HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 14 November 2017

WAKULIMA WA KANDA YA ZIWA KUFIKIWA KUPITIA KONGANE

Na Mwandishi wetu,
Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imedhamiria na kujizatiti kuhakikisha inachangia kwa kiasi kikubwa katika  kuleta Mapinduzi yenye tija katika Sekta ya Kilimo kwa wakulima wa kanda ya ziwa na Tanzania kwa ujumla ili kusaidia upatikanaji wa fedha na sera nzuri zitakazosaidia maendeleo ya kilimo nchini.

Dhamira hiyo imewekwa wazi na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila wakati akitembelea miradi mbalimbali ya kilimo mkoani Mwanza hivi karibuni.

Bibi Kurwijila alisema kuwa katika kutekeleza mkakati wa kuwafikia wakulima wengi zaidi nchini Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imejipanga kutoa huduma kupitia kongane mpya nane (8) ili kuongeza tija kwa wakulima nchini.

“Kongane ni njia ya kimkakati ya kijiografia yenye kujikita katika shughuli za kilimo zinazohusiana, wasambazaji, na taasisi zinazohusishwa katika kujenga usawa wa moja kwa moja miongoni mwa wadau, hivyo ili kukidhi mahitaji ya wakulima nchini, benki ya kilimo itawafikia kupitia njia hii,” alisema.

Aliongeza kuwa kongane ya Kanda ya Ziwa ambayo inajumuisha mikoa ya Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Geita na Simiyu itatoa fursa ya ushindani kwa njia endelevu ili kuchagiza uhusiano na ushirikiano katika uongezaji wa thamani hasa katika makundi mbalimbali ya minyororo ya thamani, pamoja na taasisi na mamlaka za udhibiti zinazosaidia sekta ya kilimo nchini.

“Tunaamini kuwa kupitia mifumo thabiti ya kongane kwenye ongezeko la thamani Benki itawajengea uwezo wakulima katika kuboresha ujuzi katika mapatano na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma pia kuwapatia wakulima katika vikundi faida za kiuchumi kwa kuzingatia nguvu ya masoko ya mazao yao,” aliongeza.

Kwa mujibu wa mpango kazi wa Benki hiyo, dhana ya Kongane imeandaliwa kwa kutokana na mgawanyo wa kiokolojia kwenye kilimo kuzingatia kanda zilibainishwa kwenye Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Kilimo (ASDP II 2016/17-2020/21) ambapo mikoa imegawanywa ili kurahisisha utoaji wa huduma na mapendekezo ya teknolojia kwenye mifumo sawa ya uzalishaji. Kongane hizi zimezingatia utendaji wa kila mnyororo wa thamani ya kilimo na faida za linganifu katika kila mkoa katika uzalishaji.

Mpango kazi huo unaweka bayana kuwa matumizi ya Kongane yanalenga kuchagiza ufanisi katika kuimarisha minyororo ya thamani hasa wakati hakuna misingi thabiti katika kuendeleza minyororo hiyo ambayo inajumuisha kuanzia uzalishaji, usindikaji, usafiri, usambazaji, kuwezesha mazingira na soko. Hivyo uhitaji wa kuingilia kati juhudi hizi kutoka kwa wadau wengi ambao hawawezi kutatua suala lolote kwa pekee.

Akizungumzia mgawanyo wa mazao yatakayopata kipaumbele kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa Benki hiyo, Bw. Augustino Matutu Chacha alisema kuwa uteuzi wa minyororo ya thamani ya kipaumbele katika kila eneo umechukulia mchango wa mnyororo wa thamani katika usalama wa chakula, athari chanya kwa wakulima wadogo wadogo, mchango katika mikakati ya maendeleo ya kitaifa (hasa uendelezaji wa viwanda) - mpango wa maendeleo ya miaka mitano, soko la ndani na mauzo ya nje.
“Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa mazao ya kipaumbele ni Mihogo, Mpunga, Mikunde, Ng’ombe wa Nyama na Maziwa, Pamba, Miwa na Samaki,” alisema.
Bw. Chacha aliongeza kuwa Benki ya Kilimo inaamini kuwa kupitia Kongane wakulima wa watafikiwa kwa haraka kwa kuzingatia kuwa Tanzania ni nchi kubwa na yenye maeneo tofauti ya kimazingira/kilimo (Makundi) ambayo yana faida linganifu kwa ajili ya kuzalisha mazao maalum au seti ya bidhaa (mazao, mifugo, uvuvi).
TADB iliyozinduliwa rasmi mnamo tarehe 08 Agosti 2015 imeanzishwa kwa madhumuni makubwa mawili ya kusaidia utoshelezi na usalama wa chakula endelevu nchini Tanzania; na kuchagiza mapinduzi ya kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda cha kibiashara ili kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.
 Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Chobo, Bw. Charles Hotar (kulia) akitoa maelezo juu ya uchakataji wa nyama kwenye Kiwanda hicho kwa ugeni kutoka Benki ya Kilimo. Ugeni huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila (wapili kulia).
 Ugeni huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila (wapili kushoto) wakiangalia namna ng’ombe anavyoandaliwa mara baada ya kuchinjwa.
 Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Chobo, Bw. Charles Hotar (wapili kushoto) akionesha soseji zilizokuwa katika hatua za ufungaji. Wanaomuangalia ni wageni kutoka Benki ya Kilimo.
 Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TADB wakiangalia bidhaa mbalimbali zinazosindikwa na Kiwanda cha Chobo. Kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi Bw. Joseph Mutashubilwa (wapili kulia) na Bw. Dome Malosha (kulia).
 Mmiliki wa Kiwanda cha Chobo Investment, Bw. John Chobo  (mbele) akiwaonesha mahala maji taka yanapochujwa ili kulinda mazingira ya kiwanda. Wanaongalia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila (kulia) na Mkurugenzi wa Biashara na Mikopo wa Benki hiyo, Bw. Augustino Matutu Chacha (kushoto). Wapili kushoto ni Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Chobo, Bw. Charles Hotar.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo, Bibi Rosebud Kurwijila (kulia) akiangalia pembe ya ng’ombe kutoka Kiwanda cha Chobo. Kwa mujibu wa Meneja Uendeshaji wa Kiwanda cha Chobo, Bw. Charles Hotar (kushoto) pembe hizo uuzwa kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad