HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, November 10, 2017

JAFO AZINDUA KAMPENI YA MKOA WETU VIWANDA VYETU

Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo akizindua Mwongozo wa Kampeni ya uanzishwaji wa Viwanda kwa kila Mkoa hapa nchini ili kuendana na dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano inayosisistiza ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo akisisitiza umuhimu wa Wakuu wa Mikoa Kusimamia Kampeni ya uanzishwaji wa viwanda 100 katika kila Mkoa wakati akizindua kamapeni hiyo leo Mjini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akieleza umuhimu wa Ujenzi wa Viwanda katika kuzalisha ajira kwa Vijana na kukuza uchumi wa nchi.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Seleman Jafo akionesha moja ya viatu vinavyozalishwa hapa nchini katika Viwanda vidogo na vya Kati wakati akikagua mabanda ya wajasiriamali wanaozalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo za ngozi mara baada ya kuzindua kampeni yenye kauli Mbiu ya “Mkoa Wetu Viwanda vyetu” ili kuhamasisha ujenzi wa Viwanda katika Mikoa yote nchini.
Waziri wa nchi ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya Wakuu wa Mikoa(kushoto), kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama walioshiriki katika Uzinduzi wa Kampeni ya ujenzi wa Viwanda vidogo na vya kati katika kila Mkoa. ( Picha zote na Frank Mvungi – Maelezo, Dodoma)

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO, DODOMA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI) Mhe. Seleman Jafo amezindua kampeni ya “Mkoa wetu, Viwanda vyetu” yenye lengo la kuanzisha viwanda 100 katika kila Mkoa nchini, leo Mjini Dodoma.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mhe. Jafo amesema kuwa ni jambo lililowazi kuwa ili nchi iweze kuendelea inahitaji kufanya mapinduzi makubwa katika viwanda.

“Historia ya Viwanda siyo ngeni katika nchi yetu, tangu tupate Uhuru mwaka 1961 Serikali imekuwa ikilenga katika kujenga Uchumi kupitia Viwanda ambapo tokea wakati huo viwanda vingi vidogo vya kati na vikubwa vilianzishwa na kusimamiwa huku sehemu kubwa ya viwanda hivyo vikisimamiwa na Serikali” ameeleza Mhe. Jafo.

Aidha amesema kuwa ili azma hiyo iweze kufikiwa TAMISEMI itashirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji katika kuweka mazingira wezeshi pamoja na kutoa mwongozo wa namna ya kushirikisha Tasisi za Serikali na Sekta Binafsi na wadau wa maendeleo katika kuanzisha, kuendesha na kusimamia Viwanda ili kuikuza sekta hiyo nchini.

“TAMISEMI kupitia Mikoa na Halmashauri imedhamiria kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Uchumi wa Viwanda, hivyo kila Mkoa uanishe Viwanda vya vipaumbele kwa kuzingatia Malighafi muhimu za Viwanda zinazopatikana kwenye maeneo yao pamoja na mahitaji muhimu ya soko” amefafanua Mhe. Jafo.

Hata hivyo, Mhe. Jafo amewataka Wakuu wa Mikoa, wakuu wa Wilaya na Halmashauri kuwatumia ipasavyo Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ugani ili kuwahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhandisi Stella Manyanya amesema kuwa Wizara yake itaendelea kuweka mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kuanza kujenga majengo maalumu kwa ajili ya uendelezaji viwanda katika Ofisi zote za SIDO Mikoani.

Naye Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa Kauli Mbiu ya Mkoa wetu viwanda vyetu itapunguza changamoto ya upatikanaji wa ajira kwa vijana nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad