Na Mwandishi Wetu, Iringa
WAWEKEZAJI katika sekta ya kilimo na mifugo wamelalamikia ushindani
unaoletwa na bidhaa kutoka nje kutokana na serikali kushindwa
kuzidhibiti kwa njia ya kupunguza kodi na tozo mbalimbali katika
uzalishaji.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana wawekezaji hao ambao pia ni
sehemu ya wabia wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Kusini mwa Tanzania
(SAGCOT), wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
Kilimo, Mifugo, Maji na Umwagiliaji katika Kongani ya Ihemi mkoani
Iringa na Njombe, walisema ipo haja serikali ikaangalia suala hilo kwa
jicho pana ili kulinda bidhaa za ndani.
Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS Dairies Limited kilichopo
mkoani hapa, Bwana Fuad Abri alisema haiwezekani Tanzania iwe nchi ya
pili kwa idadi ya ng’ombe barani Afrika baada ya Ethiopia lakini bado
inapitwa katika uzalishaji na uingizaji maziwa nchini.
“Wenzetu Kenya wanazalisha lita 1,500,000 za maziwa kwa siku lakini
Tanzania inazalisha lita 120,000 kwa siku. Wakati huohuo sisi
tunawapita kwa umbali katika idadi ya ng’ombe, kama hiyo haitoshi
bidhaa za maziwa kutoka mataifa jirani zinaingia kwa wingi na kutoa
ushindani mkubwa na bidhaa za ndani,” alisema Bw. Abri.
Alisisitiza kuwa zipo namna nyingi za kuzuia ushindani huu kwa sababu
Serikali ya Kenya inashirikiana kwa kiasi kikubwa na wazalishaji
maziwa na ndiyo maana wana uwezo wa kusafirisha nje kwa bei shindani.
“Katika biashara hii ya maziwa kitu kikubwa kinachotakiwa kuangaliwa
ni namna gani unapata maziwa yako, bei utakayonunulia ikupe faida
lakini faida yenyewe iwe katika soko shindani,” alisema Bw. Abri.
Wabunge hao wakiongozwa na mwenyeji wao Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT,
Bwana Geofrey Kirenga ambapo kwa upande wao waliongozwa na kaimu
mwenyekiti wa kamati Bwana. Mashimba Ndaki, walitembelea kiwanda cha
kuzalisha chakula cha mifugo na ufugaji kuku wa nyama na mayai, Silver
Land kilichopo mkoani hapa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Bwana Jack
Bennie alisema mbali ya kuwepo na utaratibu wa kulipa kiasi kidogo cha
kodi kutokana na utaratibu wa kiuwekezaji lakini bado bidhaa za kuku
na chakula cha mifugo vinaathiri soko kutokana na kuzalishwa chini ya
kiwango lakini vingine vinaingia nchini na kuuzwa kwa bei ndogo
inayovuruga ushindani.
“Tumeamua kufanya uwezekazi mkubwa katika sekta hii ya mifugo, lakini
kuna tatizo la ushindani usioendana na uhalisia ambapo bidhaa kutoka
nje zilituathiri kwa kiasi kikubwa, tunashukuru kwa sasa serikali
imezuia kuingiza vifaranga vya kuku kutoka nje, tunaomba washikilie
hapohapo kwa sababu kukosekana kwa vifaranga hivyo kumesaidia
wazalishaji wa ndani kupata soko,” alisema Bwana Bennie.
Akizungumzia hali hiyo mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Dkt. Immaculate
Sware alisema wawekezaji wakubwa namna hiyo ni fursa kwa watanzania
hivyo serikali haina budi kuangalia namna ya kuwatengenezea mazingira
mazuri ya biashara ili walipe kodi vizuri lakini pia wanufaishe jamii.
“Tumetembelea miradi mingi iliyo katika ubia na SAGCOT, mradi huu wa
Silverlands ni mkubwa kwa hiyo tunapopata muda wa kusikiliza kero zao
inakua jambo jema kujua namna ya kuzifikisha ili zitatuliwe na
kusaidia jamii ambayo ndiyo wanufaika kwa njia nyingi ikiwemo kupata
ajira na kupata huduma au bidhaa,” alisema Dkt. Sware.
SAGCOT imeamua kuwatembeza wajumbe wa kamati hiyo ya bunge ili kuona
shughuli zinazofanyika katika kongani ya Ihemi ambayo ni miongoni mwa
kongani sita zilizopo katika kituo hicho. Maeneo mengi waliyotembelea
ni ile inayosimamia mnyororo wa ongezeko la thamani katika mazao ya
nyanya, viazi mviringo, soya na maziwa.
Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS Dairies Limited mkoani Iringa, Bwana Fuad Abri akitoa mada juu ya uendeshaji wa kiwanda chake na ubia wao na Kituo cha Kuendeleza kilimo Nyanda za juu kusini mwa Tanzania (SAGCOT) alipotembelewa na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo,Mifugo , Maji na Umwagiliaji. Lengo la ziara ya Kamati hiyo ni kujionea na kujifunza juu ya Kongani ya Ihemi na shughuli za SAGCOT.
Mkurugenzi wa kiwanda cha maziwa cha ASAS Dairies Limited, Bwana Fuad
Abri (kulia)akitoa
maelekezo ya uendeshaji wa kiwanda chake alipotembelewa na wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge Kilimo,Mifugo , maji na umwagiliaji. Ikiwa ni
sehemu ya ziara ya kamati hiyo kujionea na kujifunza juu ya kongani ya
Ihemi na shughuli mbalimbali za Mpango wa Kuendeleza Kilimo Nyanda za juu
kusini mwa Tanzania(SAGCOT). Wapili kulia ni Kaimu Mwenyekiti wa Kamati
hiyo ambaye pia ni mbunge wa Maswa Magharibi, Bwana Mashimba Ndaki. Watatu
kulia ni Mjumbe wa kamati ambaye pia Mbunge wa viti Maalum Bibi Khadija
Hassan Aboud. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT , Bwana Geoffrey Kirenga
No comments:
Post a Comment