HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Tuesday, October 24, 2017

KESI YA LULU KUENDELEA TENA KESHA, MAHAKAMA YAAMURU ASKARI ALIYEANDIKA MAELEZO YA SHAHIDI WA PILI UPANDE WA UTETEZI KUFIKA MAHAKAMANI

Msanii maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu (aliyeshika kichwa) akiwa katika Mahakama kuu anakosomewa kesi yake ya kuua bila kukusudia.

 Na Karama Kenyunko, Globu ya jamii.

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imeamuru askari Polisi aliyechukua maelezo ya mke wa Dk. Wilbroad  Slaa, Josephine Mushumbus ambaye alipaswa kuwa shahidi wa pili wa upande wa  utetezi katika kesi ya mauaji bila kukusudia inayomkabili msanii maarufu wa filamu nchini, Elizabeth Michael maarufu kama Lulu kufika mahakamani hapo kesho kwa ajili ya utetezi.

Jaji Sam Rumanyika amesema hayo mapema leo October 24, wakati kesi hiyo ya mauji ya 'Lulu' dhidi ya msanii mwenzake, marehemu Steven Kanumba ilipokuja kwa ajili ya kusikiliza ushahidi wa upande wa utetezi.

 Jaji Rumanyika ametoa uamuzi huo, baada ya Wakili wa utetezi, Peter Kibatala kudai kuwa jitihada za kumpata Josephine Mshumbusi (mke wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema), zimeshindikana kwa kuwa yupo nje ya nchi na kuomba kusoma na kuyatoa maelezo hayo ili mahakama iyatumie kama kielelezo cha upande wa utetezi.

Wakili wa Serikali, Faraja George alipinga vikali maelezo hayo kusomwa na kutolewa na Kibatala akieleza kwamba Kibatala anazifahamu sheria hivyo alitegemea kwa kuwa aliyetoa maelezo polisi hapatikani, basi angeletwa askari aliyeandika maelezo hayo ili aweze kutoa taarifa hiyo.

Amedai kuwa Kibatala hana mamlaka ya kutoa taarifa hiyo wala kusoma kwani hawezi kuvaa kofia mbili kwa wakati mmoja, badala yake atabaki kumuwakilisha mteja wake hivyo afuate taratibu zilizowekwa.
Akitoa uamuzi huo, Jaji Rumanyika amesema swali la msingi ni nani atakayeitoa taarifa hiyo mahakamani kati ya wakili na aliyeandika maelezo.

"Kupatikana kwa shahidi imekuwa ngumu lakini anayepaswa kutoa maelezo hayo ni yule ambaye imeshindikana kufika mahakamani hapo na mwengine anayetakiwa kutoa maelezo hayo ni askari Polisi namba E 103 Nyangea. Hivyo, askari huyu anatakiwa kuja kesho kutoa maelezo na hati ya wito apatiwe," alisema Jaji Rumanyika.

Katika kesi ya msingi namba 125 ya mwaka 2012, inadaiwa kuwa Aprili 7,  2012 Sinza Vatican jijini Dar es Salaam, Lulu alimuua Msanii wa filamu, Steven Kanumba bila kukusudia.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad