HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Saturday, October 28, 2017

HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA VIWE NA HUDUMA YA UCHUNGUZI WA SARATANI YA MATITI- WAZIRI UMMY



Meza kuu ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu watatu kutoka kushoto wakati alipofungua matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti, kulia kwa Mh. Waziri ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage na kushoto ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Grace Maghembe.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu aagiza Hospitali na Vituo vya Afya vyote vya Serikali nchini kuanzia kutoa huduma ya uchunguzi wa Saratani kila siku wakati wa kliniki ya mama na mtoto, sambamba na huduma hizi kila mwezi wanatakiwa kuwa na siku moja kwaajili ya kuchunguza na kufanya matibabu ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti.

Ameyasema hayo wakati alipofungua matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti, yalifunguliwa katika viwanja vya hospitali ya Ocean Road mapema leo jijini Dar es salaam.

Ummy ameipongeza kazi nzuri inayofanywa na Uongozi wa Hospitali ya Ocean Road katika kutimiza majukumu yake ikiwemo kuongeza vitanda 40 mpaka vitanda 100 kwa gharama zao kwaajili ya wagonjwa wa saratani pindi wanapopata huduma za matibabu ya Chemotherapy.

“Katika kuwaunga mkono Serikali ya awamu ya tano ya Mh. Magufuli imewapatia Bilioni 5 kwajili yakukamilisha mashine za kisasa za matibabu ya Saratani kwa kutumia mionzi.” alisema.

Ametoa maelekezo kwa Uongozi wa Hospitali ya Ocean Road kuwa wanatakiwa kwenda kwenye shule za Msingi na Sekondari ili kuwajengea watoto uelewa kuhusu ugonjwa wa Saratani, lakini ni vipi wataweza kujikinga na magonjwa yasiyo yakuambulizwa ikiwemo ugonjwa wa Saratani.

Pia ametoa rai kwa wananchi wote hususani wanawake kujitokeza kupima ugonjwa huo kwani unatibika endapo itagunduliwa mapema, Nae Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Grace Maghembe ambae pia alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar Es salaam ameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Raisi Dkt. John Pombe Magufuli kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto kwa kazi kubwa wanayoifanya ikiwemo kuongeza kwa bajeti ya Dawa , vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu.

Kwa upande mwingine Dkt. Grace Maghembe kwa niaba ya bodi ameahidi kuendelea kufanya kazi kwa uaminifu na bidii kubwa katika kuhakikisha kwamba wanakabiliana na ugonjwa huu wa Saratani kwa wananchi hasa wale wa hali ya chini na kuahidi kuendelea kuboresha huduma hii.

“Niwaombe wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam kwenda kupima Saratani kwani ni bure, usisubiri mpaka kuugua, ukichelewa grarama zinaongezeka lakini pia uwezekano wa kupona unakuwa ni mdogo”, alisema Dkt Maghembe

Aidha Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Ocean Road Dkt. Julius Mwaiselage amemhakikishia Waziri Ummy kwamba upatikanaji wa dawa katika Hospitali hiyo ni 80% na dawa za wagonjwa wengi zinapatikana kwa 100%, ukilinganisha na 2015/2016 upatikanaji wa dawa ilikuwa 4% tu, jambo ambalo lilikuwa ni changamoto kubwa na kufanya malalamiko ya dawa kuwa makubwa sana katika hospitali hiyo, hivyo kuishukuru Serikali ya Magufuli kwa niaba ya Waziri wa Afya Mh. Ummy Mwalimu.

Mwisho Dkt. Julius Mwaiselage amemhakikishia waziri kwamba Hospitali ya Ocean Road ipo katika hatua ya Mwisho ya kuweka mashine mpya mbili (Linear accerelators), hivyo zitasaidia kupunguza muda wa kusubiri kwa wagonjwa kusubiri huduma , lakini kubwa kupunguza wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akimkabidhi cheti moja ya wadau waliofanikisha matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti iliofanyika mapema leo katika viunga vya Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu wakirusha Maputo juu kuashiria ufunguzi rasmi wa matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti, iliofanyika katika viunga vya Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam
Wadau kutoka taasisi mbali mbali walioungana na Ummy Mwalimu na watumishi wa Hospitali ya Ocean Road katika matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti yaliyofanyika mapema leo jijini Dar es salaam.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akiambatana na Binti yake katika matembezi ya hisani ya kuhamasisha uchunguzi wa Saratani ya matiti yaliyofanyika mapema leo jijini Dar es salaam.Na WAMJWW







No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad