HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 17 October 2017

SIDO WATOE MAFUNZO KWA WANAFUNZI WA VYUO ILI WAJIAJIRI: RC NCHIMBI.

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitoa hundi ya Mkopo uliotolewa na SIDO kwa mjasiriamali Sarah Isaya kutoka Singida katika hafla fupi ya kukabidhi mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani hapa.
  Mkurugenzi Mtendaji SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji akitoa nasaha zake kwenye hafla ya utoaji wa hundi za mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali mkoani Singida uliofanyika kwenye viwanja vya SIDO mjini hapa. Wa kwanza kushoto (aliyekaa) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi.
  Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akitazama ubora wa mafuta ya alizeti  na kupata maelezo ya mafuta hayo yanayosindikwa katika viwanda vya Mkoa wa Singida kutoka kwa Mkurugenzi wa kampuni ya kuzalishaji  Mafuta ya alizeti  ya  Sunshiwe Oil Mill, Salum Khalifan.
 Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende akitoa taarifa ya Viwanda Vidogo vidogo na ujasiriamali Mkoa wa Singida kwenye hafla ya utoaji wa hundi za mikopo kwa wajasiriamali mbalimbali. Wa kwanza kushoto (waliokaa) ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Mkurugenzi Mtendaji SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amelitaka shirika la Viwanda Vidogo vidogo (SIDO) kuandaa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa vyuo mbali mbali mkoani hapa ili wakihitimu waweze kujiajiri

Dkt. Nchimbi ametoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mikopo ya SIDO kwa wajasiriamali iliyofanyika kwenye viwanja vya SIDO ambapo amesema mafunzo hayo yatawajengea mazingira mazuri wahitimu kujiajiri.

Amesema Mkoa wa Singida una fursa nyingi za kujiajiri pamoja na kuwa na vijana wengi hasa walipo katika vyuo mbalimbali lakini hawawekezi katika fursa hizo kwa kutokujua au kukosa elimu ya kutosha juu ya ujasiriamali, na hata waliopo vyuoni wakihitimu wanasubiri kuajiriwa badala ya kujiajiri.

Dkt. Nchimbi amesema ili wananchi wakiwemo vijana waweze kuzitambua fursa hizo, SIDO Mkoa na wadau wengine wanapaswa kuongeza juhudi zaidi katika utoaji mafunzo ya ujasiriamali ambapo amewataka wajielekeze kwenye vyuo mbalimbali.

“Singida ina kila aina ya fursa ambazo zinaweza kumkomboa mwananchi kiuchumi. Kwa hiyo hakuna sababu vijana au watu wengine kuukimbia mkoa wao na kwenda kutafuta maisha katika mikoa mingine. Ni suala la kujipanga na kupata fursa ya mafunzo kutoka SIDO mkoa”, amefafanua.

Aidha ameziagiza halmashauri zote na manispaa Mkoani hapa kutangaza fursa, bidhaa, mazao, na huduma zinazopatikana katika maeneo yao ili kuwasaidia wajasiriamali kupata soko la uhakika.

“ Halmashauri zote tumieni fedha mnazopata kwenye vyanzo vya mapato ya ndani muwasaidie wajasiriamali wenu kutangaza kwenye vyombo vya habari, nina imani na uhakika kuwa mkitangaza bidhaa na mazao yao yatapata soko na nyinyi halmashauri mtapata mapato yenu”, amesema Dk.Nchimbi.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa SIDO Taifa Mhandisi Profesa Sylvester Mpanduji amesema SIDO imekuwa tegemeo kubwa kwa wajasiriamali hasa katika kutoa mafunzo na kusaidia teknolojia ya kuongeza thamani ya mazao na malighafi.

“Mikopo ya SIDO imeweza kuwasaidia wajasiriamali kuthubutu na kuanzisha miradi ya usindikaji mara tu baada ya kupata mafunzo. Kundi hili limekuwa na changamoto ya mitaji kwa kuwa halikidhi na halijaweza kuthubutu kuzifikia benki kutokana na woga na gharama za mikopo”, amesema.

Mhandisi Profesa Mpanduji amesema kwa kipindi cha mwaka 2016/2017 SIDO imeweza kutoa mikopo 4,464 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7.2. Mikopo hiyo imetengeneza ajira 11,861 kati ya ajira hizo asilimia 51 ni wanawake.

Kwa upande wake Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida Shoma Kibende amesema kwa Mkoa wa Singida wametoa mikopo yenye jumla ya shilingi milioni 724.6 kwa wajasiriamali 693 na vikundi 47. Hali ya urejeshaji wa mikopo hiyo ni asilimia 98.

Kibende amesema SIDO wameweza kutoa mafunzo ya wajasiriamali mbalimbali 37 kwa wajasiriamali 996 ambao kati yao wanawake walikuwa 536 na wanaume 460.

Amesema baadhi ya changamoto zinazowakabili kuwa ni upungufu wa wafanyakazi na ukosefu wa fedha kwa ajili ya kutekeleza mipango waliyojiwekea ikiwemo kuendeleza na kuboresha mtaa wa viwanda.

Naye Mjasiriamali kutoka Kampuni ya Singida Super Quality Oil and Rice mills Simon Kitundu amezishauri halmashauri na manispaa kutenga maeneo maalum ya kufanyia biashara wajasiriamali waweze kuondokana na adha mbalimbali ikiwemo ya kuuza bidhaa zao kwenye madirisha ya mabasi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad