HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 10, 2017

MBOWE AMSHANGAA ASKOFU PENGO KWA KUUPINGA MCHAKATO WA KATIBA MPYA

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo kuhusu mchakato wa Katiba imewasikitisha.

Wakati Mbowe akitoa kauli hiyo, mwenyekiti wa kamati ya kitaifa ya maadili, amani na haki za binadamu kwa jamii ya madhehebu ya dini zote Tanzania, Askofu William Mwamalanga amemshauri Rais John Magufuli kuufufua mchakato huo uliokwama.

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akizungumza jana baada ya kuombwa kutoa maoni yake kuhusu msimamo wa Kardinali Pengo kwamba Katiba siyo kipaumbele chake, bali huduma za jamii, Mbowe alisema Askofu huyo ni kiongozi wa dini anayepaswa kulinda heshima aliyonayo ndani na nje ya kanisa.

Katika taarifa yake ya kufafanua kauli iliyotolewa na Askofu wa Jimbo la Rulenge mkoani Kagera, Severine Niwemugizi baada ya kukaririwa akisema kwamba Katiba Mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi, Kardinali Pengo alisema hayo yalikuwa maoni yake binafsi siyo msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.

“Mtu akiniambia priority (kipaumbele) ya Tanzania ni Katiba Mpya inabidi anithibitishie huo ukipaumbele maana siwezi kuona mtoto anakufa kwa njaa au kwa kukosa dawa eti kwa sababu ya Katiba Mpya. Kwangu mimi Katiba ni kitu ambacho kije baadaye, si cha haraka.

“Wanasiasa wasiache watoto wetu wafe kwa njaa kisa malumbano ya Katiba. Wasiache watoto wakose shule kwa sababu hela zote zimeishia kwenye malumbano juu ya Katiba,” alisisitiza Kadinali Pengo.

Lakini jana akizungumzia msimamo huo, Mbowe alisema, “Askofu Pengo ni kiongozi wa kanisa, anaheshimika na wananchi ambao si wale anaowaongoza tu lakini kwa kauli yake kuhusu Katiba, imetushangaza na imenisikitisha,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Suala la elimu, chakula na maisha yetu yanalindwa na Katiba, ndiyo msingi wa mifumo ya rasilimali za Taifa. Anaposema haoni umuhimu wa Katiba anatufikirisha, anataka kusema mchakato wa Katiba uliogharimu mabilioni ya fedha leo hauna maana?”

Mbowe alisema umefika wakati mchakato wa Katiba uliokwama ukaendelezwa na hasa kuanzia katika rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti, Jaji mstaafu Joseph Warioba.

“Katiba ni maridhiano, tunahitaji kupata maridhiano ya pande zote, nirudie tu kwamba alichokisema Askofu Pengo kinasikitisha.”

Mbali ya Mbowe, Askofu Mwamalanga alisema suala la Katiba ni la Watanzania wote na si la mtu au kundi la watu hivyo mchakato huo unapaswa kuhitimishwa na si vinginevyo.

“Sisi mtazamo wetu, tuko pamoja na wale wanaotaka Katiba Mpya, suala la Katiba si la mtu mmoja. Mapambano ya ufisadi na rushwa yanapaswa kutambulika na Katiba na wananchi wanataka Katiba kwa nini wasipewe Katiba yao?

“Ni aibu kuona mabilioni yaliyotumika kwa Tume ya Jaji Warioba na Bunge Maalumu ya Katiba halafu mchakato unaishia juujuu. Nimshauri Rais (John) Magufuli kama anataka heshima kubwa ni huu mchakato uanzishwe kwani wananchi wanataka katiba yao.”

Pia, katibu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania, Sheikh Khamis Mataka ambaye aliomba kutoa maoni yake binafsi kuhusu mchakato huo wa Katiba alisema kinachopaswa kufanyika sasa ni jamii nzima kutafakari ni Katiba ipi ambayo wanaitaka.

“Vyama vya siasa, NGO (mashirika yasiyo ya kiserikali), kada za dini waendelee kuzungumza na kutafakari ni Katiba ipi tunaitaka, hii inayopendekezwa au turudi nyuma, unaweza kujiuliza ukiendelea na hii kwa kuipigia kura ya ndiyo au hapa, jibu litakuwa ni hapana hivyo tujadili ni Katiba ipi tunaitaka” alisema Sheikh Mataka ambaye pia ni msemaji wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata).

Kardinali Pengo Jumamosi iliyopita alinukuliwa akisema kauli iliyotolewa hivi karibuni na Askofu wa Jimbo la Rulenge-Ngara, Severine Niwemugizi kuwa Katiba mpya ndiyo kipaumbele cha wananchi ni maoni yake binafsi na si msimamo wa Kanisa Katoliki nchini.

Alisema hilo alipotoa ufafanuzi kuhusu sitofahamu iliyojitokeza miongoni mwa Watanzania na waumini wa kanisa hilo kutokana na kauli ya Askofu Niwemugizi.

“Napenda kutamka moja kwa moja kwamba huo si msimamo wa kanisa na hauwezi kuwa msimamo wa kanisa kwa sababu sisi tuna utaratibu wetu wa kuishauri Serikali au kuzungumzia masuala ya jamii,” alisema.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad