HABARI MPYA

Home Top AdPost Top Ad

Friday, 8 September 2017

UTAPIAMLO NI JANGA LA KITAIFA – DK. MPANGO

 WAZIRI wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango amesema utapiamlo ni janga la Kitaifa na kwamba theluthi moja ya vifo nchini inasababishwa na tatizo hilo.

Ametoa kauli hiyo juzi jioni (Jumatano, Septemba 6, 2017) wakati akitoa nasaha kwenye mkutano wa nne wa mwaka wa wadau wa lishe wa kutathmini afua za lishe nchini kwenye ukumbi wa Hazina mjini Dodoma.

“Haipendezi kuona katika kila watoto 100, watoto 34 wana udumavu wa akili na katika kila watoto 100, watoto 59 wenye umri kati ya miezi sita na miaka mitano wana upungufu mkubwa wa damu,” alisema. Alisema Serikali inatumia asilimia mbili ya pato la Taifa sawa na dola za Marekani milioni 518 kununua dawa za vitamin A na folic acid (vidonge vya kuongeza damu).

Alisema kuna haja ya kubuni mbinu za kilimo ambazo zitainua kiwango cha upatikanaji wa lishe nchini (nutrition smart agriculture) kama njia ya kudumu ya kukabili tatizo la utapiamlo na udumavu.

Amesema kwa vile Serikali imetenga sh. bilioni 11 ili kukabiliana na utapiamlo, wizara yake itahakikisha inatafuta fedha zilizotengwa na hata ikibidi kutafuta fedha na misaada ya kitaalamu kutoka nje ya nchi ili kuhakikisha suala hilo linatekelezwa.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bw. Selemani Jaffo aliziagiza Halmashauri zote nchini zitoe taarifa za kila mwezi za matumizi ya fedha za afua ya lishe kwenye Kamati zake za Fedha. “Hizi fedha si za kufanya masikhara, Serikali iko committed katika suala hili,” alisema.

“Zamani katika bajeti za Halmashauri tulikuwa tukitenga sh. 500 kwa kila mtoto, lakini katika bajeti ya mwaka 2017/2018 tumetenga sh. 1,000 kwa kila mtoto, ambazo ni sawa na sh. bilioni 11 kwa mwaka,” alisema wakati alipopewa fursa ya kutoa nasaha zake.

“Wiki iliyopita, Makamu wa Rais alituagiza tuandike performance contracts kwa Wakuu wote wa Mikoa nchini ili tuweze kufuatilia utekelezaji wao katika suala zima za kuboresha upatikanaji wa lishe nchini. Kazi hiyo tumeshaianza na tarehe 22 Septemba, 2017 itakuwa ni siku ya mwisho ya kukamilisha zoezi hilo,” alisema.

Bw. Jaffo aliwataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya waifanye ajenda ya afya ya lishe kuwa kipaumbele chao.

Wakati huohuo, Naibu Waziri Jaffo amesema kuwa maafisa lishe 660 wataajiriwa nchini kote hivi karibuni. Amesema waliopo hivi sasa ni wataalamu 121 tu ambao kati yao 17 wako mikoani na 104 wako kwenye Halmashauri mbalimbali.

Naye Mkurugenzi wa USAID hapa nchini, Bw. Andrew Karas aliipongeza Serikali kwa uamuzi wake wa kuchukua umiliki na usimamizi wa masuala ya lishe ikiwa ni hatua muhimu ya uratibu wa suala hilo baina ya wahisani, wadau na Serikali.

Alisema ushirikishwaji wa wadau ni suala muhimu na ambalo haliepukiki lakini akaonya kuwa kuna haja ya kuangalia namna ya kuongeza uwezo wadau kwa vitendo ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Lengo leni ni letu, na kipaumbele chenu ni chetu. Tukisaidiana tutaweza kufanikisha suala la kuongeza lishe na kupunguza atahari za utapiamlo hapa nchini,” alisema Bw. Karas kwa Kiswahili fasaha na kuamsha shangwe katika ukumbi huo.

Bw. Karas ambaye alizungumza kwa Kiswahili kwa zaidi ya dakika tano, alikuwa akitoa salamu kutoka mtandao wa wahisani wa wenye lengo la kufuta utapiamlo kwa kuboresha lishe nchini (Scaling Up Nutrition -SUN) ambao unajumuisha mashirika ya Children Investment Fund, DfID, Umoja wa Ulaya (EU), Global Affairs Canada, Irish Aid na USAID.

Naye Mwakilishi Mkazi wa UNICEF, Bibi Maniza Zaman, akitoa salamu kwa niaba ya mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliyo chini ya mtandao wa SUN, alisema kufutwa kwa utapiamlo na kuimarishwa kwa uapikanaji wa lishe bora nchini kunaenda sambamba na utekelezaji wa malengo 17 endelevu ya maendeleo.

“Kipengele kimojawapo kikidumaa, kinakwamisha utendaji kazi wa kingine,” alisema na kuongeza: “Mpango uliozinduliwa unahitaji kuwa na fedha za uhakika ili uweze kutekelezeka. Inatia moyo kuona Halmashauri na Sekretarieti za Mikoa zimetenga bajeti kwa ajili ya mpago huu.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Masuala ya Lishe Tanzania (Partnership for Nutrition in Tanzania - PANITA), Bw. Tumaini Mikindo aliiomba Serikali iziwekee uzio maalum wa kibajeti (ring-fence) fedha za masuala ya lishe ili kuzilinda zisitumike kinyume na matumizi yaliyopangwa.

“Tunaomba fedha za kasama ya lishe ziwe ring-fenced ili ziweze kutumika kama zilivyopangwa. Watendaji watakaofanya vizuri wapongezwe na wale watakaoharibu wachukuliwa hatua za kinidhamu kwa sababu wanataka kuua Taifa letu,” alisema wakati akitoa salamu kwa niaba ya mashirika yasiyokuwa ya Serikali zaidi ya 300 yaliyo chini ya mtandao wa SUN.

Alisema mtandao wao umeenea nchi nzima na akiomba Serikali ilisimamie suala la kupambana na utapiamlo na kuboresha lishe kwa wananchi wake kama ambavyo ilisimamia suala la uhaba wa madawati nchini.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 DODOMA, 
IJUMAA, SEPTEMBA 8, 2017.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad