HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, December 17, 2017

WANAFUNZI 7 MBINGA WAPIGWA MIMBA

Na Mwandishi wetu, Mbinga
WANAFUNZI 7 wa kike wanaosoma katika shule ya Sekondari Kiamili iliyopo kwenye kata ya Kigonsera Wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma, wamekatisha masomo yao katika kipindi cha mwaka huu kutokana na kuwa wajawazito.

Imeelezwa kuwa wanafunzi hao kidato cha kwanza yupo mmoja, cha tatu mmoja na kidato cha nne walikuwa wa nne ambao ilibidi wahitimu masomo yao baada ya kufanya mtihani wao wa mwisho.


Changamoto hiyo inasababishwa na shule hiyo kukosa mabweni ya kulala wanafunzi, kutokana na watoto wengi hutembea umbali mrefu kutoka majumbani kwao pale wanapokwenda shuleni kuhudhuria vipindi vya masomo.


Hayo yalisemwa na Mkuu wa shule hiyo, Frank Kinunda alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambao walitembelea shule hiyo kwa ajili ya kujionea maendeleo mbalimbali.


Kinunda alifafanua kuwa shule hiyo ambayo ina wanafunzi 800 wakiwemo wavulana 450 na wasichana 350 changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa vyumba vya kulala watoto hao ili waweze kukabiliana na tatizo hilo lisiweze kuendelea kutokea.


Shule hiyo ambayo ni ya kata ina bweni moja tu la kulala wanafunzi wa kike ambapo pia halitoshelezi mahitaji na kwamba halmashauri ya wilaya ya Mbinga, kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Kigonsera wamejenga bweni lingine moja la kulala watoto hao ili kuweza kukabiliana na hali hiyo.


Alibainisha kuwa wanafunzi wengine ambao ni wavulana wanaoishi mbali na shule wamekuwa wakati mwingine wakilazimika kuwalaza kwenye vyumba vya madarasa.


Kwa upande wake Kaimu Afisa mipango wa wilaya hiyo, Zainabu Mfinanga alisema kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo wamekuwa wakihamasisha wananchi kujitolea kujenga mabweni ya kulala wanafunzi katika shule mbalimbali za sekondari zilizopo wilayani humo na halmashauri imekuwa ikichangia vifaa vya kiwandani katika kuweza kukamilisha ujenzi husika.


“Wananchi wanapaswa kuendelea kujitolea, waandae benki tofari za kutosha ili ujenzi uweze kuwa rahisi na sisi kama halmashauri tuweze kuendelea kutoa vifaa vya kiwandani”, alisema Mfinanga.


Hata hivyo halmashauri ya wilaya ya Mbinga imeweza kuipatia shule ya sekondari Kiamili vifaa vya kiwandani ili kuweza kukamilisha ujenzi wa bweni linguine ambalo linajengwa sasa ikiwemo saruji mifuko 100, bati 220, nondo na gharama nyingine za kuweza kukamilisha ujenzi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad