HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Thursday, November 2, 2017

EU yatoa Euro Milioni 50 kuendeleza Umeme vijijini

 Katibu Mkuu wa  Wizara ya  Fedha na Mipango, Dotto James (kulia) na Kamishna wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU), Neven Mimica (kushoto)  wakisaini makubaliano ya msaada wa Euro Milioni 50 kwa ajili ya uboreshaji wa sekta ya nishati nchini.
 Kamishna Msaidizi anayeshughulikia Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Edward Ishengoma (kulia waliokaa mbele) pamoja na wajumbe wengine akifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa Katibu Mkuu wa  Wizara ya  Fedha na Mipango, Dotto James (hayupo pichani) katika mkutano huo.
Katibu Mkuu wa  Wizara ya  Fedha na Mipango, Dotto James ( wa pili kushoto waliosimama mbele) na Kamishna wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU), Neven Mimica ( wa tatu kushoto waliosimama mbele) wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe mara baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo.

Na Mwandishi wetu
Umoja wa Ulaya (EU) umetoa msaada wa   kiasi cha  Euro Milioni 50 ambazo ni sawa na takribani  shilingi  bilioni 130 za kitanzania  kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa Umeme  Vijijini inayotekelezwa na  Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Makubaliano ya msaada huo yalisainiwa jijini Dar es Salaam  tarehe 2 Novemba, 2017 kati ya  Umoja wa Ulaya (EU) ukiwakilishwa na Kamishna wa Maendeleo  wa Umoja huo, Neven Mimica na  Serikaliya Tanzania kupitia  Wizara ya  Fedha na Mipango  ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Dotto James. Katika mkutano huo, Wizara ya Nishati iliwakilishwa na  Kamishna Msaidizi  anayeshughulikia Nishati Jadidifu, Edward Ishengoma
Akizungumza kabla ya kusaini makubaliano hayo, Katibu Mkuu wa  Wizara ya  Fedha na Mipango, Dotto James alisema kuwa kiasi hicho cha  fedha ni sehemu ya awali ya kiasi cha Euro Milioni 180 zilizotolewa kwa ajili  ya kuboresha Sekta ya Nishati na kufafanua kuwa fedha hizo  zitatolewa katika Awamu mbalimbali.
Alisema kuwa kati ya Euro Milioni 180, Euro Milioni 90 zitatumika kwa ajili ya mpango wa kusambaza Umeme Vijijini kupitia  REA  na nyingine Euro Milioni 90 zitatumika kwa ajili ya kuboresha Sekta ya Nishati kupitia  Shirika la  Umeme Tanzania (TANESCO) na REA.
Aliendelea kusema kuwa msaada huo usio na masharti ni moja ya mikakati ya  Umoja wa Ulaya (EU) kuunga mkono juhudi za Serikaliya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli katika usambazaji wa Umeme Vijijini.
Katika hatua nyingine, James aliushukuru Umoja wa Ulaya (EU) kwa msaada huo na kusisitiza kuwa Serikaliitautumia  msaada huo katika kuhakikisha kuwa vijiji vyote Tanzania  vinapata Umeme ifikapo mwaka 2020.
Awali akielezea mafanikio ya REA, James alisema wakati REA inaanzishwa mwaka 2008 asilimia mbili tu  ya vijiji vyote vilikuwa vinapata Umeme lakini hadi kufikia  Desemba, 2016 ni asilimia 49.3 wananchi waishio vijijini wanapata Umeme.
Aliendelea kufafanua kuwa mwaka 2008 asilimia 10 ya wananchi kitaifa walikuwa wanapata Umeme (overall electricity access level) lakini hadi kufikia Desemba, 2016 ni asilimia 67.5 wanapata Umeme wa uhakika.
“Mafanikio haya ni makubwa na ninaamini kupitia msaada huu na ongezeko la kasi ya usambazaji wa Umeme vijijini, ifikapo mwaka 2020 vijiji  vyote nchini  Tanzania  vitakuwa na  Umeme wa uhakika na kupelekea kwenda kwenye uchumi wa Viwanda,” alisema James.
Wakati huo huo akizungumza kabla ya utiaji saini wa makubaliano hayo Kamishna wa Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU), Neven Mimica alisema kuwa  Umoja huo unatambua juhudi  zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara ya Nishati katika usambazaji wa Umeme vijijini hivyo wapo  tayari kuisaidia  Serikaliili iweze kutimiza malengo ya  Dira ya Maendeleo ya  Taifa yenye lengo la kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025.
Alisema kuwa Nishati ya Umeme ni muhimu husan katika maeneo  ya vijijini kwa kuwa inachangia uboreshaji wa huduma za jamii kama Shule, Vituo  vya Afya, Hospitali, Viwanda vidogo vidogo na Kilimo.
Aliendelea kusema kuwa, kupatikana kwa Umeme wa uhakika vijijini kutapelekea ongezeko la ajira kwa kuwa wananchi wataweza kujiajiri kwa kuanzisha  viwanda vidogo  vidogo vya kusindika mazao.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad