HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Friday, October 13, 2017

TEWW YAJIDHATITI KUMKOMBOA MTOTO KIELIMU



 Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Watuwazima (TEWW), Dk. Fidelice Mafumiko, akizungumza wakati maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike katika ukumbi wa taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam, jana. Katikati ni Afisa Tarafa ya Kariakoo, Christina Kalekezi na kushoto ni Naibu Mkurugenzi Taaluma wa TEWW, Dkt. Kasim Nihuka.


Na Mwandishi Wetu
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima imejizatiti kutoa elimu bora kwa wasichana wanaoshindwa kuendelea na shule kutokana na changamoto mbalimbali kama vile  umbali mrefu, mimba za mashuleni, mazingira magumu kama vile uyatima na umasikini.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt.Dkt. Fidelice Mafumiko wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike yaliyoadhimishwa katika Taasisi hiyo mapema jana, Jijini Dar es Salaam.

“Wasichana hupatiwa stadi za ufundi, ujasiriamali, stadi za maisha kama malezi, kujitambua pamoja na stadi za msingi za masomo ya shule kama hisabati, Kiswahili na English ili kuwawezesha kuwasiliana katika mazingira tofauti hali itakayosaidia kukuza na kuchochea ustawi wa jamii yetu,” alisisitiza Dkt. Mafumiko.

Dkt. Mafumiko amesema kuwa mipango yakuwawezesha watoto wakike inajikita katika azma ya Serikali kuweka mfumo nyumbufu katika elimu na mafunzo ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kujielimisha na kuwa huru kutafuta elimu katika fani wanayopenda hadi kufikia upeo wowote kulingana na stahili na uwezo wao kwa kuzingatia sera ya Taifa ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014.

Aliongeza kuwa, Taasisi hiyo pia imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya sekondari kwa njia ya ujifunzaji huria, ukiwa ni mpango wa elimu unaotolewa sambamba na mfumo rasmi kwa ajili ya walengwa waliokosa fursa hiyo katika shule rasmi na hivyo kuwawezesha kujisomea kwa mfumo huria na masafa katika madarasa ya jioni au majumbani kwa kutumia vitabu na moduli zilizoandaliwa na TEWW.

 Mipango hiyo inahusisha mafunzo ya ujasiriamali, malezi ya familia na watoto, lishe bora, ufugaji na kilimo. Vilevile TEWW huandaa mipango yenye lengo la kutoa fursa za elimu kwa wasichana ambao wamekosa elimu katika mfumo rasmi.

Pia aliongeza kuwa walengwa huandaliwa programu maalum ya kuwawezesha kufanya mtihani wa maarifa (QT) na ule wa kidato cha nne sawa na wale walio katika shule rasmi za sekondari.

Kwa kupitia mpango huo wasichana wengi wameweza kupata fursa za kumalizia masomo waliyokatisha kutokana na changamto mbalimbali walizokuwa nazo.


Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) ilianzishwa mnamo mwaka 1975 na kupewa jukumu la kuandaa mipango ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi nchini. Mipango hiyo inalenga makundi mbalimbali ya watu katika jamii kuanzia vijana, wakulima, wafanyakazi na makundi maalum kama wanawake.

Ofisa Tarafa ya Kariakoo, Christina Kalekezi, akizungumza na wanafunzi wa wakike wakati wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike katika ukumbi wa taasisi hiyo, Dar es Salaam, jana  katikati ni Mkurugenzi wa TEWW, Dk. Fidelice Mafumiko. 
Wanafunzi wakiwa katika hafla ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani katika ukumbi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Dar es Salaam mapema jana.
TEWW Yajizatiti Kumkomboa Mtoto wa Kike Kielimu.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad