HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, November 7, 2017

AZAM FC WAACHANA NA MSHAMBULIAJI WAO WA KIMATAIFA YAHYA MOHAMED



Uongozi wa klabu ya Azam FC imeamua kuvunja mkataba na mshambulizi wake, Yahaya Mohammed raia wa Ghana baada ya kuona ameshindwa kuwapatia kile ambacho wanakihitaji kwa muda wote aliokuwa ametumikia kwenye klabu hiyo.

Mwishoni mwa wiki baada ya mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting , Kocha Mkuu wa Azam  Aristica Cioba aliweka wazi mkakati wake wa kutaka kupata washambuliaji  wengine wawili ili kuongeza nguvu ya kikosi chake.

Akitoa ufafauzi wa maamuzi hayo, Msemaji wa Azam Jaffary Idd Maganga alisema kuwa wamefikia uamuzi wa kuvunja mkataba na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 baada ya kuonesha kiwango duni tofauti na matarajio yao walipomchukua mwaka jana wakati wa dirisha Dogo la usajili.

"Nichukue nafasi hii kuwafahamisha kwamba hatutaendelea kuwa naye, uongozi umekutana naye, wamezungumza kuhusiana na suala lake na wamemalizana. Hivi sasa Mohamed sio mchezaji tena wa Azam  baada ya makubaliano kati yake na uongozi," alisema ..

Maganga amesema tayari wameshampatia release letter na pamoja na hayo tayari wameshampatia kila kitu ikiwemo tiketi ya ndege ambapo wanatarajia ataondoka kurudi kwao Ghana Jumanne hii.

"Tutamkumbuka Yahaya, kwa Maana kwamba yale ambayo ameyafanya kwenye timu yetu, ametusaidia kupata ubingwa wa Kombe la Mapinduzi na pia msimu ndiye aliyefunga bao la kwanza," alisema.

Mbadala wa Yahaya Mohamed kwa mujibu wa Afisa Habari Jaffary Maganga, ni kwamba atatangazwa baada ya benchi la ufundi kufanya tathmini na kuchambua wale wanaowahitaji.

Mshambuliaji huyo alijiunga na Azam akitokea Aduana Stars ya Ghana, ambayo aliisaidia kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Ghana msimu 2015/16, Mohammed pia aliiibuka mfungaji bora namba mbili wa ligi hiyo kwa mabao 15 aliyofunga nyuma ya Latif Blessing wa Liberty Proffesional aliyetupia 17.

Mohammed alikuwa moja ya wachezaji  kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Ghana kilichoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika mwaka juzi nchini Afrika Kusini na timu hiyo kuwa washindi wa pili.



No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad