HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Sunday, October 15, 2017

JAJI KAIJAGE AWATAKA WASIMAMIZI WA UCHAGUZI MDOGO KUZINGATIA SHERIA NA KANUNI ILI KUEPUKA KUISABABISHIA SERIKALI HASARA.

 Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji (R) Semistocles Kaijage akifungua  mafunzo kwa Wasimamizi na Wasimamizi wasaidizi wa Uchaguzi Mjini Dodoma leo. Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku tatu ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mdogo wa Kata 43 utakaofanyika Novemba 26 mwaka huu.
 Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Dodoma, James Karayemaha akiwasimamia wasimamizi na wasimamizi wasidizi wa uchaguzi kula kiapo cha utii wa kanuni na taratibu za uchaguzi kabla ya kuanza kwa mafunzo ya siku tatu yanayoratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) mjini Dodoma.
Wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wakila kiapo cha utii wa taratibu za uchaguzi kabla ya kuanza kwa mafunzo ya siku tatu yaliyoandaliwa na kuratibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Mjini Dodoma jana. (Picha na Abdulwakil Saiboko)


Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (R) Semistocles Kaijage amewataka wasimamizi wa uchaguzi mdogo wa madiwani kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi ili kuepuka kuisababishia serikali hasara.
Jaji Kaijage ameyasema hayo leo (Tarehe 15.10.2017) mjini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi.
“…Tusipozingatia na kufuata taratibu za uchaguzi tunaweza kusababisha kesi nyingi za uchaguzi na kuitumbukiza nchi katika gharama ambazo zingeweza kutumika katika huduma za jamii,” ameonya Jaji Kaijage.
Mhe. Kaijage amesema kuwa hamasa katika siasa za Tanzania imeongezeka sana na kwamba kumekua na ongezeko la hali ya kutokuaminiana haswa katika mchakato wa uchaguzi na kwamba endapo wasimamizi hawatafanya kazi yao kwa ufasaha wataitumbukiza nchi kwenye matatizo makubwa.
“Mmeaminiwa na kuteuliwa kwa sababu mna uwezo wa kufanya kazi hii, kitu cha muhimu ni kujiamini na kujitambua. Pia kuhakikisha mnayajua vyema maeneo yenu mnayofanyia kazi, kuhakikisha mnawatumia vizuri wasaidizi mlio nao kwa matokeo bora,” alisema.
Jaji Kaijage amewakumbusha washiriki wa mafunzo hayo juu ya jukumu lao la kuimarisha imani ya wananchi kwa NEC, na kwamba Imani hiyo itadumishwa endapo watafanya kazi kwa uwazi, uhuru na kwa ufanisi wa hali ya juu bila kuegemea upande wowote.
Ameogeza kusema kwamba uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali za kisheria na kikanuni zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa.
“Hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi kuwa mzuri, wenye ufanisi na usio na malalamiko au vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi kuanzia utoaji wa fomu, uteuzi wa wagombea, uratibu wa kampeni, upigaji kura, kuhesabu kura, kujumlisha hesabu za kura na kutangaza matokeo,” alisema.
Aidha, Jaji Kaijage, amewaasa wasimamizi wenye uzoefu kujiepusha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wazingatie mafunzo ambayo watapewa na tume pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria zinazosimamia uchaguzi.
Mkutano huo wa ufunguzi ulihudhuriwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Bw. Ramadhan Kailima na maafisa wa kada mbalimbali wa NEC  pamoja na wasimamizi, wasimaizi wasaidizi na maafisa wa uchaguzi 230 ambao walikula kiapo cha kuheshimu maadili ya uchaguzi.
Awali Bw. Kailima amesema kwamba uchaguzi mdogo umepangwa kufanyika kwenye Kata 43 tarehe 26 mwenzi Novemba, mwaka huu.
“Uchaguzi mdogo unafanyika kwenye Kata 43 ambazo zipo kwenye mikoa 19 kwenye Halmashauri 36 na Majimbo 37 kwa hiyo uchaguzi huu mdogo unafanyika karibia maeneo ya nchi nzima,” alisema Kailima
Uchaguzi huo unatarajiwa kuhusisha wapiga kura waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wapatao 336,182 katika jumla ya vituo vya kupigia kura 893 ambapo Kata yenye wapiga kura wengi wanafikia 58,622 na Kata yenye wapiga kura wachache wanafikia 1,402.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad