HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Thursday, 19 October 2017

SAROTA AWAASA WAJUMBE WA BARAZA LA WAFANYAKAZI WA STAMICO KUKUZA UBUNIFU

 Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico), Mhandisi John Nayopa akizungumza katika kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa Shirika hilo leo jijini Dar es Salaam.
Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Taifa la Madini (Stamico) wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Mhandisi John Nayopa leo jijini Dar es Salaam.
 Picha mbalimbali za wafanyakazi katika baraza la wafanyakazi.

KAMISHNA Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Madini Bw. Julius Sarota amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kukuza ubunifu katika kutekeleza majumu yao ili kuleta ustawi endelevu wa Shirika hilo na tija kwa Taifa.

Bw. Sarota ametoa rai hiyo leo, wakati akizungumza katika mkutano wa tatu wa Baraza la Wafanyazi wa STAMICO, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini; uliofanyika katika makao makuu ya Shirika hilo jijini Dar es Salaam.
Bw. Sarota amesema Baraza la Wafanyakazi mahala pa kazi ni chombo muhimu cha kukuza ustawi wa taasisi husika; hivyo ni wajibu wa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la STAMICO kuongeza ubunifu na kutekeleza miradi ya utafiti na uchimbaji madini; itakayoleta faida kwa STAMICO na kukuza uchumi wa Tanzania.

“ Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli amekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza azma ya Taifa ya kujenga Tanzania ya Viwanda, ambavyo vitahitaji madini kutumika kama mali ghafi. Nichukue fursa hii kusisitiza STAMICO mtekeleze miradi ya uchimbaji madini itakayosaidia kutoa mali ghafi kwa viwanda vinavyotarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.” Alisisitiza Bw. Sarota.

Amesema STAMICO inabidi iongeze mwendo katika utekelezaji wa miradi yake ya vipaumbele, ili kwenda sambamba na kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ya viwanda; hatimaye kumudu soko la mali ghafi za madini nchini kama vile phosphate na graphite, hatua ambayo itasaidia kuwazuia wenye viwanda kuhangaika kuagiza mali ghafi hizo kutoka nchi za nje.
Aidha Sarota amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi la STAMICO kumpa ushirikiano mkubwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika hilo Mhandisi John Nayopa, ili kwa pamoja kukuza uzalishaji katika miradi ya Shirika, uchangiaji wa uchumi wa nchi na ukuaji wa pato la Taifa.

Awali, akifungua rasmi mkutano huo Baraza la Wafanyakazi, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa STAMICO, Mhandisi John Nayopa, amesema atahakikisha kuwa utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Shirika wa mwaka 2017/18 hadi 2020/21 unakwenda sambamba na Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Mwaka 2016/17 – 2020/21; ambao umeweka kipaumbele kwenye maendeleo ya viwanda nchini.

Mhandisi Nayopa amewataka wajumbe wa Baraza hilo la Wafanyakazi kushiriki kikamilifu katika mjadala ya kupitia rasimu Sera ya Uwekezaji ya Shirika na ile ya Mpango Mkakati na kuziboresha rasimu hizo kikamilifu kwa kuzingatia vipaumbele vya sasa vya Shirika na mwelekeo wa sera za kiuchumi za Taifa. 

Rasimu hizo zimelenga kutoa mwelekeo mpya wa Shirika katika kutekeleza majukumu yake na kuleta tija na ustawi endelevu. 

Aidha, Mhandisi Nayopa pia amewataka wajumbe wa Baraza hilo la Wafanyakazi waisome na kuilewa bajeti ya Shirika ya mwaka 2017/2018 ili waweze kuismamia kikamilifu utekelezaji wake.

Nayopa pia ametoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa STAMICO na Watumishi wote, kuendelea kutimiza wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa wadau wa Shirika ili kuiwezesha STAMICO kufikia malengo yake kwa ufanisi mkubwa.

“Mamlaka za nidhamu zilizomo ndani ya STAMICO, ziendelee kulinda  nidhamu na taswira ya Shirika, kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wasiotimiza wajibu wao au wanaoidhalilisha Serikali kwa kuendekeza vitendo visivyostahili sehemu ya kazi, vikiwemo vitendo vya rushwa” Alisisitiza Mhandisi Nayopa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala wa STAMICO Bw. Deusdedith Magala, amewataka wajumbe wa Baraza hilo kufanya kazi kwa bidii na kasi, ili kwenda sambamba na mabadiliko yanayofanywa sasa na Serikali katika sekta hii ya madini; hatua ambayo itasaidia kuimarisha kiwango cha mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa pato la Taifa.
“Niwatake wajumbe wa Baraza hili muwe chachu ya kufikia mageuzi haya ambayo Serikali imeyakusudia kuyafanya ili kuongeza mapato yatokanayo na miradi ya uchimbaji madini nchini.” Alisisitiza Bw. Magala.

Mkutano huo wa tatu wa Baraza la Wafanyakazi wa STAMICO umeshirikisha wajumbe wa Baraza hilo kutoka STAMICO makao makuu na Dodoma; wawakilishi kutoka Wizara ya Madini na wawakilishi wa Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati, Ujenzi na Kazi nyinginezo yaani TAMICO mkoa wa Dar es Salaam na Ofisi ya TAMICO-Taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad