HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, January 18, 2018

KWANDIKWA AAGIZA DARAJA LA RUHUHU KUKAMILIKA

 Mhandisi Mkazi anayesimamia ujenzi wa Daraja la Ruhuhu, Mhandisi Napegwa Kiseko, akitoa maelezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, kuhusu maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo linalounganisha Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe na wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma wakati alipofanya ziara ya ukaguzi wa daraja hilo kwa upande wa  mkoa wa Ruvuma.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Lazeck Alinanuswe (katikati), akitoa taarifa ya mradi wa ujenzi wa Daraja la Ruhuhu lililopo wilayani Nyasa, mkoani humo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, wakati alipokagua  daraja hilo kuona maendeleo ya ujenzi wake.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoa wa Ruvuma, Mhandisi Lazeck Alinanuswe (katikati), wakati alipokagua ujenzi wa Daraja la Ruhuhu linalojengwa wilayani Nyasa na mkandarasi wa kampuni ya Lukolo kwa gharama ya shilingi bilioni 6.
Muonekano wa Daraja la Ruhuhu linalojengwa wilayani Nyasa na mkandarasi wa kampuni ya Lukolo kwa gharama ya shilingi bilioni 6. Daraja hilo litaunganisha Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kukifanyia ukarabati kivuko cha MV Ruhuhu kinachotoa huduma kati ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe ili kiweze kutoa huduma kipindi chote wakati ujenzi wa Daraja la Ruhuhu ukiendelea.
Muonekano wa Kivuko cha MV. Ruhuhu kinachotoa huduma kati ya wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma na Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe. Kivuko hicho kina uwezo wa kubeba magari 6 na watu 100.
Muonekano wa barabara ya Kitai-Lituhi yenye urefu wa KM 89 inayojengwa kwa kiwango cha changarawe mkoani Ruvuma.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, amemtaka mkandarasi anayejenga daraja la Ruhuhu wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha  anamaliza daraja hilo kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Agizo hilo amelitoa leo Wilayani Nyasa, mkoani Ruvuma alipokuwa akikagua ujenzi wa daraja hilo  ambapo ameusisitiza Uongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Makao makuu kuhakikisha kuwa utaratibu wa zoezi zima la ununuzi wa vyuma vitakavyowekwa juu ya daraja hilo linaenda sambamba na makadirio ya muda wa mradi ili kupelekea kazi hiyo kukamilika kwa muda uliopangwa.
"Nafikiri sasa jipangeni vizuri ili masika yakiiisha mhakikishe mnafanya kazi kwa bidii ya hali ya juu, nataka kufikia mwezi Juni daraja liwe limekamilika, pia TANROADS Makao makuu hakikisheni mchakato wa manunuzi ya vyuma vya daraja mnauanza mapema ili kuweza kukamilika mapema, msisubiri hadi daraja hili kukamilika", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Ameongeza kuwa daraja hilo likikamilika litakuwa ni kiungo kwa watu wa Nyasa mkoani Ruvuma na Ludewa mkoani Njombe kwani wamekuwa wakilisubiri daraja hilo kwa ajili ya kujiendeleza katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Aidha, amemwagiza Meneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), mkoani humo, Mhandisi Elisha Mgira, kuhakikisha anarekebisha kasoro zilizopo kwenye kivuko cha Ruhuhu ili kuweza kufanya kazi katika kipindi hiki ambacho wananchi wanasubiri ujenzi wa daraja kukamilika.
Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa daraja hilo, Mhandisi Napegwa Kiseko, amesema kuwa Ujenzi wa mradi huo umefika asilimia 50 ambapo kazi zinazofanyika sasa ni kujaza matabaka ya barabara zinazoingia darajani hapo ili kunyanyua tuta la barabara.
Amefafanua kuwa kazi hiyo inaendelea pande zote mbili yaani mkoa wa Ruvuma na Njombe ingawa kwa kipindi hiki cha  mvua kazi hiyo imekuwa na vikwazo vingi.
"Ujenzi wa misingi ya daraja kwa upande wa mkoa wa Ruvuma upo kwenye hatua za mwisho na kwa upande wa Njombe ujenzi wa misingi ulianza mwishoni mwa mwezi Disemba na unaendelea", amesisitiza Mhandisi Kiseko.
Mradi wa ujenzi wa daraja la mto Ruhuhu ambao upo mpakani mwa mkoa wa Ruvuma na Njombe unatarajiwa kugharimu takribani kiasi cha shilingi Bilioni 6 ambazo ni fedha za Serikali kwa asilimia mia moja na unatarajiwa kukamilka mwezi Juni mwaka huu.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad