HABARI MPYA

Home Top Ad

Post Top Ad

Wednesday, September 20, 2017

WALIMU WA SAYANSI LINDI WAIOMBA SERIKALI KUWASAIDIA.

 Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, Bi. Liberatha Alphonce, akionesha mfano wa picha iliyochorwa kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mchinga mkoani Lindi (hawapo pichani), ili kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi.
 Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mchinga mkoani Lindi, wakimsikiliza Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, Bi. Liberatha Alphonce (hayupo pichani) wakati akitoa mada kuhusu uhamasishaji wa masomo ya Sayansi kwa wasichana.
 Wahandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, wakisikiliza maoni kutoka kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mchinga mkoani Lindi walipotembelea shule hiyo kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi kwa wasichana.
 Baadhi ya Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mchinga mkoani Lindi, wakionesha ndoto zao kwa Wahandisi wa kike kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, walipotembelea shule hiyo kuhamasisha usomaji wa masomo ya Sayansi kwa wasichana.
 Mwanafunzi kutoka Shule ya Sekondari ya Lindi, akitoa maoni yake kuhusu changamoto  zinazokabili shule  yao kwa Wahandisi wa kike kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara.
Mhandisi kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, Bi. Rahma Mwinyi, akigawa zawadi ya madaftri kwa wanafunzi wa shule ya Mkonge mkoani Lindi ili  kuhamasisha wanafunzi  hao kupenda masomo ya sayansi.
 Wahandisi wa kike kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Mchinga mkoani Lindi.



Walimu wa masomo ya Sayansi mkoani Lindi wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka za kuandaa na kuimarisha miundombinu bora kwa shule za Sekondari zinazofundisha masomo hayo ili kuendeleza na kufufua vipaji vya wanafunzi.

Akizungumza kwa niaba ya walimu hao wakati wa ziara iliyofanywa na wahandisi wa kike kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara katika shule za mkoa huo,   Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mchinga iliyopo  mkoani humo, Bw. Makopa Selemani , amesisitiza kwa Serikali kuona namna ya kujenga maabara  nyingi za sayansi ambazo zitakuwa na vifaa na kuongeza walimu wa Sayansi ambao wameonekana kuwa ni wachache katika mkoa huo.
"Tunaiomba Serikali kutazama kwa jicho la pekee shule za mkoa huu hususan zenye michepuo ya sayansi kwani si kwamba wanafunzi hawapendi masomo haya bali miundombinu hairidhishi", amesema Mwalimu Mkuu.
Aidha, Mwalimu Mkuu ameongeza kuwa ili kuwasaidia wanafunzi wa kike katika mkoa huo serikali iwajengee mabweni wanafunzi hao ili kuepusha kupata vishawishi kwani wengi wao wanaishi mbali na shule.
Mwalimu Mkuu Selemani, ameelezea baadhi ya mikakati ya shule yake katika kuhamasisha wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi ikiwemo kufanya vikao vya mara kwa mara na wanafunzi hao ili kujadili changamoto zao na kuzitatua.
Ametoa wito kwa Wizara kufanya ziara za mara kwa mara katika shule mbalimbali nchini ili kuhamasisha wanafunzi husasan wa kike kupenda na kujifunza masomo ya sayansi ambayo yameonekana kuwa ni vikwazo katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mhandisi  kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara, Bi Liberatha  Alphonce,  amewasisitiza wanafunzi  wa kike mkoani humo kuanza kujituma na kujijengea misingi imara ya kupenda masomo ya sayansi wakiwa katika ngazi za awali ili kufikia malengo yao.
Amefafanua kuwa masomo ya Sayansi yanatoa fursa za kujiajiri na urahisi wa kupata mikopo kwa wanafunzi wanaochaguliwa kujiunga na elimu ya juu.
Naye, mwanafunzi Shamira Salum, kutoka shule ya Sekondari ya Mchinga, ameiomba serikali kuongeza walimu na vifaa katika shule za mkoa huo ili kuweza kutimiza malengo yao ya kuwa wahandisi na madaktari wa baadae.
Ziara ya wahandisi wa kike kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), kupitia Kitengo maalum cha ushirikishwaji wa wanawake katika masuala ya barabara imelenga kutoa elimu na kuhamasisha wanafunzi wa kike nchini kusoma masomo ya sayansi ambapo pamoja na mambo mengine wahandisi hao wametembelea shule ya sekondari ya Mchinga, Lindi, Mkonge na Mingoyo ambazo zipo mkoani Lindi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad