOA WA RUVUMA

AWAONYA DC NA DED NYASA
*Asema waache kuwavuruga watumishi, madiwani

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaonya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Bi. Isabella Chilumba na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Oscar Mbyuzi waache malumbano ambayo yanawavuruga watendaji walio chini yao.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Januari 6, 2018) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa kwenye kikao kilichofanyika hoteli ya Mt. Vicent, mjini Mbamba Bay, wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

Amesema katika ziara zake zote za mikoani, amekuwa akipata malalamiko mengi kwenye Halmashauri na mabaraza ya madiwani lakini katika wilaya ya Nyasa amekuta hali ni shwari  isipokuwa kuna migogoro midogo kwenye uongozi wa juu.

“Tatizo ni dogo huku juu, bado mnavurugana Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi. Ninyi ni viongozi wa juu, acheni kuvurugana, fanyeni kazi. Mkigombana wanaoumia ni wananchi,” alisema.

“Mkuu wa Wilaya anaweza kuingia kwenye kikao chochote cha Halmashauri na kudai apewe taarifa, mpeni. Yeye siyo mjumbe wa kikao hicho lakini anayo mamlaka ya kushiriki.”

“Mkurugenzi wewe ni mtendaji mkuu, tumekukabidhi watumishi uwaongoze. Tumekukabidhi fedha kwa ajili ya maendeleo ya wilaya hii. Mtu akizitamani, mwambie hizi fedha zina maelekezo rasmi, hazipaswi kwenda kokote,” alisisitiza.

Aliwataka madiwani wasijenge tabia ya kuongeza siku za vikao kwa makusudi ili tu wapate posho za ziada. “Msitengeneze siku za ziada na kumpa presha Mkurugenzi. Kama kikao ni cha siku moja, basi kiishe. Siyo kulaza ajenda ili mmalizie kesho yake. Mkurugenzi akiwanyima fedha, msianze kugombana naye kwa sababu yeye hana fedha za kumgawia mtu,” alisisitiza.
AWEKA JIWE LA MSINGI KITUO CHA KUPOZEA UMEME NJIA YA MAKAMBAKO - SONGEA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea na kuahidi kuwa Serikali itaendelelea kuwasambazia umeme wananchi wote.

Ametoa ahadi hiyo leo (Jumapili, Januari 7, 2018) wakati Akizungumza na wananchi wa eneo la Unangwa nje kidogo ya mji wa Songea, mara bada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.

Waziri Mkuu amesema ujenzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Joseph Magufuli ya kuwataka Watanzania wapate umeme kwa urahisi. “Mheshimiwa Rais ameshusha gharama za umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000. Zamani ulikuwa unalipia fomu za kuomba umeme, sasa hivi nazo amesema zitolewe bure. Nguzo za umeme zilikuwa zinatozwa sh. 150,000, sasa hivi amesema zitolewe bure,” alisema.

Waziri Mkuu amesema zamani mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma, Songwe, Mtwara na Lindi ilikuwa na matatizo sufu ya kupata umeme lakini hivi sasa mikoa ya Mbeya na Iringa imepata suluhisho baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa kilovoti 400 wa kutoka Iringa hadi Shinyanga.

“Sasa hivi tunaingia Njombe na Ruvuma na baadaye tutaenda Mtwara na Lindi,” alisema.

Alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wanaoishi jirani na mahali kituo hicho kinapojengwa, wawe walinzi wakuu wa mali za mkandarasi ili mradi huo uweze kukamilika mapema. “Eneo hili lina saruji, nyanya na nondo, si vema watu wachache wjiokeze na kuiba vifaa vya ujenzi. Saidieni kulinda eneo hili, na mali za mkandarasi ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisisitiza.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka alisema mradi huo utakapokamilika utaunganisha vijiji 120 na wateja 22,700.


Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za TANESCO mjini Songea ambalo litagharimu sh. bilioni 2.27. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2018.

Akimkaribisha kuzungumza na watumishi wa TANESCO na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri wa Madini, Dk. Medard Kalemani alisema jengo hilo ni moja ya majengo makubwa saba nchini ambayo yatakuwa makao makuu ya kimkoa ya TANESCO.

Majengo mengine yatajengwa kwenye mikoa ya Singida, Kilimanjaro, Mtwara, Njombe, Pwani, Geita na Kigoma. “Kukamilika kwa ofisi hizi haimaanishi wafanyakazi wakae ofisini na kufaidi viyoyozi. Ni lazima waende nje kuwafuata wateja,” alisisitiza.

Dk. Kalemani alisema chini ya mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea, Serikali imeamua kujenga vituo vya kupozea umeme huko Makambako, Madaba na Songea ambavyo vitakamilika Agosti 30, 2018.

“Kukamilika kwa mradi huo kutaiepusha TANESCO na mzigo mkubwa wa kutumia fedha nyingi kununua mafuta mazito ambao pia utapunguza gharama za umeme kwa watumiaji. Kabla ya hapa, TANESCO ilikuwa inatumia sh. milioni 900 kwa siku kugharimia mafuta hayo,” alisema.

Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Kaimu MKurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka alisema ujenzi wa jengo hilo ambao umefikia asilimia 78, unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 31, mwaka huu.

“Gharama za ujenzi kwa jengo zima ni sh. bilioni 2.198 na gharama za mshauri ni sh. milioni 78 na gharama zote zinafikia sh. bilioni 2.276. Fedha hizi zimetolewa na Serikali,” alisema.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Nyasa, katika Hoteli ya Mt. Vicent iliyopo Mbambabay, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongea na Madiwani na Watumishi wa Halmashauri ya Nyasa, katika Hoteli ya Mt. Vicent iliyopo Mbambabay, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Nyasa, eneo la Kilosa Bambabay katika Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikata utepe wakati akifungua Bwalo la Chakula katika Shule ya Sekondari Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiangalia ngoma ya mganda,katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, Januari 6, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi, kutoka kwa Bibi Cecilia Manyai, katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, akiwa ni Mgeni rasmi katika Tamasha hilo, Januari 6, 2018. 
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi, kutoka kwa Mzee Gidion Ndembeka, katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, akiwa ni Mgeni rasmi katika Tamasha hilo
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya ungo, kutoka kwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, katika Tamasha la utalii lililofanyika Bambabay, Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma, akiwa ni Mgeni rasmi katika Tamasha hilo, Januari 6, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad