HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 17, 2017

TUNDU LISSU AFANYIWA UPASUAJI WA 18

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amefanyiwa upasuaji wa 18.
Upasuaji huo ulifanyika jana katika hospitali ya Nairobi nchini Kenya ambako Lissu anaendelea na matibabu tangu Septemba 7, baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 akiwa katika makazi yake, area D mjini Dodoma.
Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, kaka yake Lissu, Alute Mughwai alisema, “Lissu leo (jana) amefanyiwa upasuaji ambao ulianza asubuhi na umemalizika salama. Nimeambiwa muda mfupi uliopita (ilikuwa saa 9.32 alasiri wakati akizungumza na Mwananchi) kuwa ameshatoka chumba cha upasuaji.”
Alute alisema, “Nimeambiwa upasuaji ulikwenda vizuri na sasa atapaswa kupumzika kama siku nne kisha ataendelea na mazoezi kama kawaida.”
Ingawa Alute hakueleza huo ni upasuaji wa ngapi, Oktoba 17 mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza na waandishi wa habari alisema Lissu alikuwa amefanyiwa upasuaji mara 17 hivyo kama hakufanyiwa mwingine huo wa jana utakuwa ni wa 18.
“Lissu mpaka sasa amefanyiwa upasuaji mkubwa mara 17, ameongezewa damu nyingi kuliko mgonjwa yeyote aliyewahi kutibiwa hospitali hiyo ya Nairobi kwa miaka 20 iliyopita,” alisema Mbowe siku hiyo.
Alute alisema mpaka sasa bado hawajaanza mipango ya kushughulikia matibabu ya awamu ya tatu ambayo yalielezwa na Mbowe kuwa yatafanyikiwa nje ya Kenya.
“Nilisema nitazungumza na waandishi, lakini sijafanya hivyo kwani hakuna taarifa zaidi ya hizi na utaratibu wa matibabu ya awamu ya tatu bado hayajaanza ndio maana niko kimya,” alisema Alute.


Chanzo: Mwananchi

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad