HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Monday, December 11, 2017

Ukawa watishia kususia uchaguzi mdogo

Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimetaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuahirisha uchaguzi mdogo unaotarajiwa kufanyika Januari 13, 2018 vinginevyo havitashiriki.
Vyama hivyo ni Chadema, CUF, Chauma, NLD na NCCR-Mageuzi.
Akizungumza kwa niaba ya Ukawa leo Jumatatu Desemba 11,2017 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema vyama hivyo havitashiriki uchaguzi kwa sababu ya kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi mdogo wa udiwani wa kata 43 ulifanyika Novemba 26,2017.
Mbowe amesema uchaguzi huo uligeuka kuwa uwanja wa vita badala ya kuwa jukwaa la kuchagua viongozi.
"Ndiyo maana tunaiomba Serikali kuahirisha uchaguzi ili wadau wajadili kasoro zilizojitokeza," amesema.
Amesema majadiliano ya wadau yatasaidia kuondoa kasoro zilizojitokeza, hivyo kuwa na uchaguzi ulio huru na haki.
Mbowe amesema iwapo Serikali kupitia NEC itakataa kuahirisha uchaguzi wao hawatashiriki.
"Hatuwezi kushiriki uchaguzi wakati tumefungwa mikono, hii ni sawa na timu ya mpira kwenda kwenye mashindano bila kufanya mazoezi," amesema.
Mbowe amesema wakati vyama vya upinzani vikizuiwa kufanya mikutano ya hadhara, chama tawala kinafanya mikutano.

Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad