HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Tuesday, 31 October 2017

MWAMUZI ALITUNYIMA PENATI MBILI DHIDI YA YANGA- MANARA

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara akitoa lawama kwa mwamuzi Hery Sasii katika 

mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC uliomalizika kwa sare ya 1-1 Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.


KLABU ya Simbe imelalamika kunyimwa penalti mbili na refa Hery Sasii katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC uliomalizika kwa sare ya 1-1 Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.Akizungumza na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Hajji Sunday Manara amesema refa alikwenda na matokeo yake uwanjani. 

Manara aliwawekea Waandishi wa Habari video ya mchezo huo kuwaonyesha namna ambavyo refa Sasii hakutoa penalti licha ya mpira kuwagonga mikononi beki, Kevin Yondan na kiungo Mkongo, Papy Kabamba Tshishimbi Jumamosi.


Manara aliyewabeza watani wao hao wa jadi, kwamba ni kawaida yao kupendelewa na marefa kila wanapokutana na Simba amesema watapeleka malalamiko Bodi ya Ligi dhidi ya refa huyo na wengine walioionea timu yao katika mechi zilizotangulia.


Akasema huo ni mwendelezo wa matukio ya klabu yake kutotendewa haki na marefa katika mechi za Ligi Kuu msimu huu, akidai walinyimwa pia penalti mbili katika mechi dhidi ya Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, kabla ya wapinzani wao wengine, Singida United kupewa penalti ya utata Uwanja wa CCM Kambarage Shinyanga.

Simba ilitoa sare ya 2-2 na Mbao FC kabla ya kushinda 3-1 dhidi ya Stand United, katika mchezo ambao pia walikataliwa bao zuri la mshambuliaji wao, Laudit Mavugo.

Pamoja na hayo, Manara amelalamikia kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kukataa ombi la klabu, Simba na Yanga kutaka mchezo wao ufanyike Uwanja mkubwa wa Taifa na kuupeleka Uwanja mdogo wa Uhuru.


Manara amesema hali hiyo ilizikosesha klabu fedha kutokana na watazamaji kutojitokeza kwa wingi kwa kuhofia usalama wao kutokana na udogo wa Uwanja wa Uhuru. 


Aidha, Manara  amesema kwamba kikosi cha Simba sasa kinaelekeza nguvu zake katika mchezo wake ujao dhidi ya Mbeya City Jumapili Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na  kikosi kitaondoka  Ijumaa kwenda Mbeya na  kitakaa kwa muda mrefu kutokana na kukabiliwa na mechi nyingine pia za Ligi Kuu Nyanda za Juu Kusini. 

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad